Hosea 2
2
1Basi, waiteni kaka zenu, “Watu wangu,” na dada zenu, “Waliohurumiwa.”
Mke mzinzi – taifa potovu la Israeli
2Mlaumuni mama yenu mlaumuni,
maana sasa yeye si mke wangu
wala mimi si mume wake.
Mlaumuni aondokane na uasherati wake,
ajiepushe na uzinzi wake.
3La sivyo, nitamvua nguo abaki uchi,
nitamfanya awe kama alivyozaliwa.
Nitamfanya awe kama jangwa,
nitamweka akauke kama nchi kavu.
Nitamuua kwa kiu.
4Na watoto wake sitawahurumia,
maana ni watoto wa uzinzi.
5Mama yao amefanya uzinzi,
aliyewachukua mimba amefanya mambo ya aibu.
Alisema; “Nitaambatana na wapenzi wangu,
ambao hunipa chakula na maji,
sufu na kitani, mafuta na divai.”
6Basi, nitaiziba njia yake kwa miiba,
nitamzungushia ukuta,
asipate njia ya kutokea nje.
7Atawafuata wapenzi wake,
lakini hatawapata;
naam, atawatafuta,
lakini hatawaona.
Hapo ndipo atakaposema,
“Nitarudi kwa mume wangu wa kwanza;
maana hapo kwanza nilikuwa nafuu kuliko sasa.”
8Hakujua kwamba ni mimi
niliyempa nafaka, divai na mafuta,
niliyemjalia fedha na dhahabu kwa wingi,
ambazo alimpelekea Baali.
9Kwa hiyo wakati wa mavuno nitaichukua nafaka yangu,
nitaiondoa divai yangu wakati wake.
Nitamnyang'anya nguo zangu za sufu na kitani,
ambazo zilitumika kuufunika uchi wake.
10Nitamvua abaki uchi mbele ya wapenzi wake,
wala hakuna mtu atakayeweza kunizuia.
11Nitazikomesha starehe zake zote,
sikukuu zake za mwezi mwandamo na za Sabato,
na sikukuu zote zilizoamriwa.
12Nitaiharibu mizabibu yake na mitini,
anayosema ni malipo kutoka kwa wapenzi wake.
Nitaifanya iwe misitu,
nao wanyama wa porini wataila.
13Nitamlipiza sikukuu za Baali alizoadhimisha,
muda alioutumia kuwafukizia ubani,
akajipamba kwa pete zake na johari,
na kuwaendea wapenzi wake,
akanisahau mimi.
Mimi Mwenyezi-Mungu nasema.
Upendo wa Mwenyezi-Mungu kwa watu wake
14Kwa hiyo, nitamshawishi,
nitampeleka jangwani
na kusema naye kwa upole.
15Huko nitamrudishia mashamba yake ya mizabibu,
bonde la Akori nitalifanya lango la tumaini.
Atanifuata kwa hiari kama alipokuwa kijana,
kama wakati alipotoka katika nchi ya Misri.
16“Mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Siku hiyo, wewe utaniita ‘Mume wangu,’ na sio tena ‘Baali wangu.’ 17Maana, nitalifanya jina la Baali lisitamkike tena kinywani mwako. 18Nitafanya agano na wanyama wa porini, ndege wa angani pamoja na vyote vitambaavyo, wasikuumize. Nitatokomeza upinde, upanga na silaha za vita katika nchi, na kukufanya uishi kwa usalama. 19Nitakufanya mke wangu milele; uwe wangu kwa uaminifu na haki, kwa fadhili na huruma. 20Naam, nitakuposa kwa uaminifu, nawe utanijua mimi Mwenyezi-Mungu.
21“Siku hiyo, mimi Mwenyezi-Mungu nasema,
nitaikubali haja ya mbingu ya kunyesha mvua,
mbingu nazo zitaikubali haja ya ardhi.
22Ardhi itaikubali haja ya nafaka, divai na mafuta,
navyo vitatosheleza mahitaji ya Yezreeli.#2:22 Yezreeli: Kuna mchezo wa maneno hapa. Yezreeli maana yake Mungu hupanda mbegu (aya 23).
23Nitamwotesha Yezreeli katika nchi;
nitamhurumia ‘Asiyehurumiwa’,
na wale walioitwa ‘Siwangu’,
nitawaambia, ‘Nyinyi ni watu wangu.’
Nao watasema, ‘Wewe ni Mungu wetu.’”
Currently Selected:
Hosea 2: BHN
Highlight
Share
Copy
Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.