2 Timotheo UTANGULIZI
UTANGULIZI
Barua hii ni mojawapo ya barua zijulikanazo kama “Barua za kichungaji” (taz utangulizi wa 1 Tim). Barua hii inamhusu Timotheo binafsi katika mambo mengi, naye Paulo anasema kwa undani kabisa juu ya shida na matatizo ambayo anayapata yeye mwenyewe akiwa kifungoni. Wakati Paulo alipomwandikia barua hii, Timotheo alikuwa kiongozi wa kanisa na mambo mengi ambayo Paulo anaeleza: Maagizo ya jumla na mashauri, yanaafiki viongozi wote wa kanisa na jumuiya ya waumini wake pia. Kwa hiyo walengwa wa mbali wa Barua hii ni wale ambao, kama Timotheo wana wadhifa katika jumuiya ya waumini.
Katika Barua hii kuna habari kadha wa kadha ambazo zinaonesha mahali Paulo alipo wakati huo. Huo ni wakati wa shida na mateso kwake. Paulo anasema katika 2Tim 4:7 “Nimefanya bidii katika mashindano, nimemaliza safarina imani nimeitunza”. Hizi ni nyakati zake za mwisho. Tena wazi zaidi katika aya ya 6: “Niko karibu kabisa kutolewa tambiko na wakati wa kufariki kwangu umefika”. Tena hali ya upweke imemsonga (2Tim 4:9). Kutokana na hayo na mengine mengi katika Barua hii, inaonekana kwamba wakati huo ni kati ya mwaka 61-63 B.K. katika kifungo chake cha pili.
Barua yenyewe inaanza na shukrani za Paulo kwa Mungu kwa vile Timotheo anayo imani na upendo mkubwa. Kisha, pamoja na maneno ya kutia moyo, Paulo anamhimiza Timotheo ashike kwa makini mafundisho aliyopewa, alinde alichokabidhiwa kwa nguvu ya Roho Mtakatifu, na awe tayari kushiriki mateso “kama askari mwaminifu wa Kristo Yesu” (1:3–2:13).
Paulo anawatahadharisha watu kwa njia ya Timotheo waachane na ubishi juu ya maneno ambayo hayafai, bali yanasababisha fujo na kuwatenga watu mbali na imani yao. Paulo anamtaka Timotheo amwige yeye mwenyewe na kuzingatia mafundisho yalivyo, kulingana na Maandiko Matakatifu ambayo ameyapokea tangu alipokuwa kijana. (2:14–4:5).
Karibu na mwisho wa maisha yake (4:5-8), Paulo anamshauri mwanafunzi wake Timotheo namna nzuri zaidi ya kutekeleza majukumu yake ya kichungaji. Sehemu iliyobaki yahusu maagizo mbalimbali na salamu (4:9-22).
Currently Selected:
2 Timotheo UTANGULIZI: BHN
Highlight
Share
Copy
Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.