Mathayo 21
21
Yesu anaingia Yerusalemu kwa shangwe
(Marko 11:1-11; Luka 19:28-40; Yoh 12:12-19)
1Yesu na wanafunzi wake walipokaribia Yerusalemu na kufika Bethfage katika mlima wa Mizeituni, aliwatuma wanafunzi wake wawili, 2akawaambia, “Nendeni hadi kijiji kilicho mbele yenu na mtamkuta punda amefungwa na mtoto wake. Wafungueni mkawalete kwangu. 3Kama mtu akiwauliza sababu, mwambieni, ‘Bwana anawahitaji,’ naye atawaachieni mara.” 4Jambo hili lilifanyika ili yale yaliyosemwa na nabii yatimie:
5“Uambieni mji wa Siyoni:
Tazama, Mfalme wako anakujia!
Ni mpole na amepanda punda,
mwanapunda, mtoto wa punda.”
6Hivyo, wale wanafunzi walikwenda wakafanya kama Yesu alivyowaagiza. 7Wakamleta yule punda na mtoto wake, wakatandika nguo zao juu yao na Yesu akaketi juu yake. 8Umati mkubwa wa watu wakatandaza nguo zao barabarani, na watu wengine wakakata matawi ya miti wakayatandaza barabarani. 9#Taz Zab 118:25-26 Makundi ya watu waliomtangulia na wale waliomfuata wakapaza sauti:
“Sifa#21:9 Sifa: Kiebrania: Hosana. kwa Mwana wa Daudi!
Abarikiwe huyo ajaye kwa jina la Bwana!
Sifa kwa Mungu juu!”
10Yesu alipokuwa anaingia Yerusalemu, mji wote ukajaa ghasia. Watu wakawa wanauliza, “Huyu ni nani?” 11Watu katika ule umati wakasema, “Huyu ni nabii Yesu, kutoka Nazareti mji wa Galilaya.”
Yesu anawafukuza wafanyabiashara hekaluni
(Marko 11:15-19; Luka 19:45-48; Yoh 2:13-22)
12Basi, Yesu akaingia hekaluni, akawafukuza nje watu waliokuwa wanauza na kununua vitu ndani ya hekalu; akazipindua meza za wale waliokuwa wanavunja fedha, na viti vya wale waliokuwa wanauza njiwa. 13Akawaambia, “Imeandikwa katika Maandiko Matakatifu: ‘Nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala.’ Lakini nyinyi mmeifanya kuwa pango la wanyanganyi.”
14Vipofu na vilema wengine walimwendea huko hekaluni, naye Yesu akawaponya. 15Basi, makuhani wakuu na waalimu wa sheria walipoyaona maajabu aliyoyafanya Yesu, na pia watoto walipokuwa wanapaza sauti zao hekaluni wakisema: “Sifa kwa Mwana wa Daudi,” wakakasirika. 16#Taz Zab 8:2 Hivyo wakamwambia, “Je, husikii wanachosema?” Yesu akawajibu, “Naam, nasikia! Je hamjapata kusoma Maandiko haya?
‘Kwa vinywa vya watoto wadogo na wachanga
wajipatia sifa kamili.’”
17Basi, akawaacha, akatoka nje ya mji na kwenda Bethania, akalala huko.
Mtini usiozaa
(Marko 11:12-14,20-24)
18Yesu alipokuwa anarudi mjini asubuhi na mapema, aliona njaa. 19Akauona mtini mmoja kando ya njia, akauendea; lakini aliukuta hauna chochote ila majani matupu. Basi, akauambia, “Usizae tena matunda milele!” Papo hapo huo mtini ukanyauka. 20Wanafunzi walipouona walishangaa wakisema, “Kwa nini mtini huu umenyauka ghafla?” 21Yesu akawajibu, “Kweli nawaambieni, kama mkiwa na imani bila kuwa na mashaka, mnaweza si tu kufanya hivyo, bali hata mkiuambia mlima huu: ‘Ngoka ukajitose baharini,’ itafanyika hivyo. 22Na mkiwa na imani, chochote mtakachoomba kwa sala, mtapata.”
Suala juu ya mamlaka ya Yesu
(Marko 11:27-33; Luka 20:1-8)
23Yesu aliingia hekaluni, akawa anafundisha. Alipokuwa akifundisha, makuhani wakuu na wazee wa watu wakamwuliza, “Unafanya mambo haya kwa mamlaka gani? Nani amekupa mamlaka haya?”
24Yesu akawajibu, “Na mimi nitawaulizeni swali moja; mkinijibu, basi nami nitawaambia ninafanya mambo haya kwa mamlaka gani. 25Je, mamlaka ya Yohane ya kubatiza yalitoka kwa nani? Je, yalitoka mbinguni ama kwa watu?” Lakini wakajadiliana wao kwa wao hivi: “Tukisema, ‘Yalitoka mbinguni,’ atatuuliza, ‘Basi, mbona hamkumsadiki?’ 26Na tukisema, ‘Yalitoka kwa watu,’ tunaogopa umati wa watu maana wote wanakubali kwamba Yohane ni nabii.” 27Basi, wakamjibu, “Hatujui!” Naye Yesu akawaambia, “Nami pia sitawaambia ninafanya mambo haya kwa mamlaka gani.
Mfano wa wana wawili
28“Nyinyi mnaonaje; mtu mmoja alikuwa na wana wawili. Akamwambia yule wa kwanza, ‘Mwanangu, leo nenda ukafanye kazi katika shamba la mizabibu.’ 29Yule kijana akamwambia, ‘Sitaki!’ Lakini baadaye akabadili nia, akaenda kufanya kazi. 30Yule baba akamwambia mtoto wake wa pili vivyo hivyo, naye akamjibu, ‘Naam baba!’ Lakini hakuenda kazini. 31Je, ni nani kati ya hawa wawili aliyetimiza matakwa ya baba yake?” Wakamjibu, “Yule mtoto wa kwanza.”
Basi, Yesu akawaambia, “Kweli nawaambieni, watozaushuru na waasherati wataingia katika ufalme wa Mungu kabla yenu. 32Maana Yohane alikuja kwenu akawaonesha njia adili ya kuishi, nanyi hamkumwamini; lakini watozaushuru na waasherati walimwamini. Hata baada ya kuona hayo yote nyinyi hamkutubu na kumsadiki.”
Mfano wa shamba la mizabibu na wakulima
(Marko 12:1-12; Luka 20:9-19)
33Yesu akasema, “Sikilizeni mfano mwingine. Mtu mmoja mwenye nyumba alilima shamba la mizabibu; akalizungushia ukuta, akachimba kisima cha kusindikia divai, akajenga humo mnara pia. Kisha akalikodisha kwa wakulima, akasafiri kwenda hadi nchi ya mbali. 34Wakati wa mavuno ulipofika, aliwatuma watumishi wake kwa wale wakulima, ili wakachukue sehemu ya mavuno yake. 35Wale wakulima wakawakamata hao watumishi; mmoja wakampiga, mwingine wakamuua na mwingine wakampiga mawe. 36Huyo mtu akawatuma tena watumishi wengine, wengi kuliko wa safari ya kwanza. Wale wakulima wakawatendea namna ileile. 37Mwishowe akamtuma mwanawe huku akifikiri: ‘Watamjali mwanangu.’ 38Lakini wale wakulima walipomwona mwanawe wakasemezana wao kwa wao: ‘Huyu ndiye mrithi; na tumuue ili tuuchukue urithi wake!’ 39Basi, wakamkamata, wakamtoa nje ya lile shamba la mizabibu, wakamuua.
40“Sasa, huyo mwenye shamba la mizabibu atakapokuja, atawafanyaje hao wakulima?” 41Wao wakamjibu, “Atawaangamiza vibaya hao waovu, na lile shamba atawapa wakulima wengine ambao watampa sehemu ya mavuno wakati wake.”
42 # Taz Zab 118:22-23 Hapo Yesu akawaambia, “Je, hamkusoma jambo hili katika Maandiko Matakatifu?
‘Jiwe walilokataa waashi
sasa limekuwa jiwe kuu la msingi.
Bwana ndiye aliyefanya jambo hili,
nalo ni la ajabu sana kwetu!’
43“Kwa hiyo nawaambieni, ufalme wa Mungu utaondolewa kwenu na kupewa watu wa mataifa mengine wenye kutoa matunda yake.” 44Atakayeanguka juu ya jiwe hilo atavunjika vipandevipande; na likimwangukia mtu yeyote, litamponda” (taz. Luka 20:18).
45Makuhani wakuu na Mafarisayo waliposikia hiyo mifano yake walitambua kwamba alikuwa anawasema wao. 46Kwa hiyo wakawa wanatafuta njia ya kumtia nguvuni, lakini waliwaogopa watu kwa sababu wao walimtambua yeye kuwa nabii.
Currently Selected:
Mathayo 21: BHN
Highlight
Share
Copy
Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.