Zaburi 88
88
Kilio cha msaada
(Wimbo. Zaburi ya Wakorahi. Kwa Mwimbishaji: Mtindo wa Mahalathi Nealothi. Utenzi wa Hemani Mwezrahi)
1Ee Mwenyezi-Mungu, mwokozi wangu,
ninalia mchana kutwa,
na usiku nakulalamikia.
2Sala yangu ikufikie,
usikilize kilio changu.
3Maafa mengi yamenipata,
nami niko karibu kufa.
4Ninaonekana kama mtu anayekufa,
nguvu zangu zote zimeniishia.
5Nimesahauliwa kati ya wafu,
kama waliouawa, walioko kaburini;
kama wale ambao huwakumbuki tena,
ambao wametengwa na ulinzi wako.
6Umenitupa katika kina cha kaburi;
katika sehemu za giza na kina kikuu.
7Hasira yako imenilemea;
umenisonga kwa mawimbi yako yote.
8Umewafanya rafiki zangu waniepe,
umenifanya kuwa chukizo kwao.
Nimefungwa ndani, wala siwezi kutoroka;
9macho yangu yamefifia kwa huzuni.
Kila siku nakulilia, ee Mwenyezi-Mungu;
ninakunyoshea mikono yangu.
10Je, wewe huwatendea wafu maajabu yako?
Je, mizimu hufufuka na kukusifu?
11Je, fadhili zako zinatajwa kaburini,
au uaminifu wako kwenye makao ya maangamizi?
12Je, maajabu yako yanajulikana humo gizani,
au wema wako katika nchi ya waliosahauliwa?
13Lakini mimi nakulilia, ee Mwenyezi-Mungu;
kila asubuhi nakuletea ombi langu.
14Mbona ee Mwenyezi-Mungu wanitupilia mbali?
Kwa nini unanificha uso wako?
15Nimeteseka na kukaribia kifo tangu ujana wangu;
nateseka kwa mapigo yako, niko hoi kabisa.
16Ghadhabu yako imeniwakia;
mashambulio yako ya kutisha yananiangamiza.
17Yananizunguka kama mafuriko mchana kutwa;
yananizingira yote kwa pamoja.
18Umewafanya rafiki na wenzangu wote waniepe;
giza ndilo limekuwa mwenzangu.
Currently Selected:
Zaburi 88: BHN
Highlight
Share
Copy
Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.