Methali 5
5
Onyo dhidi ya uasherati
1Mwanangu, sikia hekima yangu,
tega sikio usikilize elimu yangu.
2Ndipo utakapoweza kuhifadhi busara,
na midomo yako izingatie maarifa.
3Mdomo wa mwanamke mpotovu ni mtamu kama asali,
maneno yake ni laini kuliko mafuta;#5:3-5 Kuhusu aya 3-5 Taz pia 2:16; 7:6-27; 22:14; Mhu 7:26
4lakini hatimaye ni mchungu kama pakanga,
ni mkali kama upanga wenye makali kuwili.
5Nyayo zake zaelekea chini mautini,
hatua zake zaenda kuzimu.
6Yeye haijali njia ya uhai,
njia zake ni za kutangatanga, wala hajui.
7Sasa enyi wanangu, nisikilizeni,
wala msisahau maneno ya kinywa changu.
8Iepushe njia yako mbali naye,
wala usiukaribie mlango wa nyumba yake.
9Usije ukawapa wengine heshima yako,
na wakatili miaka yako;
10wageni wasije wakajishibisha kwa mali yako,
na jasho lako likaishia nyumbani kwa mgeni.
11Mwishoni mwa maisha yako utaomboleza
wakati mwili wako utakapoangamizwa.
12Hapo utasema, “Jinsi gani nilivyochukia nidhamu,
na kudharau maonyo moyoni mwangu!
13Sikuisikiliza sauti ya waalimu wangu,
wala kuwategea sikio wakufunzi wangu.
14Sasa niko karibu kuangamia kabisa
mbali na jumuiya ya watu.”
15Mkeo ni kama kisima cha maji safi:
Kunywa maji ya kisima chako mwenyewe.
16Ya nini chemchemi zako zitawanywe mbali,
na vijito vya maji barabarani?
17Hiyo ni yako wewe mwenyewe,
wala usiwashirikishe watu wengine.
18Chemchemi yako na ibarikiwe,
umfurahie mke uliyemwoa ukiwa kijana.
19Ni mzuri kama ayala, apendeza kama paa.
Mahaba yake yakufurahishe kila wakati,
umezwe daima na pendo lake.
20Mwanangu, ya nini kutekwa na mwanamke mwasherati?
Ya nini kumkumbatia kifuani mwanamke mgeni?
21Kumbuka njia za mtu zi wazi mbele ya Mwenyezi-Mungu;
yeye anaona kila hatua anayochukua binadamu.
22Mtu mwovu hunaswa kwa uovu wake mwenyewe;
hukamatwa katika tanzi za dhambi yake mwenyewe.
23Yeye hufa kwa utovu wa nidhamu,
huangamia kwa sababu ya upuuzi wake mkuu.
Currently Selected:
Methali 5: BHN
Highlight
Share
Copy
Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.