Zaburi 83
83
Sala dhidi ya adui za Israeli
(Zaburi ya Asafu. Wimbo)
1Ee Mungu, usikae kimya!
Usinyamaze ee Mungu, wala usitulie!
2Tazama! Maadui zako wanafanya ghasia;
wanaokuchukia wanainua vichwa kwa kiburi.
3Wanapanga kwa hila kuwadhuru watu wako;
wanashauriana dhidi ya hao unaowalinda.
4Wanasema: “Njoni tuliangamize taifa lao,
jina la Israeli lisikumbukwe tena.”
5Naam, wanakubaliana kwa moyo mmoja,
wanakula kiapo dhidi yako:
6Watu wa Edomu na Waishmaeli,
Wamoabu na watu wa Hagari;
7watu wa Gebali, Amoni na Amaleki,
watu wa Filistia na wakazi wa Tiro.
8Hata Ashuru imeshirikiana nao,
imewaunga mkono wazawa wa Loti!
9Uwatende ulivyowatenda watu wa Midiani,
ulivyowatenda Sisera na Yabini mtoni Kishoni,
10watu uliowaangamiza kule Endori,
wakawa takataka juu ya nchi.
11Uwatende wakuu wao kama Orebu na Zeebu;
watawala wao wote kama Zeba na Zalmuna,
12ambao walisema: “Tutajitekea nchi ya Mungu.”
13Ee Mungu wangu, uwafanye kama vumbi;
kama makapi yapeperushwayo na upepo.
14Kama vile moto unavyoteketeza msitu,
na miali ya moto inavyounguza milima,
15uwakimbize hao kwa tufani yako,
na kuwatisha kwa kimbunga chako!
16Uzijaze nyuso zao fedheha,
wapate kukutafuta, ee Mwenyezi-Mungu.
17Waone fedheha na kuhangaika milele,
waangamie kwa aibu kabisa.
18Wajue kwamba wewe peke yako
ambaye jina lako ni Mwenyezi-Mungu,
ndiwe Mungu Mkuu juu ya dunia yote.
Currently Selected:
Zaburi 83: BHN
Highlight
Share
Copy
Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.