Yohana 19
19
Isa ahukumiwa kusulubiwa
(Mathayo 27:15-31; Marko 15:6-20; Luka 23:13-25)
1Ndipo Pilato akamtoa Isa akaamuru apigwe mijeledi. 2Askari wakasokota taji la miiba, wakamvika Isa kichwani. Wakamvalisha joho la zambarau. 3Wakawa wanapanda pale alipo tena na tena, wakisema, “Salamu, mfalme wa Wayahudi!” Huku wakimpiga makofi usoni.
4Pilato akatoka tena nje, akawaambia wale waliokusanyika, “Tazameni, namkabidhi Isa kwenu kuwajulisha kwamba mimi sioni msingi wowote wa kumshtaki.” 5Kwa hiyo Isa akatoka nje akiwa amevaa lile taji la miiba na lile vazi la zambarau. Pilato akawaambia, “Tazameni, mtu ndiye huyu!”
6Wale viongozi wa makuhani na maafisa walipomwona, wakapiga kelele wakisema, “Msulubishe! Msulubishe!”
Pilato akawaambia, “Mchukueni ninyi mkamsulubishe. Lakini mimi sioni msingi wowote wa kumshtaki.”
7Viongozi wa Wayahudi wakamjibu, “Sisi tunayo sheria, na kutokana na sheria hiyo, hana budi kufa kwa sababu yeye alijiita Mwana wa Mungu#19:7 Yaani Mwana wa asili moja na Mwenyezi Mungu (Yohana 1:1-2), wa kiroho, bali si wa kimwili..”
8Pilato aliposikia haya, akaogopa zaidi. 9Akaingia tena ndani ya jumba la kifalme, akamuuliza Isa, “Wewe umetoka wapi?” Lakini Isa hakumjibu. 10Pilato akamwambia, “Wewe unakataa kuongea na mimi? Hujui ya kuwa nina mamlaka ya kukuachia huru au kukusulubisha?”
11Ndipo Isa akamwambia, “Wewe hungekuwa na mamlaka yoyote juu yangu kama hungepewa kutoka juu. Kwa hiyo yeye aliyenitia mikononi mwako ana hatia ya dhambi iliyo kubwa zaidi.”
12Tangu wakati huo, Pilato akajitahidi kutafuta njia ya kumfungua Isa, lakini viongozi wa Wayahudi wakazidi kupiga kelele wakisema, “Ukimwachia huyu mtu, wewe si rafiki wa Kaisari. Mtu yeyote anayedai kuwa mfalme anampinga Kaisari.”
13Pilato aliposikia maneno haya, akamtoa Isa nje tena. Akaketi kwenye kiti chake cha hukumu, mahali palipoitwa Sakafu ya Jiwe (kwa Kiebrania ni Gabatha). 14Basi ilikuwa siku ya Maandalio ya Pasaka, yapata kama saa sita hivi.
Pilato akawaambia Wayahudi, “Huyu hapa mfalme wenu!”
15Wao wakapiga kelele, “Mwondoe! Mwondoe! Msulubishe!”
Pilato akawauliza, “Je, nimsulubishe mfalme wenu?”
Wale viongozi wa makuhani wakamjibu, “Sisi hatuna mfalme mwingine ila Kaisari.”
16Ndipo Pilato akamkabidhi Isa kwao ili wamsulubishe.
Isa asulubishwa
(Mathayo 27:32-44; Marko 15:21-32; Luka 23:26-43)
Kwa hiyo askari wakamchukua Isa. 17Isa, akiwa ameubeba msalaba wake, akatoka kuelekea mahali palipoitwa Fuvu la Kichwa (kwa Kiebrania ni Golgotha). 18Hapo ndipo walipomsulubisha. Pamoja naye walisulubisha watu wawili, mmoja kila upande wake, naye Isa katikati.
19Pilato akaamuru tangazo liandikwe na liwekwe juu kwenye msalaba wa Isa; likasema:
Isa Al-Nasiri
Mfalme wa Wayahudi.
20Kwa kuwa mahali hapo Isa aliposulubiwa palikuwa karibu na mjini, Wayahudi wengi walisoma maandishi haya yaliyokuwa yameandikwa kwa lugha za Kiebrania, Kiyunani na Kilatini. 21Viongozi wa makuhani wa Wayahudi wakapinga, wakamwambia Pilato, “Usiandike ‘Mfalme wa Wayahudi,’ bali andika kwamba mtu huyu alisema yeye ni mfalme wa Wayahudi.”
22Pilato akawajibu, “Nilichokwisha kuandika, nimeandika!”
Mavazi ya Isa yagawanywa
23Askari walipokwisha kumsulubisha Isa, walichukua nguo zake wakazigawa mafungu manne, kila askari fungu lake. Ila walikubaliana wasilichane lile vazi lake kwa maana lilikuwa halina mshono, bali limefumwa tangu juu hadi chini.
24Wakaambiana, “Tusilichane ila tulipigie kura ili kuamua ni nani atalichukua.”#19:24 Zaburi 22:18
Hili lilitukia ili Maandiko yapate kutimizwa yale yaliyosema,
“Wanagawana nguo zangu,
na vazi langu wanalipigia kura.”
Hayo ndiyo waliyoyafanya wale askari.
25Karibu na msalaba wa Isa walikuwa wamesimama mama yake, na dada wa mamaye, na Mariamu mke wa Klopa, na Mariamu Magdalene. 26Isa alipomwona mama yake mahali pale, na yule mwanafunzi aliyempenda akiwa amesimama karibu, Isa akamwambia mama yake, “Mama, huyu hapa ndiye mwanao.” 27Kisha akamwambia yule mwanafunzi, “Nawe huyu hapa ndiye mama yako.” Tangu wakati huo yule mwanafunzi akamchukua mama yake Isa nyumbani mwake.
Kifo cha Isa
(Mathayo 27:45-56; Marko 15:33-41; Luka 23:44-49)
28Baada ya haya, akijua kuwa mambo yote yamemalizika, na ili kutimiza Maandiko, Isa akasema, “Naona kiu.” 29Hapo palikuwa na bakuli lililojaa siki. Kwa hiyo wakachovya sifongo kwenye hiyo siki, wakaiweka kwenye ufito wa mti wa hisopo, wakampelekea mdomoni. 30Baada ya kuionja hiyo siki, Isa akasema, “Imekwisha.” Akainamisha kichwa chake, akaitoa roho yake.
Isa achomwa mkuki ubavuni
31Ilikuwa siku ya Maandalio ya Pasaka, na siku iliyofuata ingekuwa Sabato maalum. Kwa kuwa viongozi wa Wayahudi hawakutaka miili ibaki msalabani siku ya Sabato, wakamwomba Pilato aamuru miguu ya wale waliosulubiwa ivunjwe, na miili iondolewe kwenye misalaba. 32Kwa hiyo askari wakaenda wakavunja miguu ya mtu wa kwanza aliyesulubiwa pamoja na Isa, na ya yule mwingine pia. 33Lakini walipomkaribia Isa, wakaona ya kuwa amekwisha kufa, hivyo hawakuvunja miguu yake. 34Badala yake mmoja wa wale askari akamchoma mkuki ubavuni, na mara pakatoka damu na maji. 35Mtu aliyeona mambo hayo ndiye alitoa ushuhuda, nao ushuhuda wake ni kweli. Anajua kuwa anasema kweli, naye anashuhudia ili pia nanyi mpate kuamini. 36Kwa maana mambo haya yalitukia ili andiko litimie, lisemalo, “Hakuna hata mfupa wake mmoja utakaovunjwa.”#19:36 Kutoka 12:46; Hesabu 9:12; Zaburi 34:20 37Tena andiko lingine lasema, “Watamtazama yeye waliyemchoma.”#19:37 Zekaria 12:10
Maziko ya Isa
(Mathayo 27:57-61; Marko 15:42-47; Luka 23:50-56)
38Baada ya mambo haya, Yusufu wa Arimathaya, aliyekuwa mfuasi wa Isa, ingawa kwa siri kwa sababu ya kuwaogopa viongozi wa Wayahudi, alimwomba Pilato ruhusa ili kuuchukua mwili wa Isa. Pilato alimruhusu, hivyo akaja, akauchukua. 39Naye Nikodemo, yule ambaye kwanza alimwendea Isa usiku, akaja, akaleta mchanganyiko wa manemane na manukato, yenye uzito wa zaidi ya kilo thelathini. 40Wakauchukua mwili wa Isa, wakaufunga katika sanda ya kitani safi pamoja na yale manukato, kama ilivyokuwa desturi ya Wayahudi. 41Basi palikuwa na bustani karibu na mahali pale aliposulubiwa, na pale ndani ya ile bustani palikuwa na kaburi jipya, ambalo halikuwa limezikiwa mtu bado. 42Kwa hiyo, kwa kuwa ilikuwa siku ya Wayahudi ya Maandalio, nalo kaburi hilo lilikuwa karibu, wakamzika Isa humo.
Currently Selected:
Yohana 19: NENO
Highlight
Share
Copy
Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.