YouVersion Logo
Search Icon

Luka 22

22
Kufa na kufufuka kwa Isa
(Luka 22:1–24:53)
Yuda akubali kumsaliti Isa
(Mathayo 26:14-16; Marko 14:10-11)
1Wakati huu Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu, iitwayo Pasaka, ilikuwa imekaribia. 2Viongozi wa makuhani na walimu wa Torati walikuwa wanatafuta njia ya kumuua Isa, kwa sababu waliwaogopa watu. 3Shetani akamwingia Yuda, aliyeitwa Iskariote, mmoja wa wale kumi na wawili. 4Yuda akaenda kwa viongozi wa makuhani na kwa maafisa wa walinzi wa Hekalu, akazungumza nao jinsi angeweza kumsaliti Isa. 5Wakafurahi na wakakubaliana kumpa fedha. 6Naye akakubali, akaanza kutafuta wakati uliofaa wa kumsaliti Isa kwao, ambapo hakuna umati wa watu.
Maandalizi ya Pasaka
(Mathayo 26:17-25; Marko 14:12-21; Yohana 13:21-30)
7Basi ikawadia siku ya Mikate Isiyotiwa Chachu, siku ambayo mwana-kondoo wa Pasaka huchinjwa. 8Hivyo Isa akawatuma Petro na Yohana, akisema, “Nendeni mkatuandalie chakula cha Pasaka ili tuweze kuila.”
9Wakamuuliza, “Unataka tukuandalie wapi?”
10Isa akawaambia, “Tazameni, mtakapokuwa mkiingia mjini, mtakutana na mwanaume amebeba mtungi wa maji. Mfuateni hadi kwenye nyumba atakayoingia. 11Nanyi mwambieni mwenye nyumba, ‘Mwalimu anauliza: Kiko wapi chumba cha wageni, ambamo mimi na wanafunzi wangu tutakula Pasaka?’ 12Atawaonesha chumba kikubwa ghorofani, kikiwa kimepambwa vizuri. Andaeni humo.”
13Wakaenda, nao wakakuta kila kitu kama Isa alivyowaambia. Hivyo wakaiandaa Pasaka.
Kuanzishwa kwa Chakula cha Bwana Isa
(Mathayo 26:31-35; Marko 14:27-31; Yohana 13:36-38)
14Wakati ulipowadia, Isa akaketi mezani pamoja na wale mitume wake. 15Kisha akawaambia, “Nimetamani sana kuila Pasaka hii pamoja nanyi kabla ya kuteswa kwangu. 16Kwa maana, nawaambia, sitaila tena Pasaka hadi itakapotimizwa katika ufalme wa Mungu.”
17Baada ya kukichukua kikombe, akashukuru, akasema, “Chukueni hiki mnywe wote. 18Kwa maana nawaambia tangu sasa sitakunywa tena katika uzao wa mzabibu, hadi ufalme wa Mungu utakapokuja.”
19Kisha akachukua mkate, akashukuru, akaumega, na kuwapa, akisema, “Huu ni mwili wangu unaotolewa kwa ajili yenu. Fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu.”
20Vivyo hivyo baada ya kula, akakitwaa kikombe, akisema, “Kikombe hiki ni agano jipya katika damu yangu, imwagikayo kwa ajili yenu. 21Lakini mkono wake huyo atakayenisaliti uko hapa mezani pamoja nami. 22Mwana wa Adamu anaenda zake kama ilivyokusudiwa. Lakini ole wake mtu huyo amsalitiye!” 23Wakaanza kuulizana wenyewe ni nani miongoni mwao angeweza kufanya jambo hilo.
Mabishano kuhusu ukuu
(Mathayo 18:1-5; Marko 9:33-37; Luka 9:46-48)
24Pia yakazuka mabishano katikati ya wanafunzi kwamba ni nani aliyeonekana kuwa mkuu kuliko wote miongoni mwao. 25Isa akawaambia, “Wafalme na watu wa Mataifa huwatawala watu kwa nguvu. Nao wenye mamlaka juu yao hujiita ‘Wafadhili.’ 26Lakini ninyi msifanane nao. Bali yeye aliye mkuu kuliko wote miongoni mwenu, inampasa kuwa kama yeye aliye mdogo wa wote, naye anayetawala na awe kama yeye anayehudumu. 27Kwani ni nani aliye mkuu? Ni yule anayeketi mezani au ni yule anayehudumu? Si ni yule aliyeketi mezani? Lakini mimi niko miongoni mwenu kama yule anayehudumu. 28Ninyi mmekuwa pamoja nami katika majaribu yangu. 29Nami kama Baba#22:29 Jina Baba linaonesha uhusiano maalum wa Isa na Mwenyezi Mungu. yangu alivyonipa ufalme, nami ninawapa ninyi, 30ili mpate kula na kunywa mezani pangu katika karamu ya ufalme wangu, na kukaa katika viti vya utawala, mkihukumu makabila kumi na mawili ya Israeli.”
Isa atabiri kuwa Petro atamkana
(Mathayo 26:31-35; Marko 14:27-31; Yohana 13:31-38)
31Isa akasema, “Simoni, Simoni, sikiliza, Shetani ameomba kuwapepeta ninyi wote kama ngano. 32Lakini nimekuombea wewe Simoni ili imani yako isishindwe, nawe baada ya kunirudia, uwaimarishe ndugu zako.”
33Petro akajibu, “Bwana, niko tayari kwenda pamoja nawe gerezani na hata katika kifo.”
34Isa akamjibu, “Ninakuambia Petro, kabla jogoo hajawika usiku wa leo, utakana mara tatu kwamba unanijua.”
Mfuko, mkoba na upanga
35Kisha Isa akawauliza, “Nilipowatuma bila mfuko, wala mkoba, wala viatu, mlipungukiwa na kitu chochote?”
Wakajibu, “La, hatukupungukiwa na kitu chochote.”
36Akawaambia, “Lakini sasa, aliye na mfuko na auchukue, na aliye na mkoba vivyo hivyo. Naye asiye na upanga, auze joho lake anunue mmoja. 37Kwa sababu, nawaambia, andiko hili lazima litimizwe kunihusu, kwamba, ‘Alihesabiwa pamoja na wakosaji’; kwa kweli yaliyoandikwa kunihusu hayana budi kutimizwa.”
38Wanafunzi wake wakamwambia, “Bwana, tazama hapa kuna panga mbili.”
Akawajibu, “Inatosha.”
Isa aomba kwenye Mlima wa Mizeituni
(Mathayo 26:36-46; Marko 14:32-42)
39Isa akatoka, akaenda kwenye Mlima wa Mizeituni kama ilivyokuwa kawaida yake, nao wanafunzi wake wakamfuata. 40Walipofika huko, akawaambia wanafunzi wake, “Ombeni, msije mkaingia majaribuni.” 41Akajitenga nao kama umbali wa kutupa jiwe, akapiga magoti, akaomba 42akisema, “Baba, kama ni mapenzi yako, niondolee kikombe hiki. Lakini si kama nipendavyo, bali mapenzi yako yatendeke.” 43Malaika kutoka mbinguni akamtokea, akamtia nguvu. 44Naye akiwa katika maumivu makuu, akaomba kwa bidii, nalo jasho lake likawa kama matone ya damu yakidondoka ardhini.
45Baada ya kuomba, akawarudia wanafunzi wake akawakuta wamelala, wakiwa wamechoka kutokana na huzuni. 46Naye akawauliza, “Mbona mmelala? Amkeni, mwombe ili msije mkaingia majaribuni.”
Isa akamatwa
(Mathayo 26:47-56; Marko 14:43-50; Yohana 18:1-11)
47Isa alipokuwa bado anazungumza, umati mkubwa wa watu wakaja. Waliongozwa na Yuda, aliyekuwa mmoja wa wale kumi na wawili. Akamkaribia Isa ili ambusu. 48Lakini Isa akamwambia, “Yuda, je, unamsaliti Mwana wa Adamu kwa busu?”
49Wafuasi wa Isa walipoona yale yaliyokuwa yanakaribia kutokea, wakasema, “Bwana, tuwakatekate kwa panga zetu?” 50Mmoja wao akampiga mtumishi wa kuhani mkuu kwa upanga, akamkata sikio la kuume.
51Lakini Isa akasema, “Acheni!” Akaligusa lile sikio la yule mtu na kumponya.
52Kisha Isa akawaambia wale viongozi wa makuhani, maafisa wa walinzi wa Hekalu, pamoja na wazee waliokuwa wamekuja kumkamata, “Mmekuja na panga na marungu, kana kwamba mimi ni mnyang’anyi? 53Kila siku nilikuwa pamoja nanyi Hekaluni lakini hamkunikamata. Lakini hii ni saa yenu, wakati giza linatawala!”
Petro amkana Isa
(Mathayo 26:57-75; Marko 14:53-72; Yohana 18:12-27)
54Kisha wakamkamata Isa, wakamchukua, wakaenda naye hadi nyumbani mwa kuhani mkuu. Lakini Petro akafuata kwa mbali. 55Walipokwisha kuwasha moto katikati ya ua na kuketi pamoja, Petro naye akaketi pamoja nao. 56Mjakazi mmoja akamwona kwa mwanga wa moto akiwa ameketi pale. Akamtazama sana, akasema, “Huyu mtu pia alikuwa pamoja na Isa!”
57Lakini Petro akakana, akasema, “Ewe mwanamke, hata simjui!”
58Baadaye kidogo, mtu mwingine alimwona Petro akasema, “Wewe pia ni mmoja wao!” Petro akajibu, “Wewe mtu, mimi sio mmoja wao!”
59Baada ya muda wa kama saa moja hivi, mtu mwingine akazidi kusisitiza, “Kwa hakika huyu mtu naye alikuwa pamoja na Isa, kwa maana yeye pia ni Mgalilaya.”
60Petro akajibu, “Wewe mtu, mimi sijui unalosema!” Wakati huo huo, akiwa bado anazungumza, jogoo akawika. 61Naye Bwana Isa akageuka, akamtazama Petro. Ndipo Petro akakumbuka lile neno ambalo Bwana alimwambia: “Kabla jogoo hajawika leo, utanikana mara tatu.” 62Naye akaenda nje, akalia kwa majonzi.
Walinzi wamdhihaki Isa na kumpiga
(Mathayo 26:67-68; Marko 14:65)
63Watu waliokuwa wanamlinda Isa wakaanza kumdhihaki na kumpiga. 64Wakamfunga kitambaa machoni na kumuuliza, “Tabiri! Tuambie ni nani aliyekupiga?” 65Wakaendelea kumtukana kwa matusi mengi.
Isa mbele ya Baraza la Wayahudi
(Mathayo 26:59-66; Marko 14:55-64; Yohana 18:28-38)
66Kulipopambazuka, Baraza la Wazee, yaani viongozi wa makuhani na walimu wa Torati, wakakutana pamoja, naye Isa akaletwa mbele yao. 67Wakamwambia, “Kama wewe ndiwe Al-Masihi#22:67 Al-Masihi maana yake Aliyetiwa mafuta., tuambie.”
Isa akawajibu, “Hata nikiwaambia, hamtaamini. 68Nami nikiwauliza swali, hamtanijibu. 69Lakini kuanzia sasa, Mwana wa Adamu ataketi mkono wa kuume wa Mungu Mwenye Nguvu.”
70Wote wakauliza, “Wewe basi ndiwe Mwana wa Mungu#22:70 Yaani Mwana wa asili moja na Mwenyezi Mungu (Yohana 1:1-2), wa kiroho, bali si wa kimwili.?”
Yeye akawajibu, “Ninyi mwasema kwamba mimi ndiye.”
71Kisha wakasema, “Tuna haja gani tena ya ushahidi zaidi? Tumesikia wenyewe kutoka kinywani mwake.”

Currently Selected:

Luka 22: ONMM

Highlight

Share

Copy

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in