Wagalatia UTANGULIZI
UTANGULIZI
Barua ya Paulo kwa jumuiya ya Wakristo huko Galatia labda iliandikwa Paulo akiwa Antiokia mnamo mwaka 48 B.K., baada ya ziara yake ya kwanza. Paulo alianzisha jumuiya hiyo au kanisa hilo la Galatia katika Antiokia, eneo ambalo lilikuwa mojawapo ya mikoa iliyokuwa chini ya utawala wa Roma. Sehemu hiyo sasa ni nchi ya Uturuki.
Jambo muhimu katika barua hii ni masuala kadha wa kadha yaliyotokana na mkutano wa mitume kule Yerusalemu mwaka 48 B.K. (taz Mate 15). Katika ziara yake ya kwanza, Paulo alikabiliwa na pingamizi zilizosababishwa na watu waliofika kutoka Uyahudi. Hawa walifundisha kwamba watu wasio Wayahudi waliotaka kuwa Wakristo sharti kwanza wawe Wayahudi, aghalabu watahiriwe, ndipo waweze kuwa watu wa Kristo. Hilo lilikuwa tatizo la kimsingi katika lile kanisa changa la awali.
Barua hii kwa Wakristo wa Galatia inaonesha dhahiri, tena kwa maneno mazitomazito, msimamo wake Paulo kuhusu tatizo hilo. Shabaha yake ni kuwaondoa hao Wakristo waliopotoshwa na mafundisho ya wapinzani wake wairudie imani safi ya kweli! Basi, kwanza Paulo anajitetea dhidi ya hao waalimu wa uongo kwa kuonesha kwamba wito wake wa kuwa mtume hakuupata kutoka kwa binadamu, bali kutoka kwa Mungu, na kwamba alitumwa kwenda kuwahubiria hasa wasio Wayahudi. Kisha anaeleza waziwazi hoja yake kwamba watu hufanywa kuwa waadilifu mbele ya Mungu sio kwa kutii sheria, bali kwa kumtegemea au kumwamini Mungu. Kristo aliwaondoa watu katika utumwa wa sheria, na hivyo uhuru aliowapa usitumiwe tena vibaya. Uhuru huo utaleta mafanikio ambayo ni “matunda ya Roho Mtakatifu!”
Currently Selected:
Wagalatia UTANGULIZI: BHN
Highlight
Share
Copy
Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.