Yohana 5
5
Isa Amponya Mtu Kwenye Bwawa La Bethzatha
1 Baada ya haya, kulikuwa na Sikukuu ya Wayahudi, naye Isa akapanda kwenda Yerusalemu. 2 Huko Yerusalemu, karibu na mlango uitwao Mlango wa Kondoo, palikuwa na bwawa moja lililoitwa kwa Kiebrania Bethzatha,#5:2 Bethzatha ni neno la Kiebrania ambalo maana yake ni Nyumba ya mizeituni; mahali pengine limetajwa kama Bethesda kwa Kiaramu, yaani Nyumba ya huruma, na pengine kama Bethsaida, yaani Nyumba ya uvuvi. ambalo lilikuwa limezungukwa na kumbi tano. 3Hapa palikuwa na idadi kubwa ya wasiojiweza, yaani, vipofu, viwete, na waliopooza [wakingojea maji yatibuliwe. 4Kwa maana malaika alikuwa akishuka wakati fulani, akayatibua maji. Yule aliyekuwa wa kwanza kuingia ndani baada ya maji kutibuliwa alipona ugonjwa wowote aliokuwa nao]. 5Mtu mmoja alikuwako huko ambaye alikuwa ameugua kwa miaka thelathini na minane. 6Isa alipomwona akiwa amelala hapo, naye akijua kuwa amekuwa hapo kwa muda mrefu, akamwambia, “Je, wataka kuponywa?”
7Yule mgonjwa akamjibu, “Bwana,#5:7 Wale ambao hawakumfahamu Isa kuwa Masihi walimwita “Bwana” kwa heshima ya kawaida. mimi sina mtu wa kuniingiza bwawani maji yanapotibuliwa. Nami ninapotaka kutumbukia bwawani, mtu mwingine huingia kabla yangu.”
8 Isa akamwambia, “Inuka, chukua mkeka wako, uende.” 9 Mara yule mtu akapona, akachukua mkeka wake, akaanza kutembea.
Basi siku hiyo ilikuwa siku ya Sabato. 10 Kwa hiyo Wayahudi wakamwambia yule mtu aliyeponywa, “Leo ni Sabato, si halali wewe kubeba mkeka wako.”
11Yeye akawajibu, “Yule mtu aliyeniponya aliniambia, ‘Chukua mkeka wako na uende.’ ”
12 Wakamuuliza, “Ni mtu gani huyo aliyekuambia uchukue mkeka wako uende?”
13Basi yule mtu aliyeponywa hakufahamu ni nani aliyemponya, kwa sababu Isa alikuwa amejiondoa katika ule umati wa watu uliokuwa hapo.
14 Baadaye Isa akamkuta yule mtu aliyemponya ndani ya Hekalu na kumwambia, “Tazama umeponywa, usitende dhambi tena. La sivyo, lisije likakupata jambo baya zaidi.” 15 Yule mtu akaenda, akawaambia wale Wayahudi kuwa ni Isa aliyemponya.
Uzima Kupitia Mwana
16 Kwa hiyo Wayahudi wakaanza kumsumbua Isa, kwa sababu alikuwa anafanya mambo kama hayo siku ya Sabato. 17 Isa akawajibu, “Baba#5:17 Jina Baba linaonyesha uhusiano maalum wa Isa na Mwenyezi Mungu. yangu anafanya kazi yake daima hata siku hii ya leo, nami pia ninafanya kazi.” 18 Maneno haya yaliwaudhi sana viongozi wa Wayahudi. Wakajaribu kila njia wapate jinsi ya kumuua, kwani si kwamba alivunja Sabato tu, bali alikuwa akimwita Mungu Baba yake, hivyo kujifanya sawa na Mungu.
Mamlaka Ya Mwana Wa Mungu
19 Isa akawaambia, “Amin, amin nawaambia, Mwana hawezi kufanya jambo lolote peke yake, yeye aweza tu kufanya lile analomwona Baba yake akifanya, kwa maana lolote afanyalo Baba, Mwana pia hufanya vivyo hivyo. 20 Baba ampenda Mwana na kumwonyesha yale ambayo yeye Baba mwenyewe anayafanya, naye atamwonyesha kazi kuu kuliko hizi ili mpate kushangaa. 21 Hakika kama vile Baba awafufuavyo wafu na kuwapa uzima, vivyo hivyo Mwana huwapa uzima wale anaopenda. 22 Wala Baba hamhukumu mtu yeyote, lakini hukumu yote amempa Mwana, 23 ili wote wamheshimu Mwana kama vile wanavyomheshimu Baba. Yeyote asiyemheshimu Mwana, hamheshimu Baba aliyemtuma.
24 “Amin, amin nawaambia, yeyote anayesikia maneno yangu na kumwamini yeye aliyenituma, anao uzima wa milele, naye hatahukumiwa, bali amepita kutoka mautini, na kuingia uzimani. 25 Amin, amin nawaambia, saa yaja, nayo saa ipo, wafu watakapoisikia sauti ya Mwana wa Mungu,#5:25 Yaani Mwana wa asili moja na Mwenyezi Mungu (Yn 1:1-2), wa kiroho, bali si wa kimwili. nao watakaoisikia watakuwa hai. 26 Kama vile Baba alivyo na uzima ndani yake, vivyo hivyo amempa Mwana kuwa na uzima ndani yake. 27 Naye amempa Mwanawe mamlaka ya kuhukumu kwa kuwa yeye ni Mwana wa Adamu.
28 “Msishangae kusikia haya, kwa maana saa inakuja ambapo wale walio makaburini wataisikia sauti yake. 29 Nao watatoka nje, wale waliotenda mema watafufuka wapate uzima na wale waliotenda maovu, watafufuka wahukumiwe.
Shuhuda Kuhusu Isa
30 “Mimi siwezi kufanya jambo lolote peke yangu. Ninavyosikia ndivyo ninavyohukumu, nayo hukumu yangu ni ya haki kwa kuwa sitafuti kufanya mapenzi yangu mwenyewe, bali mapenzi yake yeye aliyenituma.
31 “Kama ningejishuhudia mimi mwenyewe, ushuhuda wangu si kweli. 32 Lakini yuko mwingine anishuhudiaye na ninajua kwamba ushuhuda wake ni wa kweli.
33 “Mlituma wajumbe kwa Yahya, naye akashuhudia juu ya kweli. 34 Si kwamba naukubali ushuhuda wa mwanadamu, la, bali ninalitaja hili kusudi ninyi mpate kuokolewa. 35 Yahya alikuwa taa iliyowaka na kutoa nuru, nanyi kwa muda mlichagua kuifurahia nuru yake.
36 “Lakini ninao ushuhuda mkuu zaidi kuliko wa Yahya. Kazi zile nizifanyazo, zinashuhudia juu yangu, zile ambazo Baba amenituma nizikamilishe, naam, ishara hizi ninazofanya, zinashuhudia kuwa Baba ndiye alinituma. 37 Naye Baba mwenyewe ameshuhudia juu yangu. Hamjapata kamwe kuisikia sauti yake wala kuona umbo lake, 38 wala hamna neno lake ndani yenu, kwa sababu hamkumwamini yeye aliyetumwa naye. 39 Ninyi mnachunguza Maandiko mkidhani ya kuwa ndani yake mna uzima wa milele, maandiko haya ndiyo yanayonishuhudia Mimi. 40 Lakini mnakataa kuja kwangu ili mpate uzima.
41 “Mimi sitafuti kutukuzwa na wanadamu. 42Lakini ninajua kwamba hamna upendo wa Mungu mioyoni mwenu. 43Mimi nimekuja kwa jina la Baba yangu, nanyi hamnipokei, lakini mtu mwingine akija kwa jina lake mwenyewe, mtampokea. 44 Ninyi mwawezaje kuamini ikiwa mnapeana utukufu ninyi kwa ninyi, lakini hamna bidii kupata utukufu utokao kwa Mungu?
45 “Lakini msidhani kuwa mimi nitawashtaki mbele za Baba, mshtaki wenu ni Musa, ambaye mmemwekea tumaini lenu. 46 Kama mngelimwamini Musa, mngeliniamini na mimi kwa maana aliandika habari zangu. 47 Lakini ikiwa hamwamini aliyoandika Musa, mtaaminije ninayoyasema?”
Currently Selected:
Yohana 5: NMM
Highlight
Share
Copy
Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018 by Biblica, Inc.
Used with permission.
All rights reserved worldwide.