Zaburi 105
105
Mungu na watu wake
(1Nya 16:8-22)
1Mshukuruni Mwenyezi-Mungu, tangazeni ukuu wake;
yajulisheni mataifa mambo aliyotenda!
2Mshangilieni, mwimbieni Mungu sifa;
simulieni matendo yake ya ajabu!
3Jisifieni jina lake takatifu;
wenye kumcha Mwenyezi-Mungu na wafurahi.
4Tafuteni msaada kwa Mwenyezi-Mungu mwenye nguvu;
mwendeeni Mwenyezi-Mungu daima.
5Kumbukeni matendo ya ajabu aliyotenda,
miujiza yake na hukumu alizotoa,
6enyi wazawa wa Abrahamu mtumishi wake,
enyi wazawa wa Yakobo, wateule wake;
7Yeye ndiye Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu;
hukumu zake zina nguvu duniani kote.
8Yeye hulishika agano lake milele,
hutimiza ahadi zake kwa vizazi elfu.
9Hushika agano alilofanya na Abrahamu,
na ahadi aliyomwapia Isaka.
10Alimthibitishia Yakobo ahadi yake,
alimhakikishia Israeli agano hilo la milele.
11Alisema: “Nitawapeni nchi ya Kanaani,
nayo itakuwa mali yenu wenyewe.”
12Watu wa Mungu walikuwa wachache; hawakuwa maarufu,
tena walikuwa wageni nchini Kanaani.
13Walitangatanga kutoka taifa hadi taifa;
kutoka nchi moja hadi nchi nyingine.
14Lakini Mungu hakuruhusu mtu awadhulumu;
kwa ajili yao aliwaonya wafalme:
15“Msiwaguse wateule wangu;
msiwadhuru manabii wangu!”
16Mungu alizusha njaa nchini mwao,
akaharibu chakula chao chote.
17Lakini aliwatangulizia mtu mmoja,
Yosefu aliyekuwa ameuzwa utumwani.
18Walimfunga miguu kwa minyororo,
na shingoni kwa nira ya chuma,
19Muda si muda alichotabiri kilitimia.
neno la Mwenyezi-Mungu lilimdhibiti.
20Mfalme wa Misri akaamuru afunguliwe;
mtawala wa mataifa akamwachilia huru.
21Alimweka kuwa mkurugenzi wa serikali yake,
na mkuu wa mali yake yote;
22awaongoze maofisa wake apendavyo,
na kuwafundisha wazee wake hekima.
23Ndipo Israeli akaingia nchini Misri;
Yakobo akawa mgeni katika nchi ya Hamu.
24Mwenyezi-Mungu akawafanya watu wake wazae sana;
akawajalia nguvu kuliko maadui zao.
25Aliwafanya Wamisri wawachukie watu wake,
wakawatendea hila watumishi wake.
26Kisha akamtuma Mose mtumishi wake,
akamtuma na Aroni mteule wake.
27Wakafanya ishara za Mungu kati ya Wamisri,
na miujiza katika nchi hiyo ya Hamu.
28Mungu akaleta giza juu ya nchi;
lakini Wamisri wakakataa kutii amri zake.#105:28 wakakataa kutii amri zake: Hivyo katika hati kadha za kale. Kiebrania: Wakatii.
29Akageuza mito yao kuwa damu,
akawaua samaki wao wote.
30Vyura wakaivamia nchi yao,
hata jumba la mfalme likajawa nao.
31Mungu akanena, kukazuka makundi ya nzi,
na viroboto katika nchi yote.
32Badala ya mvua akawapa mvua ya mawe,
na umeme uliomulika nchi yao yote;
33akaharibu mizabibu na mitini yao,
akaivunja pia miti ya nchi yao.
34Mungu akanena, kukazuka nzige,
na panzi maelfu yasiyohesabika;
35wakaitafuna mimea yote katika nchi,
wakayala mazao yao yote.
36Aliwaua wazaliwa wa kwanza nchini mwao,
chipukizi wa kwanza wa jamaa za Wamisri.
37Kisha akawatoa watu wa Israeli nchini,
wakiwa na fedha na dhahabu;
wala hakuna hata mmoja wao aliyejikwaa.
38Wamisri walifurahia kuondoka kwao,
kwani hofu iliwashika kwa sababu yao.
39Mungu alitandaza wingu juu ya watu wake,
na moto ili kuwaangazia usiku.
40Waliomba#105:40 Waliomba: Makala nyingine za kale; Aliomba. naye akawaletea kware,
akawapa mkate kutoka mbinguni kwa wingi.
41Alipasua mwamba maji yakabubujika;
yakatiririka jangwani kama mto.
42Aliikumbuka ahadi yake takatifu,
aliyompa Abrahamu mtumishi wake.
43Basi akawatoa watu wake nchini,
wateule wake wakaimba na kushangilia.
44Aliwapa nchi za mataifa mengine
na kuwakabidhi mashamba ya wenyeji;
45kusudi watu wake watii masharti yake,
na kufuata sheria zake.
Asifiwe Mwenyezi-Mungu!
Currently Selected:
Zaburi 105: BHN
Highlight
Share
Copy
Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.