YouVersion Logo
Search Icon

Isaya 43

43
Mungu aahidi kuwaokoa watu wake
1Mwenyezi-Mungu aliyewaumba enyi watu wa Yakobo,
yeye aliyewafanya enyi watu wa Israeli, asema:
“Msiogope, maana mimi nimewakomboa;
nimewaita kwa jina nanyi ni wangu.
2Mkipita katika mafuriko,
mimi nitakuwa pamoja nanyi;
mkipita katika mito,
haitawashinda nguvu.
Mkitembea katika moto,
hamtaunguzwa;
mwali wa moto hautawaunguza.
3Maana mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu,
Mungu Mtakatifu wa Israeli, Mwokozi wenu.
Nitaitoa nchi ya Misri iwe fidia yenu,
nitaitoa Kushi na Seba ili mwachwe huru.
4Kwa vile mna thamani mbele yangu,
kwa kuwa nimewapa hadhi na kuwapenda,
mimi nawaacha watu kusudi niwapate nyinyi,
nayaachilia mataifa badala ya maisha yenu.
5Msiogope maana mimi nipo pamoja nanyi.
“Nitawarudisha wazawa wenu toka mashariki,
nitawakusanyeni kutoka magharibi.
6Nitaiambia kaskazini, ‘Waache waondoke’,
na kusini, ‘Usiwazuie’!
Warudisheni watu kutoka mbali,
kutoka kila mahali duniani.
7Kila mmoja hujulikana kwa jina langu,
niliwaumba wote na kuwafanya
kwa ajili ya utukufu wangu.”
Israeli ni ushahidi wa Mwenyezi-Mungu
8Waleteni mbele watu hao,
ambao wana macho lakini hawaoni
wana masikio lakini hawasikii!
9Mataifa yote na yakusanyike,
watu wote na wakutane pamoja.
Nani kati ya miungu yao awezaye kutangaza yatakayotukia?
Nani awezaye kutuonesha yanayotukia sasa?
Wawalete mashahidi wao
kuthibitisha kwamba walifanya hivyo.
Waache wasikilize na kusema, “Ilikuwa kweli.”
10Mwenyezi-Mungu asema hivi:
“Nyinyi Waisraeli ni mashahidi wangu;
niliwachagua muwe watumishi wangu,
mpate kunijua na kuniamini,
kwamba ndimi peke yangu Mungu.
Kabla yangu hajapata kuwapo mungu mwingine,
wala hatakuwapo mungu mwingine.
11“Mimi peke yangu ndimi Mwenyezi-Mungu,
hakuna mkombozi mwingine ila mimi.
12Nilitangaza yale ambayo yangetukia,
kisha nikaja na kuwakomboa.
Hakuna mungu mwingine aliyewahi kufanya hivyo,
nanyi ni mashahidi wangu.
13Mimi ni Mungu na nitakuwa Mungu daima.
Hakuna awezaye kuiepa nguvu yangu;
hakuna awezaye kupinga ninayofanya.”
Kukombolewa kutoka Babuloni
14Mwenyezi-Mungu, Mkombozi wenu,
Mtakatifu wa Israeli, asema hivi:
“Kwa ajili yenu nitatuma jeshi Babuloni.
Nitayavunjilia mbali malango ya mji wake,
na kelele za hao Wakaldayo zitageuka maombolezo.
15Mimi ni Mwenyezi-Mungu, Mtakatifu wenu;
Mimi ndimi Muumba wa Israeli, Mfalme wenu.”
16Mwenyezi-Mungu asema hivi:
“Wakati mmoja nilifanya barabara baharini
nikaweka njia kati ya mawimbi makubwa.
17Nililipiga jeshi lenye nguvu,
jeshi la magari na farasi wa vita,
askari na mashujaa wa vita.
Niliwaangusha chini wasiweze kuinuka tena,
niliwakomesha na kuwazima kama utambi wa taa.
Sasa nasema:
18‘Msiyanganganie mambo yaliyopita,
wala msifikirie vitu vya zamani.
19Tazameni, mimi ninafanya kitu kipya.
Kinafanyika sasa hivi,
nanyi mtaweza kukiona.
Nitafanya njia nyikani,
na kububujisha mito jangwani.
20Wanyama wa porini wataniheshimu,
kina mbweha na kina mbuni,
maana nitaweka maji nyikani,
na kububujisha mito jangwani,
ili kuwanywesha watu wangu wateule,
21watu niliowaumba kwa ajili yangu mwenyewe,
ili wazitangaze sifa zangu!’
Dhambi ya Israeli
22“Lakini ewe taifa la Yakobo, hukuniabudu mimi;
enyi watu wa Israeli, mlinichoka mimi!
23Hamjaniletea kondoo wenu wa sadaka za kuteketezwa,
wala kuniheshimu kwa tambiko zenu.
Nami sikuwalemeza kwa kutaka sadaka,
wala sikuwachosha kwa kuwadai ubani.
24Hamkuninunulia manukato kwa faida yenu,
wala kuniridhisha kwa nyama nono za tambiko.
Badala yake dhambi zenu zimekuwa mzigo kwangu,
mmenichosha kabisa kwa makosa yenu.
25Walakini mimi ndimi niliyefuta makosa yenu kwa heshima yangu,
ndimi niyafutaye makosa kwa ajili yangu mwenyewe,
na wala sitazikumbuka dhambi zenu.
26“Niambie kama mna kisa nami,
njoo tukahojiane;
toeni mashtaka yenu ili tuuone ukweli wenu!
27Babu yenu wa kwanza alitenda dhambi,
wapatanishi wenu waliniasi.
28Kwa hiyo niliwafanya haramu wakuu wa mahali patakatifu
nikawaacha watu wa Yakobo waangamizwe,
naam, nikawaacha Waisraeli watukanwe.”

Currently Selected:

Isaya 43: BHN

Highlight

Share

Copy

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in