Zaburi 144
144
Shukrani kwa ushindi
(Zaburi ya Daudi)
1Atukuzwe Mwenyezi-Mungu, mwamba wangu,
anayeipa mikono yangu mazoezi ya vita,
na kuvifunza vidole vyangu kupigana.
2Yeye ni rafiki yangu amini na ngome yangu,
kinga yangu na mkombozi wangu;
yeye ni ngao yangu, kwake napata usalama;
huyashinda mataifa na kuyaweka chini yangu.
3 # Taz Zab 8:4 Ee Mwenyezi-Mungu, mtu ni nini hata umjali?
Mwanadamu ni nini hata umfikirie?
4Binadamu ni kama pumzi tu;
siku zake ni kama kivuli kipitacho.
5Uinamishe mbingu zako, ee Mwenyezi-Mungu, ushuke chini!
Uiguse milima nayo itoe moshi!
6Lipusha umeme, uwatawanye maadui;
upige mishale yako, uwakimbize!
7Unyoshe mkono wako kutoka juu,
uniokoe na kuniondoa katika maji haya mengi;
uniondoe makuchani mwa wageni,
8ambao husema maneno ya uongo,
hunyosha mkono kushuhudia uongo.
9Nitakuimbia wimbo mpya, ee Mungu;
nitakupigia kinubi cha nyuzi kumi,
10wewe uwapaye wafalme ushindi,
umwokoaye Daudi mtumishi wako!
11Uniokoe na upanga wa adui katili,
uniondoe makuchani mwa wageni,
ambao husema maneno ya uongo,
hunyosha mkono kushuhudia uongo.
12Wavulana wetu wakue kikamilifu kama mimea bustanini;
binti zetu wawe kama nguzo zilizochongwa kupambia ikulu.
13Ghala zetu zijae mazao ya kila aina.
Kondoo wetu mashambani wazae maelfu kwa maelfu.
14Mifugo yetu iwe na afya na nguvu;
isitupe mimba wala kuzaa kabla ya wakati.
Kusiwepo tena udhalimu mitaani mwetu.
15Heri taifa ambalo limejaliwa hayo!
Heri taifa ambalo Mungu wao ni Mwenyezi-Mungu!
Currently Selected:
Zaburi 144: BHN
Highlight
Share
Copy
Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.