Yobu 40
40
1Mwenyezi-Mungu akaendelea kumwambia Yobu:
2“Je, wewe mwenye kuchunguza makosa utashindana na Mungu Mwenye Nguvu?
Wewe unayebishana nami Mungu, basi jibu mambo hayo!”
3Kisha Yobu akamjibu Mwenyezi-Mungu:
4“Mimi sifai kitu nitakujibu nini?
Naufunga mdomo wangu.
5Nilithubutu kusema na sitasema tena.
Nilisisitiza lakini sitaendelea kusema zaidi.”
6Hapo Mwenyezi-Mungu akamjibu kutoka kimbunga:
7“Jikaze kama mwanamume.
Nitakuuliza, nawe utanijibu.
8Je, unataka kweli kubatilisha hukumu yangu,
kuniona nina hatia ili wewe usiwe na hatia?
9Je, una nguvu kama mimi Mungu?
Waweza kunguruma kwa sauti kama yangu?
10“Basi, jioneshe kuwa na fahari na ukuu,
ujipambe kwa utukufu na fahari.
11Wamwagie watu hasira yako kuu;
mwangalie kila mwenye kiburi na kumwangusha.
12Mwangalie kila mwenye kiburi na kumporomosha,
uwakanyage waovu mahali walipo.
13Wazike wote pamoja ardhini;
mfunge kila mmoja kwa kifungo cha kifo.
14Hapo nitakutambua,
kwamba nguvu yako mwenyewe imekupa ushindi.
15“Liangalie lile dude Behemothi,#40:15 Behemothi: Mnyama huyo huenda ni kiboko.
nililoliumba kama nilivyokuumba wewe.
Hilo hula nyasi kama ng'ombe,
16lakini mwilini lina nguvu ajabu,
na misuli ya tumbo lake ni imara.
17Huufanya mkia wake mgumu kama mwerezi,
mishipa ya mapaja yake imeshonwa pamoja.
18Mifupa yake ni mabomba ya shaba,
viungo vyake ni kama pao za chuma.
19“Hilo ni la kwanza la ajabu kati ya viumbe vyangu!#40:19 Hilo … vyangu: Au hilo ndilo tunda la kwanza la kazi ya Mungu.
Ni mimi Muumba wake niwezaye kulishinda.
20Milima wanamocheza wanyama wote wa porini
hutoa chakula chake.
21Hujilaza chini ya vichaka vya miiba,
na kujificha kati ya matete mabwawani.
22Hujisitiri katika vivuli vya vichaka vya miiba
na vya miti iotayo kando ya vijito.
23Mto ukifurika haliogopi,
halitishiki hata mto Yordani ukilifurikia kinywani.
24Nani awezaye kuliziba macho na kuliteka?
Nani awezaye kulitoboa pua kwa mtego?
25 # Taz Zab 74:14; 104:26; Isa 27:1 # 40:25 Kufuatana na Biblia ya Kiebrania; baadhi ya tafsiri ni 41:1 Je, waweza kuvua dude Lewiyathani#40:25 Lewiyathani: Au Mamba. kwa ndoana,
au kuufunga ulimi wake kwa kamba?
26Je, unaweza kulitia kamba puani mwake,
au kulitoboa taya kwa kulabu?
27Je, wadhani litakusihi uliachilie?
Je, litazungumza nawe kwa upole?
28Je, litafanya mapatano nawe,
ulichukue kuwa mtumishi wako milele?
29Je, utacheza nalo kama ndege,
au kulifunga kamba licheze na wajakazi wako?
30Wadhani wavuvi watashindania bei yake?
Je, wafanyabiashara watathubutu kulikata na kugawana?
31Je, waweza kuichoma ngozi yake kwa mikuki,
au kichwa chake kwa mfumo wa kuvua samaki?
32Jaribu tu kuligusa, uone cha mtema kuni;
Kamwe hutarudia tena kufanya hivyo!
Currently Selected:
Yobu 40: BHN
Highlight
Share
Copy
Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.