Matendo 5

5
Anania na Safira
1Lakini mtu mmoja jina lake Anania, pamoja na Safira mkewe, aliuza mali, 2#Mdo 4:37 akihifadhi kwa siri sehemu ya thamani yake, mkewe naye akijua haya, akaleta fungu moja akaliweka miguuni pa mitume. 3#Yn 13:2 Petro akasema, Anania, kwa nini Shetani amekujaza moyo wako kumwambia uongo Roho Mtakatifu, na kuhifadhi kwa siri sehemu ya thamani ya kiwanja? 4Kilipokuwa kwako, hakikuwa mali yako? Na kilipokuwa kimekwisha kuuzwa, thamani yake haikuwa katika uwezo wako? Ilikuwaje hata ukaweka neno hili moyoni mwako? Hukumwambia uongo mwanadamu, bali Mungu. 5Anania aliposikia maneno haya akaanguka, akafa. Hofu nyingi ikawapata watu wote walioyasikia haya. 6Vijana wakaondoka, wakamtia katika sanda, wakamchukua nje, wakamzika.
7Hata muda wa saa tatu baadaye mkewe akaingia, naye hana habari ya hayo yaliyotokea. 8Petro akamjibu, Niambie, Mlikiuza kiwanja kwa thamani hiyo? Akasema, Ndiyo, kwa thamani hiyo. 9Petro akamwambia, Imekuwaje hata mkapatana kumjaribu Roho wa Bwana? Angalia, miguu yao waliomzika mumeo ipo mlangoni, nao watakuchukua nje wewe nawe. 10Mara akaanguka miguuni pake akafa; wale vijana wakaingia wakamkuta amekufa, wakamchukua nje, wakamzika pamoja na mumewe. 11Hofu nyingi ikalipata kanisa lote na watu wote walioyasikia haya.
Mitume waponya wengi
12 # Mdo 3:11 Na kwa mikono ya mitume zikafanyika ishara na maajabu mengi katika watu; nao wote walikuwako kwa nia moja katika ukumbi wa Sulemani; 13na katika wote wengine hapana hata mmoja aliyethubutu kuambatana nao; ila watu waliwaadhimisha; 14#Mdo 2:47; 6:7; 21:20 walioamini wakazidi kuongezeka kwa Bwana, wengi, wanaume na wanawake; 15#Mdo 19:11,12; Mk 6:56 hata ikawa katika njia kuu hutoa nje wagonjwa, na kuwaweka juu ya mikeka na magodoro, ili Petro akija, ngawa kivuli chake kimwangukie mmojawapo wao. 16Nayo makundi ya watu wa miji iliyoko kandokando ya Yerusalemu wakakutanika, wakileta wagonjwa, nao walioudhiwa na pepo wachafu; nao wote wakaponywa.
Mitume wateswa
17 # Mdo 4:1,6 Akaondoka Kuhani Mkuu na wote waliokuwa pamoja naye, (hao ndio walio wa madhehebu ya Masadukayo), wamejaa wivu, 18wakawakamata mitume wakawaweka ndani ya gereza; 19#Mdo 12:7 lakini malaika wa Bwana akafungua milango ya gereza usiku, akawatoa, akasema, 20Nendeni mkasimame hekaluni mkawaambie watu maneno yote ya Uzima huu. 21Nao waliposikia wakaenda alfajiri hekaluni, wakaanza kufundisha.
Akaja Kuhani Mkuu nao waliokuwa pamoja naye, wakawakutanisha watu wa baraza, na wazee wote wa wana wa Israeli, wakatuma watu gerezani ili wawalete. 22Wakati watumishi walipofika hawakuwaona gerezani, wakarudi wakatoa habari, 23wakisema, Gereza tumeikuta imefungwa salama, nao walinzi wamesimama mbele ya mlango; lakini tulipoufungua hatukukuta mtu ndani. 24Basi mlinzi mkuu wa hekalu na wakuu wa makuhani waliposikia haya, wakaingiwa na shaka kwa ajili yao, litakuwaje jambo hilo. 25Mtu mmoja akaja akawapasha habari ya kwamba, Watu wale mliowaweka gerezani wako ndani ya hekalu, wamesimama wakiwafundisha watu. 26Ndipo yule jemadari akaenda pamoja na watumishi, wakawaleta, lakini si kwa nguvu, kwa maana waliogopa watu wasije wakawapiga kwa mawe. 27Walipowaleta, wakawaweka katika baraza. Kuhani Mkuu akawauliza, 28#Mt 27:25; Mdo 4:18 akisema, Je! Hatukuwaamuru ninyi kwa nguvu, msifundishe kwa jina hili? Nanyi, tazameni, mmeijaza Yerusalemu mafundisho yenu, na mnataka kuileta damu ya mtu yule juu yetu. 29#Mdo 4:19; Dan 3:18 Petro na mitume wakajibu, wakisema, Imetupasa kumtii Mungu kuliko wanadamu. 30#Kum 21:22; Mdo 3:15 Mungu wa baba zetu alimfufua Yesu, ambaye ninyi mlimwua mkimtundika katika mti. 31#Mdo 2:33; Ebr 2:10; 12:2 Mtu huyo Mungu amemtukuza kwa mkono wake wa kulia, awe Mkuu na Mwokozi, awape Waisraeli toba na msamaha wa dhambi. 32#Lk 24:48; Yn 15:26,27 Na sisi tu mashahidi wa mambo haya, pamoja na Roho Mtakatifu ambaye Mungu amewapa wote wanaomtii. 33#Mdo 7:54 Wao waliposikia wakachomwa mioyo yao; wakapanga kuwaua.
34 # Mdo 22:3 Lakini mtu mmoja, Farisayo, jina lake Gamalieli, mwalimu wa torati, mwenye kuheshimiwa na watu wote, akasimama katika baraza, akaamuru mitume wawekwe nje kitambo kidogo, 35akawaambia, Enyi wanaume wa Israeli, jihadharini jinsi mtakavyowatenda watu hawa. 36#Mdo 21:38 Kwa sababu kabla ya siku hizi aliondoka Theuda, akijidai ya kuwa yeye ni mtu mkuu, watu wapatao mia nne wakashikamana naye; naye aliuawa na wote waliomsadiki wakatawanyika wakawa si kitu. 37#Lk 2:2 Baada ya mtu huyo aliondoka Yuda Mgalilaya, siku zile za kuandikiwa orodha, akawavuta watu kadhaa nyuma yake, naye pia akapotea na wote waliomsadiki wakatawanyika. 38#Mt 15:13 Basi sasa nawaambia, Jiepusheni na watu hawa, waacheni; kwa kuwa shauri hili au kazi hii ikiwa imetoka kwa binadamu, itavunjwa, 39#Mdo 9:5 lakini ikiwa imetoka kwa Mungu hamwezi kuivunja; msije mkaonekana kuwa mnapigana na Mungu. 40#Mdo 22:19 Wakakubali maneno yake; nao walipowaita mitume, wakawapiga, wakawaamuru wasinene kwa jina lake Yesu; kisha wakawaacha waende zao. 41#Mt 5:10-12; 1 Pet 4:13 Nao wakatoka katika ile baraza, wakifurahi kwa sababu wamehesabiwa kuwa wamestahili kuaibishwa kwa ajili ya Jina hilo. 42#Mdo 18:5 Na kila siku, ndani ya hekalu na nyumbani mwao, hawakuacha kufundisha na kuhubiri Habari Njema za Yesu kwamba ni Kristo.

S'ha seleccionat:

Matendo 5: SRUVDC

Subratllat

Comparteix

Copia

None

Vols que els teus subratllats es desin a tots els teus dispositius? Registra't o inicia sessió