Maombolezo 1
1
1Ajabu mji uliokuwa umejaa watu,
sasa wenyewe umebaki tupu!
Ulikuwa maarufu kati ya mataifa;
sasa umekuwa kama mama mjane.
Miongoni mwa miji ulikuwa kama binti mfalme;
sasa umekuwa mtumwa wa wengine.
2Walia usiku kucha;
machozi yautiririka.
Hakuna hata mmoja wa wapenzi wake wa kuufariji.
Rafiki zake wote wameuhadaa;
wote wamekuwa adui zake.
3Watu wa Yuda wamekwenda uhamishoni
pamoja na mateso na utumwa mkali.
Sasa wanakaa miongoni mwa watu wa mataifa,
wala hawapati mahali pa kupumzika.
Waliowafuatia wamewakamata wakiwa taabuni.
4Barabara za kwenda Siyoni zinasikitisha;
hakuna wapitao kwenda kwenye sikukuu.
Malango ya mji wa Siyoni ni tupu;
makuhani wake wanapiga kite,
wasichana wake wana huzuni,
na mji wenyewe uko taabuni.
5Adui zake ndio wanaoutawala na wanafanikiwa,
kwani Mwenyezi-Mungu ameutesa
kwa sababu ya makosa mengi.
Watoto wake wametekwa na kupelekwa mbali.
6Fahari yote ya watu wa Siyoni imewatoweka;
wakuu wake wamekuwa kama kulungu wasio na malisho.
Bila nguvu waliwakimbia watesi wao.
7Ukiwa sasa magofu matupu,
Yerusalemu wakumbuka fahari yake.
Ulipoangukia mikononi mwa maadui zake,
hakuna aliyekuwako kuusaidia.
Washindi wake walichekelea kuanguka kwake.
8Yerusalemu ulitenda dhambi mbaya,
ukawa mchafu kwa dhambi zake.
Wote waliousifia wanaudharau,
maana wameuona uchi wake.
Wenyewe wapiga kite na kujificha kwa aibu.
9Uchafu wake ulionekana waziwazi,
lakini wenyewe haukujali mwisho wake.
Anguko lake lilikuwa kubwa mno;
hakuna awezaye kuufariji.
Wasema:
“Tazama ee Mwenyezi-Mungu mateso yangu,
maana adui yangu ameshinda.”
10Maadui wamenyosha mikono yao,
wanyakue vitu vyake vyote vya thamani.
Naam umeona watu wa mataifa wakiingia hekaluni,
watu ambao Mwenyezi-Mungu aliwakataza
kujumuika na jumuiya ya watu wake.
11Watu wa Yerusalemu wote wanahangaika kutafuta chakula;
hazina zao wanazitoa kupata chakula,
wajirudishie nguvu zao.
Nao mji unalia,
“Hebu niangalie, ee Mwenyezi-Mungu,
ona jinsi nilivyogeuka kuwa duni.
12“Enyi wapita njia, hivi hamjali kitu?
Tazameni! Hakuna aliyepatwa na uchungu kama mimi,
uchungu alioniletea Mwenyezi-Mungu,
siku ya hasira yake kali.
13“Aliteremsha moto kutoka juu,
ukanichoma hata mifupani mwangu.
Alinitegea wavu akaninasa,
kisha akanirudisha nyuma,
akaniacha nimeduwaa na kuzirai mchana kutwa.
14“Aliyahesabu makosa yangu yote
akayakusanya mahali pamoja;
aliyafunga shingoni mwangu kama nira,
nikafyonzwa nguvu zangu kwa uzito wake.
Mwenyezi-Mungu aliniweka mikononi mwao
watu ambao siwezi kuwapinga.
15“Mwenyezi-Mungu aliwakataa askari walionilinda,
alitangaza wakati maalumu wa kuniadhibu
kuwaponda vijana wangu wa kiume.
Aliwaponda kama katika shinikizo
watu wangu wa Yuda.
16“Kwa sababu ya hayo ninalia,
machozi yanitiririka,
sina mtu yeyote wa kunifariji;
hakuna yeyote wa kunitia moyo.
Watoto wangu wameachwa wakiwa,
maana adui yangu amenishinda.
17“Nainyosha mikono yangu
lakini hakuna wa kunifariji.
Mwenyezi-Mungu ametoa amri dhidi yangu mimi Yakobo,
jirani zangu wawe maadui zangu.
Naam, mimi Yerusalemu nimekuwa kinyaa kwao.
18“Lakini Mwenyezi-Mungu amefanya sawa
kwa maana nimeliasi neno lake.
Nisikilizeni enyi watu wote,
yatazameni mateso yangu.
Wasichana wangu na wavulana wangu,
wamechukuliwa mateka.
19“Niliwaita wapenzi wangu,
lakini wao wakanihadaa.
Makuhani na wazee wangu
wamefia mjini
wakijitafutia chakula,
ili wajirudishie nguvu zao.
20“Ona, ee Mwenyezi-Mungu nilivyo taabuni.
Roho yangu imechafuka,
moyo wangu unasononeka
kwani nimekuasi vibaya.
Huko nje kumejaa mauaji,
ndani nako ni kama kifo tu.
21“Sikiliza ninavyopiga kite;
hakuna wa kunifariji.
Maadui zangu wote wamesikia juu ya taabu yangu:
Wanafurahi kwamba umeniletea maafa.
Uifanye ile siku uliyoahidi ifike,
uwafanye nao wateseke kama mimi.
22“Uwapatilize kwa ajili ya uovu wao wote.
Uwatende kama ulivyonitenda mimi
kwa sababu ya makosa yangu yote.
Nasononeka sana kwa maumivu
na moyo wangu unazimia.”
Currently Selected:
Maombolezo 1: BHN
Highlight
Share
Copy
Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.