Yohana 11
11
Kifo cha Lazaro
1 #
Lk 10:38-39
Basi mtu mmoja alikuwa mgonjwa, Lazaro wa Bethania, mwenyeji wa mji wa Mariamu na Martha, dada yake. 2#Yn 12:3 Ndiye Mariamu yule aliyempaka Bwana marhamu, akamfuta miguu kwa nywele zake, ambaye Lazaro nduguye alikuwa mgonjwa. 3Basi wale dada wakatuma ujumbe kwake wakisema, Bwana, yeye umpendaye ni mgonjwa. 4#Yn 9:3 Naye Yesu aliposikia, alisema, Ugonjwa huu si wa mauti, bali ni kwa ajili ya utukufu wa Mungu, ili Mwana wa Mungu atukuzwe kwa huo. 5Naye Yesu alimpenda Martha na dada yake na Lazaro. 6Basi aliposikia ya kwamba ni mgonjwa, bado alikaa siku mbili pale pale alipokuwapo. 7Kisha, baada ya hayo, akawaambia wanafunzi wake, Twendeni Yudea tena. 8#Kum 15:11; Yn 8:59; 10:31 Wale wanafunzi wakamwambia, Rabi, juzi juzi tu Wayahudi walikuwa wakitafuta kukupiga kwa mawe, nawe unakwenda huko tena? 9#Yn 9:4,5; 1 Yoh 2:10 Yesu akajibu, Je! Saa za mchana si kumi na mbili? Mtu akienda mchana hajikwai; kwa sababu aiona nuru ya ulimwengu huu. 10#Yn 12:35; 1 Yoh 2:11 Bali akienda usiku hujikwaa; kwa sababu nuru haimo ndani yake. 11#Mt 9:24; Lk 8:52 Aliyasema hayo; kisha, baada ya hayo, akawaambia, Rafiki yetu, Lazaro, amelala; lakini ninakwenda nipate kumwamsha. 12Basi wale wanafunzi wakamwambia, Bwana, ikiwa amelala, atapona. 13Lakini Yesu alikuwa amenena habari ya mauti yake; nao walidhania ya kuwa ananena habari ya kulala usingizi. 14Basi hapo Yesu akawaambia waziwazi, Lazaro amekufa. 15#Zek 9:9 Nami nafurahi kwa ajili yenu kwamba sikuwako huko, ili mpate kuamini; lakini na twendeni kwake. 16#Mk 10:32; 14:31 Basi Tomaso, aitwaye Pacha, akawaambia wanafunzi wenziwe, Twendeni na sisi, ili tufe pamoja naye.
Yesu aliye ufufuo na uzima
17Basi Yesu alipofika, alimkuta amekwisha kuwamo kaburini yapata siku nne. 18Na Bethania ilikuwa karibu na Yerusalemu, kadiri ya maili mbili hivi; 19na watu wengi katika Wayahudi walikuwa wamekuja kwa Martha na Mariamu, ili kuwafariji kwa ajili ya ndugu yao. 20Basi Martha aliposikia kwamba Yesu anakuja, alikwenda kumlaki; na Mariamu alikuwa akikaa nyumbani. 21#Yn 3:32 Basi Martha akamwambia Yesu, Bwana, kama ungalikuwapo hapa, ndugu yangu hangalikufa. 22Lakini hata sasa najua ya kuwa yoyote utakayomwomba Mungu, Mungu atakupa. 23Yesu akamwambia, Ndugu yako atafufuka. 24#Yn 5:29; 6:40; Lk 14:14 Martha akamwambia, Najua ya kuwa atafufuka katika ufufuo siku ya mwisho. 25Yesu akamwambia, Mimi ndimi huo ufufuo, na uzima. Yeye aniaminiye mimi, hata akifa, atakuwa anaishi; 26#Yn 5:24; 8:51 naye kila aishiye na kuniamini hatakufa kabisa hata milele. Je! Unayasadiki hayo? 27#Yn 6:69 Akamwambia, Naam, Bwana, mimi nimesadiki ya kwamba wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu, yule ajaye ulimwenguni.
Yesu alia
28Naye alipokwisha kusema hayo, alikwenda zake; akamwita umbu lake Mariamu faraghani, akisema, Mwalimu yupo anakuita. 29Naye aliposikia, aliondoka upesi, akamwendea. 30#Yn 11:20 Na Yesu alikuwa hajafika ndani ya kijiji; lakini alikuwa angalipo pale pale alipomlaki Martha. 31Basi wale Wayahudi waliokuwapo na Mariamu nyumbani, wakimfariji, walipomwona jinsi alivyoondoka upesi na kutoka, walimfuata; huku wakidhania ya kuwa anakwenda kaburini ili alilie huko. 32#Yn 11:21 Basi Mariamu alipofika pale alipokuwapo Yesu, na kumwona, alianguka miguuni pake, akamwambia, Bwana, kama ungalikuwapo hapa, ndugu yangu hangalikufa. 33#Yn 13:21 Basi Yesu alipomwona analia, na wale Wayahudi waliofuatana naye wanalia, aliugua rohoni, akafadhaika roho yake, 34akasema, Mmemweka wapi? Wakamwambia, Bwana, njoo utazame. 35#Lk 19:41 Yesu akalia machozi. 36Basi Wayahudi wakasema, Angalieni jinsi alivyompenda. 37Bali wengine wao wakasema, Je! Huyu aliyemfumbua macho yule kipofu, hakuweza kumfanya na huyu asife?
Yesu amfufua Lazaro
38 #
Isa 53:1; Mt 27:60 Basi Yesu, akiwa na huzuni tena moyoni mwake, akafika kwenye kaburi. Nalo lilikuwa ni pango, na jiwe limewekwa juu yake. 39#Yn 20:1 Yesu akasema, Liondoeni jiwe. Martha, dada yake yule aliyefariki, akamwambia, Bwana, ananuka sasa; maana amekuwa maiti siku nne. 40#Isa 6:10; Yn 4:23,25,26 Yesu akamwambia, Mimi sikukuambia ya kwamba ukiamini utauona utukufu wa Mungu? 41Basi wakaliondoa lile jiwe. Yesu akainua macho yake juu, akasema, Baba, nakushukuru kwa kuwa umenisikia. 42#Yn 12:30 Nami nilijua ya kuwa wewe wanisikia sikuzote; lakini kwa ajili ya mkutano huu wanaohudhuria nilisema haya, ili wapate kusadiki kwamba ndiwe uliyenituma. 43Naye akiisha kusema hayo, akalia kwa sauti kuu, Lazaro, njoo huku nje. 44Akatoka nje yule aliyekufa, akiwa amefungwa sanda miguuni na mikononi, na uso wake amefungwa leso. Naye Yesu akawaambia, Mfungueni, mkamwache aende zake.
Njama za kumwua Yesu
45 #
Lk 16:31; Yn 10:42; 12:42 Basi wengi katika Wayahudi waliokuja kwa Mariamu, na kuyaona yale aliyoyafanya, wakamwamini. 46Lakini wengine wakaenda zao kwa Mafarisayo, wakawaambia aliyoyafanya Yesu.
47Basi wakuu wa makuhani na Mafarisayo wakakusanya baraza, wakasema, Tunafanya nini? Maana mtu huyu afanya ishara nyingi. 48Tukimwacha hivi, watu wote watamwamini; na Warumi watakuja, watatuondolea mahali petu na taifa letu. 49Mtu mmoja miongoni mwao, Kayafa, aliyekuwa Kuhani Mkuu mwaka ule, akawaambia, Ninyi hamjui neno lolote; 50#Yn 18:14 wala hamfikiri ya kwamba yafaa mtu mmoja afe kwa ajili ya watu, wala lisiangamie taifa zima. 51#Mwa 50:20; Kut 28:30; Hes 27:21 Na neno hilo yeye hakulisema kwa nafsi yake; bali kwa kuwa alikuwa Kuhani Mkuu mwaka ule, alitabiri ya kwamba Yesu atakufa kwa ajili ya taifa hilo. 52#Yn 10:16; 1 Yoh 2:2; Mt 12:30 Wala si kwa ajili ya taifa hilo tu; lakini pamoja na hayo awakusanye watoto wa Mungu waliotawanyika, ili wawe wamoja. 53Basi tangu siku ile walifanya shauri la kumwua.
54Kwa hiyo Yesu hakutembea tena kwa wazi katikati ya Wayahudi; bali alitoka huko, akaenda mahali karibu na jangwa, mpaka mji uitwao Efraimu; akakaa huko pamoja na wanafunzi wake. 55#2 Nya 30:17; Mk 10:32; Mdo 21:24,26 Na Pasaka ya Wayahudi ilikuwa karibu; na wengi wakakwea toka mashambani kwenda Yerusalemu kabla ya Pasaka, ili wajitakase. 56Basi wao wakamtafuta Yesu, wakasemezana wakiwa wamesimama hekaluni, Mwaonaje? Haji kabisa sikukuu hii? 57Na wakuu wa makuhani na Mafarisayo walikuwa wametoa amri ya kwamba mtu akimjua alipo, alete habari, ili wapate kumkamata.
S'ha seleccionat:
Yohana 11: SRUVDC
Subratllat
Comparteix
Copia
Vols que els teus subratllats es desin a tots els teus dispositius? Registra't o inicia sessió
Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.