YouVersion Logo
Search Icon

Hesabu 34

34
Mipaka ya nchi
1Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, 2“Waamuru Waisraeli ukisema: Mtakapoingia Kanaani, nchi ambayo ninawapa iwe nchi yenu, mipaka ya eneo lenu lote itakuwa kama ifuatavyo. 3Upande wa kusini mpaka wenu utakuwa kutoka jangwa la Sini kupitia upande wa Edomu. Utaanzia mashariki upande wa kusini mwisho wa Bahari ya Chumvi. 4Kisha utapinda kusini kuelekea pito la Akrabimu na kupitia Sini hadi Kadesh-barnea, upande wa kusini. Kutoka hapo, mpaka utapinda kuelekea kaskazini-magharibi hadi Hasar-adari na kupita hadi Azmoni. 5Kutoka Azmoni utapinda kuelekea kijito cha Misri kwenye mpaka wa Misri na kuishia bahari ya Mediteranea.
6“Mpaka wenu wa upande wa magharibi utakuwa bahari ya Mediteranea.
7“Mpaka wenu wa upande wa kaskazini utakuwa kama ifuatavyo: Kutoka bahari ya Mediteranea, mtatia alama hadi Mlima Hori. 8Kutoka Mlima Hori mtatia alama hadi pito la Hamathi, na kuendelea hadi Sedadi, 9na kupita hadi Zifroni na kuishia Hazar-enani; huo utakuwa mpaka wenu wa kaskazini.
10“Mpaka wenu wa upande wa mashariki mtauweka kutoka Hazar-enani hadi Shefamu. 11Kutoka Shefamu utaelekea kusini hadi Ribla, mashariki mwa Aini; kisha mpaka huo utakwenda chini hadi mteremko wa mashariki wa ziwa Kinerethi,#34:11 Kinerethi: Ziwa Galilaya. 12halafu utateremka kufuata mto Yordani hadi Bahari ya Chumvi; hii ndiyo itakuwa nchi yako kama mpaka ulivyo.”
13 # Taz Yosh 14:1-5 Basi, Mose akawaambia Waisraeli, “Hii ndiyo nchi mtakayoirithi kwa kupiga kura, nchi ambayo Mwenyezi-Mungu ameagiza yapewe makabila tisa na nusu. 14Kabila la Reubeni na la Gadi, na nusu ya kabila la Manase yamepata urithi wao kulingana na koo zao. 15Makabila hayo mawili na nusu yamepata urithi wao ngambo ya mto Yordani upande wa mashariki, mkabala wa Yeriko, mawioni.”
Viongozi watakaosimamia mgawanyo wa nchi
16Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, 17“Kuhani Eleazari na Yoshua mwana wa Nuni ndio watakaowagawia watu nchi kuwa mali yao. 18Utachukua pia kiongozi mmoja kutoka kila kabila kusaidia katika ugawaji wa nchi. 19Haya ndiyo majina yao:
Kabila la Yuda, Kalebu mwana wa Yefune.
20Kabila la Simeoni, Shemueli mwana wa Amihudi.
21Kabila la Benyamini, Elidadi mwana wa Kisloni.
22Kabila la Dani, Buki mwana wa Yogli.
23Kabila la Manase mwanawe Yosefu, Hanieli mwana wa Efodi.
24Kabila la Efraimu, mwanawe Yosefu, Kemueli mwana wa Shiftani.
25Kabila la Zebuluni, Elisafani mwana wa Parnaki.
26Kabila la Isakari, Paltieli mwana wa Azani.
27Kabila la Asheri, Ahihudi mwana wa Shelomi
28Kabila la Naftali, Pedaheli mwana wa Amihudi.
29Hawa ndio watu ambao Mwenyezi-Mungu aliwaamuru wawagawie Waisraeli nchi ya Kanaani kuwa mali yao.”

Currently Selected:

Hesabu 34: BHN

Highlight

Share

Copy

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in