YouVersion Logo
Search Icon

Methali 16

16
1Binadamu hupanga mipango yake,
lakini kauli ya mwisho ni yake Mwenyezi-Mungu.
2Matendo ya mtu huonekana kwake kuwa sawa,
lakini Mwenyezi-Mungu hupima nia ya mtu.
3Mwekee Mwenyezi-Mungu kazi yako,
nayo mipango yako itafanikiwa.
4Mwenyezi-Mungu ameumba kila kitu kwa kusudi lake;
hata waovu kwa ajili ya siku ya maangamizi.
5Kila mwenye kiburi ni chukizo kwa Mwenyezi-Mungu;
hakika mtu wa namna hiyo hataacha kuadhibiwa.
6Kwa utii na uaminifu mtu huondolewa dhambi,
kwa kumcha Mwenyezi-Mungu huepuka uovu.
7Mwenyezi-Mungu akipendezwa na mwenendo wa mtu,
huwageuza hata adui zake kuwa marafiki.
8Afadhali mali kidogo kwa uadilifu,
kuliko mapato mengi kwa udhalimu.
9Mtu aweza kufanya mipango yake,
lakini Mwenyezi-Mungu huongoza hatua zake.
10Mfalme huamua kwa maongozi ya Mungu;
anapotoa hukumu hakosei.
11Mwenyezi-Mungu hutaka kipimo na mizani halali;
mawe yote mfukoni ya kupimia ni kazi yake.
12Ni chukizo kubwa wafalme kutenda uovu,
maana msingi wa mamlaka yao ni haki.
13Mfalme hupendelea mtu asemaye kwa unyofu;
humpenda mtu asemaye ukweli.
14Hasira ya mfalme ni kama mjumbe wa kifo;
mtu mwenye busara ataituliza.
15Uso wa mfalme ukingaa kuna uhai;
wema wake ni kama wingu la masika.
16Kupata hekima ni bora kuliko dhahabu;
kupata akili ni chaguo bora kuliko fedha.
17Njia ya wanyofu huepukana na uovu;
anayechunga njia yake huhifadhi maisha yake.
18Kiburi hutangulia maangamizi;
majivuno hutangulia maanguko.
19Afadhali kuwa mnyenyekevu na kuwa maskini,
kuliko kugawana nyara na wenye kiburi.
20Anayezingatia mafundisho atafanikiwa;
heri mtu yule anayemtumainia Mwenyezi-Mungu.
21Mwenye hekima moyoni huitwa mwenye akili;
neno la kupendeza huwavutia watu.
22Hekima ni chemchemi ya uhai kwake aliye nayo,
bali upumbavu ni adhabu ya wapumbavu.
23Moyo wa mwenye hekima humwezesha kusema kwa busara;
huyafanya maneno yake yawe ya kuvutia.
24Maneno mazuri ni kama asali;
ni matamu rohoni na yenye kuupa mwili afya.
25 # Taz Meth 14:12 Mtu aweza kuona njia yake kuwa sawa,
lakini mwishowe humwongoza kwenye kifo.
26Hamu ya chakula humhimiza mfanyakazi,
maana njaa yake humsukuma aendelee.
27Mtu mwovu hupanga uovu;
maneno yake ni kama moto mkali.
28Mtu mpotovu hueneza ugomvi,
mfitini hutenganisha marafiki.
29Mtu mkatili humshawishi jirani yake;
humwongoza katika njia mbaya.
30Anayekonyeza jicho kwa hila amepanga maovu;
anayekaza midomo amekwisha nuia mabaya.
31Kuwa na mvi za uzee ni taji la utukufu;
hupatikana kwa maisha ya uadilifu.
32Asiye mwepesi wa hasira ni bora kuliko mwenye nguvu;
aitawalaye nafsi yake ni bora kuliko autekaye mji.
33Kura hupigwa kujua yatakayotukia,
lakini uamuzi ni wake Mwenyezi-Mungu.

Currently Selected:

Methali 16: BHN

Highlight

Share

Copy

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in