Kumbukumbu la Sheria 32
32
1“Tegeni masikio enyi mbingu:
Sikiliza, ee dunia, maneno ninayosema.
2Mafundisho yangu na yatone kama mvua,
maneno yangu yadondoke kama umande,
kama manyunyu kwenye mimea michanga,
kama mvua nyepesi katika majani mabichi.
3Maana nitalitangaza jina la Mwenyezi-Mungu,
nanyi mseme, ‘Mungu wetu ni Mkuu’.
4“Mwenyezi-Mungu ni Mwamba wa usalama;
kazi zake ni kamilifu,
njia zake zote ni za haki.
Yeye ni Mungu mwaminifu asiye na kosa,
yeye hufanya mambo ya uadilifu na ya haki.
5Lakini nyinyi mmekosa uaminifu kwake,
nyinyi sio watoto wake tena kwa sababu ya uovu,
nyinyi ni kizazi kiovu na kipotovu.
6Mnawezaje kumlipa hivyo Mwenyezi-Mungu,
enyi watu wapumbavu na msio na akili?
Je, yeye siye Baba yenu aliyewaumba,
aliyewafanya na kuwaimarisha?
7Kumbukeni siku zilizopita,
fikirieni miaka ya vizazi vingi;
waulizeni baba zenu nao watawajulisha,
waulizeni wakubwa wenu nao watawaeleza.
8Mungu Mkuu alipoyagawia mataifa mali yao,
alipowagawa wanadamu,
kila taifa alilipatia mipaka yake,
9kulingana na idadi ya watoto wa Mungu,#32:9 watoto wa Mungu: Tafsiri kadiri ya hati ya Kumrani. Kiebrania: Watoto wa Israeli.
lakini alijiwekea watu wa Yakobo kuwa wake,
hao alijichagulia kuwa mali yake.
10Aliwakuta katika nchi ya jangwa,
nyika tupu zenye upepo mkali.
Aliwalinda na kuwatunza,
aliwafanya kama mboni ya jicho lake.
11Kama tai alindaye kiota chake,
na kurukaruka juu ya makinda yake,
akitandaza mabawa yake ili kuwashikilia,
na kuwabeba juu ya mabawa yake.
12Yeye Mwenyezi-Mungu mwenyewe aliwaongoza
na hapakuwa na mungu mwingine wa kumsaidia.
13Aliwapitisha katika nyanda za juu za nchi,
nao wakala mazao ya mashambani.
Akawapa asali miambani waonje
na mafuta kutoka mwamba mgumu.
14Aliwapa siagi na maziwa ya mifugo,
mafuta ya wanakondoo na kondoo madume,
makundi ya mifugo ya Bashani na mbuzi.
Aliwapa ngano nzuri kabisa na divai mpya wakanywa.
15Watu wa Israeli walinona na kupiga mateke;
walinenepa, wakawa na kitambi na kunawiri;
kisha wakamwacha Mungu aliyewaumba,
wakamdharau Mwamba wa wokovu wao.
16Walimfanya aone wivu mkali kwa miungu yao,
walimchochea akasirike kwa matendo yao ya kuchukiza.
17Walitambikia majini ambayo hayakuwa miungu,
waliiendea miungu ambayo hawakuijua kamwe,
miungu mipya iliyotokea siku za karibuni,
ambayo wazee wao hawakuiheshimu kamwe.
18Hamkumjali Mwamba aliyewapa uhai,
mlimsahau Mungu aliyewazaa nyinyi.
19Mwenyezi-Mungu aliona jambo hilo akawaacha;
aliwakataa watoto wake, waume kwa wake.
20Akasema, ‘Nitawaficha uso wangu
nione mwisho wao utakuwaje!
Maana wao ni kizazi kipotovu,
watoto wasio na uaminifu wowote.
21Wamenichochea kuona wivu kwa kitu kisicho mungu,
wamenikasirisha kwa sanamu zao.
Hivyo nitawafanya waone wivu kwa kisicho watu,
nitawakasirisha kwa kutumia taifa la wapumbavu.
22Hasira yangu imewaka moto,
inachoma mpaka chini kuzimu,
itateketeza dunia na vilivyomo,
itaunguza misingi ya milima.
23Nitarundika maafa chungu nzima juu yao,
nitawamalizia mishale yangu.
24Watakonda kwa njaa,
wataangamizwa kwa homa kali.
Nitapeleka wanyama wenye meno makali kuwashambulia,
na nyoka wenye sumu wanaotambaa mavumbini.
25Vita vitasababisha vifo vingi nje
na majumbani hofu itawatawala,
vijana wa kiume na wa kike watauawa
hata wanyonyao na wazee wenye mvi.
26Nilisema, ningaliwaangamiza kabisa
na kuwafanya wasikumbukwe tena na mtu yeyote,
27ila tu kwa sababu ya majivuno ya maadui zao
ili maadui zao wasije wakafikiria vingine;
wasije wakasema, wamefaulu kuwaangamiza,
nami Mwenyezi-Mungu sihusiki katika mambo haya!’
28“Israeli ni taifa lisilo na akili,
watu wake hawana busara ndani yao.
29Wangekuwa na hekima wangejua kwa nini walishindwa,
wangeweza kuelewa mwisho wao utakuwaje.
30Mtu mmoja anawezaje kuwashinda watu 1,000,
au watu wawili wanawezaje kuwashinda watu 10,000,
isipokuwa kama Mwamba wao amewatupa,
Mwenyezi-Mungu wao amewaacha?
31Hata adui zetu wenyewe wamekiri wazi,
mwamba wao hauna nguvu kama mwamba wetu.
32Maana mizabibu yao ni miche ya Sodoma
zimetoka katika konde za Gomora;
zabibu zake ni zabibu zenye sumu,
vishada vyake ni vichungu.
33Divai yao ni kama sumu ya nyoka,
ina sumu kali ya majoka.
34“Je sina njia ya kuwaadhibu?
Silaha zangu ninazo mkononi.
35Kisasi ni juu yangu,
mimi nitalipiza,
wakati miguu yao itakapoteleza;
maana siku yao ya maafa imewadia,
mwisho wao u karibu sana.
36Mwenyezi-Mungu atawatetea watu wake,
na kuwahurumia watumishi wake,
wakati atakapoona nguvu zao zimeishia,
wala hakuna aliyebaki, mfungwa au mtu huru.
37Ndipo Mwenyezi-Mungu atakapowauliza watu wake,
‘Iko wapi ile miungu yenu,
mwamba mlioukimbilia usalama?’
38Iko wapi hiyo miungu iliyokula matoleo yenu
na kunywa divai na tambiko zenu za kinywaji?
Basi na iinuke, iwasaidieni;
acheni hiyo iwe kinga yenu sasa!
39Oneni kuwa mimi ndimi Mungu
na wala hakuna mwingine ila mimi.
Mimi huua na kuweka hai;
hujeruhi na kuponya,
na hakuna awezaye kumwokoa yeyote mikononi mwangu.
40Nanyosha mkono wangu mbinguni,
na kuapa, kwa uhai wangu wa milele,
41kama mkiuona upanga wangu umeremetao,
na kunyosha mkono kutoa hukumu,
nitawalipiza kisasi maadui zangu,
nitawaadhibu wale wanaonichukia.
42Mishale yangu nitailevya kwa damu,
upanga wangu utashiba nyama,
utalowa damu ya majeruhi na mateka
na adui wenye nywele ndefu.
43“Enyi mataifa washangilieni watu wake,
maana yeye hulipiza kisasi damu ya watumishi wake,
huwalipiza kisasi wapinzani wake,
na kuitakasa nchi ya watu wake.”
44Mose alikuja mbele ya Yoshua, mwana wa Nuni, wakakariri maneno ya wimbo huu, ili Waisraeli wote wausikie.
Wosia wa Mose
45Mose alipomaliza kuwaambia watu wa Israeli maneno haya yote, 46aliwaambia, “Yawekeni mioyoni mwenu maneno yote ambayo ninawapeni leo. Lazima muwaamuru watoto wenu ili wafuate kwa uaminifu maneno yote ya sheria hii. 47Maana sheria hii si maneno matupu bali ni uhai wenu; kwa sheria hii mtaishi maisha marefu katika nchi mnayokwenda kuimiliki, ngambo ya mto Yordani.”
48Siku hiyohiyo, Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, 49“Panda mlima huu wa Abarimu, mlima Nebo katika nchi ya Moabu, mkabala wa mji Yeriko, ukaiangalie nchi ya Kanaani ninayowapa Waisraeli waimiliki. 50Kisha ufariki hukohuko mlimani kama kaka yako Aroni alivyofariki katika mlima Hori, 51kwa sababu nyote wawili mlivunja uaminifu wenu kwangu mbele ya Waisraeli mlipokuwa kwenye maji ya Meriba, karibu na mji wa Kadeshi, katika jangwa la Sini, mkakosa kuuthibitisha utakatifu wangu kati ya Waisraeli. 52Utaiona nchi iliyo mbele yako, lakini hutaingia katika nchi hiyo ninayowapa Waisraeli.”
Currently Selected:
Kumbukumbu la Sheria 32: BHN
Highlight
Share
Copy
Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.