YouVersion Logo
Search Icon

Mika 4

4
Mungu atatawala watu wote kwa amani
(Isa 2:1-4)
1Utakuja wakati ambapo
mlima wa nyumba ya Mwenyezi-Mungu
utakuwa mkubwa kuliko milima yote.
Naam, utakwezwa juu ya vilima vyote.
Watu wengi watamiminika huko,
2mataifa mengi yataujia na kusema:
“Twendeni juu kwenye mlima wa Mwenyezi-Mungu,
twende katika nyumba ya Mungu wa Yakobo,
ili atufundishe njia zake,
nasi tufuate nyayo zake.
Maana mwongozo utatoka huko Siyoni;
neno la Mwenyezi-Mungu huko Yerusalemu.”
3Mungu atasuluhisha mizozo ya mataifa mengi,
atakata mashauri ya mataifa makubwa ya mbali.
Nayo yatafua mapanga yao kuwa majembe,
na mikuki yao kuwa miundu ya kupogolea.
Taifa halitapigana na taifa lingine,
wala hayatafanya tena mazoezi ya vita.
4Kila mtu atakaa kwa amani
chini ya mitini na mizabibu yake,
bila kutishwa na mtu yeyote.
Mwenyezi-Mungu wa majeshi, ametamka yeye mwenyewe.
5Mataifa mengine hufuata njia zao,
kwa kuitegemea miungu yao,
lakini sisi twafuata njia zetu kwa kumtegemea Mwenyezi-Mungu,
Mungu wetu, milele na milele.
Waisraeli watarudi kutoka utumwani
6Mwenyezi-Mungu asema,
“Siku ile nitawakusanya walemavu,
naam, nitawakusanya waliochukuliwa uhamishoni,
watu wale ambao niliwaadhibu.
7Hao walemavu ndio watakaobaki hai;
hao waliochukuliwa uhamishoni watakuwa taifa lenye nguvu.
Nami Mwenyezi-Mungu nitawatawala mlimani Siyoni,
tangu wakati huo na hata milele.”
8Nawe kilima cha Yerusalemu,
wewe ngome ya Siyoni,
ambamo Mungu anafanya ulinzi juu ya watu wake,
kama mchungaji juu ya kondoo wake;
wewe utakuwa tena mji maarufu kama hapo awali,
Yerusalemu utakuwa tena mji mkuu wa mfalme.
9Sasa kwa nini mnalia kwa sauti?
Je, hamna mfalme tena?
Mshauri wenu ametoweka?
Mnapaza sauti ya uchungu,
kama mama anayejifungua!
10Enyi watu wa Siyoni,
lieni na kugaagaa kama mama anayejifungua!
Maana sasa mtaondoka katika mji huu
mwende kukaa nyikani,
mtakwenda mpaka Babuloni.
Lakini huko, mtaokolewa.
Huko Mwenyezi-Mungu atawakomboa makuchani mwa adui zenu.
11Mataifa mengi yamekusanyika kuwashambulia.
Yanasema: “Acheni mji wao utiwe najisi,
nasi tuyaone magofu ya Siyoni!”
12Lakini wao
hawafahamu mawazo ya Mwenyezi-Mungu
wala hawaelewi mpango wake:
Kwamba amewakusanya pamoja,
kama miganda mahali pa kupuria.
13Mwenyezi-Mungu asema,
“Enyi watu wa Siyoni,
inukeni mkawaadhibu adui zenu!
Nitawapeni nguvu kama fahali
mwenye pembe za chuma na kwato za shaba.
Mtawasaga watu wa mataifa mengi;
mapato yao mtaniwekea wakfu mimi,
mali zao mtanitolea mimi Bwana wa dunia yote.”

Currently Selected:

Mika 4: BHN

Highlight

Share

Copy

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in

Video for Mika 4