Ezekieli 31
31
Misri inalinganishwa na mwerezi
1Mnamo siku ya kwanza ya mwezi wa tatu, mwaka wa kumi na moja tangu uhamisho wetu, neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia: 2“Wewe mtu! Mwambie hivi Farao mfalme wa Misri na watu wake wote:
Wewe wafanana na nini kwa ukuu wako?
3Wewe ni kama mwerezi wa Lebanoni#31:3 kama … Lebanoni: Au unalingana na Ashuru.
wenye matawi mazuri na majani mengi na shina refu.
Kilele chake kinafika hata mawinguni.
4Maji yaliustawisha,
vilindi vya maji viliulisha.
Mito ilibubujika mahali ulipoota,
ikapeleka vijito kwenye miti yote ya msituni.
5“Kwa hiyo, ulirefuka sana
kupita miti yote msituni;
matawi yake yalizidi kuwa mengi na makubwa,
kutokana na maji mengi mizizini mwake.
6Ndege wote waliweka viota matawini mwake,
chini yake wanyama walizaliwa,
mataifa yote makubwa yaliburudika kivulini mwake.
7Ulikuwa mzuri kwa ukubwa wake,
na kwa urefu wa matawi yake.
Mizizi yake ilipenya chini
mpaka penye maji mengi.
8 # 31:8 Taz Mwa 2:9 Miongoni mwa mierezi ya bustanini mwa Mungu,
hakuna mti uliolingana nao,
wala misonobari haikulingana na matawi yake,
mibambakofi haikuwa na matawi kama yake,
hata mti wowote wa bustani ya Mungu
haukulingana nao kwa uzuri.
9Mimi niliufanya kuwa mzuri
kwa matawi yake mengi;
ulionewa wivu na miti yote ya Edeni
iliyokuwa katika bustani ya Mungu.
10“Kwa hiyo, mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Kwa sababu wewe ulirefusha#31:10 Kwa … ulirefusha: Au Kwa sababu wewe ulirefusha. kimo chake na kukiinua kilele chake kati ya matawi makubwa, ukajivunia urefu wake, 11nitautia mikononi mwa mkuu kati ya mataifa. Yeye, atauadhibu. Nimeutupilia mbali kadiri ya uovu wake. 12Watu wa mataifa mengine katili kupindukia, wataukata na kuubwaga chini na kuuacha. Matawi yake yataanguka chini mlimani na kila mahali mabondeni; yatavunjika na kutapakaa chini katika magenge yote. Watu wote wataondoka kivulini mwake na kuuacha. 13Ndege wote watatua juu ya mabaki yake na wanyama wote wa porini watakanyaga matawi yake. 14Hayo yameupata ili mti wowote ulio mahali penye maji usiweze kurefuka tena kiasi hicho wala kukifikisha kilele chake mawinguni. Mti wowote unaonyweshwa maji usiweze tena kufikia urefu huo. Kwa maana kila kitu mwisho wake ni kifo; hali kadhalika na watu. Wote watashiriki hali yao washukao shimoni kwa wafu.
15“Kwa hiyo mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Siku ileile mwerezi ulipofika kuzimu nilitandaza giza nene juu yake nikaufunika; mito yake niliikausha na mtiririko wa maji yake mengi nikaukomesha. Nayo Lebanoni niliiweka gizani kwa ajili yake, na miti yote msituni ikazirai kwa ajili yake. 16Niliyafanya mataifa yatetemeke kwa sauti ya kuanguka kwake, naam, wakati nilipouangusha chini kuzimu pamoja nao washukao shimoni kwa wafu nayo miti yote ya Edeni, miti mizuri na ya pekee ya Lebanoni ambayo ilimwagiliwa maji ilifarijiwa huko chini kwa wafu. 17Hiyo nayo ilishuka huko kuzimu pamoja nao, ikajiunga na wale waliofungamana nao na ambao waliburudika chini ya kivuli chake.
18“Kwa uzuri na ukuu wa mti huo, hamna mti wowote bustanini Edeni ambao uliweza kulinganishwa nao. Sasa, mti huo ni wewe mfalme Farao. Wewe utatupwa chini kwa wafu pamoja na miti ya Edeni. Utalala karibu na wale wasiomjua Mungu na wale waliouawa kwa upanga. Hiyo itakuwa hali yako ewe Farao, wewe na watu wako. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema.”
Currently Selected:
Ezekieli 31: BHN
Highlight
Share
Copy
Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.