Yobu 3
3
MAJADILIANO YA YOBU NA RAFIKI ZAKE
Yobu analalamika
1 # Taz Yer 20:14-18 Hatimaye Yobu aliamua kuongea, akailaani siku aliyozaliwa. 2Yobu akasema:
3 # Taz Sir 23:14 “Ilaaniwe siku ile niliyozaliwa;
usiku ule iliposemwa, ‘Mwana amechukuliwa mimba’
4Siku hiyo na iwe giza!
Mungu juu asijishughulishe nayo!
Wala nuru yoyote isiiangaze!
5Mauzauza na giza nene yaikumbe,
mawingu mazito yaifunike.
Giza la mchana liitishe!
6Usiku huo giza nene liukumbe!
Usihesabiwe katika siku za mwaka,
wala usitiwe katika idadi ya siku za mwezi.
7Naam, usiku huo uwe tasa,
sauti ya furaha isiingie humo.
8Walozi wa siku waulaani,
watu stadi wa kuligutua dude Lewiyathani waulaani!
9Nyota zake za pambazuko zififie,
utamani kupata mwanga, lakini usipate,
wala usione nuru ya pambazuko.
10Maana usiku huo haukulifunga tumbo la mama,
wala kuficha taabu nisizione.
11Mbona sikufa nilipozaliwa,
nikatoka tumboni na kutoweka?
12Kwa nini mama yangu alinizaa?
Kwa nini nikapata kunyonya?
13Maana ningekuwa nimezikwa, kimya;
ningekuwa nimelazwa na kupumzika,
14pamoja na wafalme na watawala wa dunia,
waliojijengea upya magofu yao;
15ningekuwa pamoja na wakuu waliokuwa na dhahabu,
waliojaza nyumba zao fedha tele.
16Au, mbona sikuwa kama mimba iliyoharibika,
naam, kama mtoto aliyezaliwa mfu?
17Huko kwa wafu waovu hawamsumbui mtu,
huko wachovu hupumzika.
18Huko wafungwa hustarehe pamoja,
hawaisikii kamwe sauti ya mnyapara.
19Wakubwa na wadogo wako huko,
nao watumwa wamepata uhuru mbali na bwana zao.
20Ya nini kumjalia nuru yule aliye taabuni;
na uhai yule aliye na huzuni moyoni?
21Mtu atamaniye kifo lakini hafi;
hutafuta kifo kuliko hazina iliyofichika.
22Mtu kama huyo atashangilia mno na kufurahi,
atafurahi atakapokufa na kuzikwa!
23Ya nini kumjalia uhai mtu ambaye njia zake zimefungwa,
mtu ambaye Mungu amemwekea kizuizi?
24Kwa maana kusononeka ndio mkate wangu,
kupiga kite kwangu kunatiririka mithili ya maji.
25Kile ninachokiogopa kimenipata,
ninachokihofia ndicho kilichonikumba.
26Sina amani wala utulivu;
sipumziki, taabu imenijia.”
Currently Selected:
Yobu 3: BHN
Highlight
Share
Copy
Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.