1 Yohane UTANGULIZI
UTANGULIZI
Mapokeo (k.m. Ireneo, mwaka 140-203) yanasema kwamba barua tatu zijulikanazo kama barua za Yohane ziliandikwa na mwandishi yuleyule wa Injili ya nne, yaani mtume Yohane, ingawaje mtume Yohane hatajwi kwa jina katika barua hizo. Ama kweli, katika barua hii ya kwanza msomaji mwangalifu ataweza kuona na kukutana na msamiati, mafungu ya maneno na hata dhamira ambazo zinaafikiana sana na mambo yaliyomo katika Injili ya nne, yaani Injili aliyoandika Yohane. Yatosha tu, k.m., kutaja lengo la kijitabu hiki na la Injili ya Yohane. Katika 1Yoh 5:13 mwandishi anataja shabaha ya kuandika barua hii, “… mpate kujua kwamba mnao uhai wa milele ninyi mnaoamini kwa jina la Mwana wa Mungu.” Katika Yoh 20:31 tunasoma, “… zimeandikwa ili mpate kuamini kuwa Yesu ni Masiha, Mwana wa Mungu, na kwa kuamini mpate kuwa na uhai kwa jina lake.” Dhamira ni ileile na msamiati karibu ni uleule. Linganisha pia utangulizi wa barua hii na ule wa Injili ya nne.
Kuhusu mazingira ya wakati barua hii ilipoandikwa, yaonekana kwamba waumini wa jumuiya hiyo ya mwandishi walikabiliwa na matatizo na mafundisho ambayo yalitishia kutikisa imani yao au hata kuifanya ififie. Baadhi ya fikra na mafundisho ya wakati huu ni ile fikra kwamba maumbile ni mabaya; chochote cha mwili hakiwezi kuwa chema. Kwa hiyo Yesu Kristo, Mwana wa Mungu, hangeweza kuwa na mwili, alionekana tu kuwa nao. Ndiyo maana mwandishi anasisitiza kwa bidii sana kwamba Yesu Kristo aliye Neno la Mungu, alikuwa na mwili kweli (1:1-3). Tena wakati huohuo kulikuwa na watu waliojitenga na jumuiya ya waumini, wakafuata mafundisho yaliyopingana na imani ya awali (2:19).
Muundo wa barua hii
Tofauti na barua nyingine za A.J., hii haina muundo ule wa barua tunaoujua. Haitaji mwandishi na wala haisemi waandikiwa ni akina nani. Badala ya hayo, maandishi haya yanaanza na utangulizi na kumalizia na maneno ya muundo tofauti kabisa na miisho ya barua za A.J. Maandishi haya yanafanana na hotuba au mahubiri ambapo mafundisho yanatolewa pamoja na kuwahimiza waumini wawe na hadhari. Hata hivyo, kwamba hapa tunahusika na barua, inawezekana aghalabu kwa vile mara kwa mara mwandishi anarudiarudia kwamba yaliyomo yametolewa kwa kuandika (1:4; 2:7-26; 5:13).
Kwa jumla, barua yenyewe yaonekana kuwa na sehemu mbili ambazo zimetanguliwa na utangulizi (1:1-4) kama vile katika Injili ya nne (Yoh 1:1-18). Sehemu ya kwanza 1:5–3:10 ina dhamira muhimu ya Mungu ni mwanga. Nayo sehemu ya pili dhamira yake muhimu ni “Tunapaswa kupendana kama vile Mungu alivyotupenda katika Yesu Kristo”. Barua yenyewe inamalizia kwa tamko kuhusu lengo lake.
Currently Selected:
1 Yohane UTANGULIZI: BHN
Highlight
Share
Copy
Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.