Yobu 29
29
1Kisha Yobu akaendelea na hoja yake, akasema:
2“Laiti ningekuwa kama zamani,
wakati ule ambapo Mungu alinichunga;
3wakati taa yake iliponiangazia kichwani,
na kwa mwanga wake nikatembea gizani.
4Wakati huo nilifikia ukamilifu wa maisha,
wakati urafiki wa Mungu ulikaa nyumbani kwangu.
5Mungu Mwenye Nguvu alikuwa bado pamoja nami,
na watoto wangu walinizunguka.
6Nyakati hizo niliogelea kwenye ufanisi,
miamba ilinitiririshia vijito vya mafuta!
7Nilipokutana na wazee langoni mwa mji
na kuchukua nafasi yangu mkutanoni,
8vijana waliponiona walisimama kando,
na wazee walisimama wima kwa heshima.
9Wakuu waliponiona waliacha kuzungumza
waliweka mikono juu ya midomo kuwataka watu wakae kimya.
10Sauti za waheshimiwa zilinyamazishwa,
na vinywa vyao vikafumbwa.
11Kila aliyesikia habari zangu alinitakia heri
na aliponiona, alikubali habari hizo kuwa kweli:
12Nilimwokoa maskini aliyenililia msaada,
kadhalika na yatima asiyekuwa na wa kumsaidia.
13Waliokuwa karibu kuangamia walinitakia baraka,
niliwafanya wajane waone tena furaha moyoni.
14Uadilifu ulikuwa vazi langu;
kutenda haki kulikuwa kama joho na kilemba changu.
15Kwa vipofu nilikuwa macho ya kuwaonesha njia,
kwa viwete nilikuwa miguu yao.
16Kwa maskini nilikuwa baba yao,
nilifanya bidii kutetea haki za watu nisiowajua.
17Nilizivunja nguvu za watu waovu,
nikawafanya wawaachilie mateka wao.
18Kisha nikafikiri: Nitafia kiotani mwangu nimetulia;
siku za maisha yangu zitaongezeka kama mchanga.
19Mimi ni kama mti uliotandaza mizizi majini,
umande wa usiku huburudisha matawi yangu.
20Napata fahari mpya daima,
na nguvu zangu tayari kama mshale na upinde.
21“Wakati huo watu walinisikiliza na kungoja,
walikaa kimya kungojea shauri langu.
22Nilipomaliza kusema hawakuwa na cha kuongeza,
maneno yangu yaliwakolea kama matone ya mvua.
23Watu waliningojea kama wangojeavyo mvua,
walikuwa kama watu wanaotazamia msimu wa vuli.
24Walipokata tamaa niliwaonesha uso wa furaha,
uchangamfu wa uso wangu wakaungangania.
25Niliwatangulia kuwaongoza, nikawaonesha njia;
nilikuwa kwao kama mfalme kati ya majeshi yake;
kama mtu anayewafariji wenye msiba.
Currently Selected:
Yobu 29: BHN
Highlight
Share
Copy
Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.