Yoeli 1
1
1Neno la Mwenyezi-Mungu lililomjia Yoeli, mwana wa Pethueli:
Watu waombolezea mimea
2Sikilizeni kitu hiki enyi wazee;
tegeni sikio wakazi wote wa Yuda!
Je, jambo kama hili limewahi kutokea maishani mwenu,
au nyakati za wazee wenu?
3Wasimulieni watoto wenu jambo hili,
nao wawasimulie watoto wao,
na watoto wao wakisimulie kizazi kifuatacho.
4Nzige, makundi kwa makundi, wameivamia mimea;
kilichoachwa na nzige kimeliwa na tunutu,
kilichoachwa na tunutu kimeliwa na parare,
kilichoachwa na parare kimeliwa na matumatu.
5Enyi walevi, levukeni na kulia;
pigeni yowe, enyi walevi wa divai;
zabibu zote za kutengeneza divai mpya zimeharibiwa.
6 # Taz Ufu 9:8 Jeshi la nzige limeivamia nchi yetu;
lina nguvu na ni kubwa ajabu;
meno yake ni kama ya simba,
na magego yake ni kama ya simba jike.
7Limeiharibu mizabibu yetu,
na kuitafuna mitini yetu.
Limeyabambua magamba yake na kuyatupa chini,
na matawi yake yameachwa meupe.
8Lieni kama msichana aliyevaa vazi la gunia
akiombolezea kifo cha mchumba wake.
9Sadaka za nafaka na kinywaji zimetoweka nyumbani kwa Mwenyezi-Mungu.
Makuhani, wahudumu wa Mwenyezi-Mungu, wanaomboleza.
10Mashamba yamebaki matupu;
nchi inaomboleza,
maana nafaka imeharibiwa,
divai imetoweka,
mafuta yamekosekana.
11Ombolezeni enyi wakulima;
pigeni yowe enyi watunza mizabibu.
Ngano na shayiri zimeharibika,
mavuno yote shambani yameangamia.
12Mizabibu imenyauka;
mitini imedhoofika;
mikomamanga, mitende na mitofaa imekauka,
naam miti yote shambani imekauka.
Furaha imetoweka miongoni mwa watu.
13Enyi makuhani, jivikeni magunia kuomboleza,
lieni enyi wahudumu wa madhabahu.
Ingieni hekaluni mkaomboleze usiku kucha!
Sadaka za nafaka na kinywaji zimetoweka nyumbani kwa Mungu.
14Toeni amri watu wafunge;
itisheni mkutano wa kidini.
Kusanyeni wazee na wakazi wote wa nchi,
nyumbani kwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu,
na humo mkamlilie Mwenyezi-Mungu.
15Ole wetu kwa ile siku ya Mwenyezi-Mungu,
siku hiyo ya Mwenyezi-Mungu inakaribia;
inakuja pamoja na maangamizi,
kutoka kwa Mungu Mkuu.
16Mazao yetu yameharibiwa huku tunatazama.
Furaha na kicheko vimetoweka nyumbani kwa Mungu wetu.
17Mbegu zinaoza udongoni;
ghala za nafaka ni ukiwa mtupu,
ghala zimeharibika,
kwa kukosa nafaka ya kuhifadhi.
18Tazama wanyama wanavyolia kwa huzuni!
Makundi ya ng'ombe yanahangaika,
kwa sababu yamekosa malisho;
hata makundi ya kondoo yanateseka.
19Ninakulilia wewe, ee Mwenyezi-Mungu,
moto umemaliza malisho nyikani,
miali ya moto imeteketeza miti mashambani.
20Hata wanyama wa porini wanakulilia wewe,
maana, vijito vya maji vimekauka,
moto umemaliza malisho nyikani.
Currently Selected:
Yoeli 1: BHN
Highlight
Share
Copy
Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.