Mathayo 13
13
Simulizi Kuhusu Mkulima Aliyepanda Mbegu
(Mk 4:1-9; Lk 8:4-8)
1Siku hiyo hiyo Yesu alitoka nje ya nyumba na kukaa kando ya ziwa. 2Kundi kubwa wakakusanyika kumzunguka. Hivyo akapanda mtumbwini na kuketi. Watu wote wakabaki ufukweni. 3Kisha Yesu akatumia simulizi kuwafundisha mambo mengi. Akawaambia simulizi hii:
“Mkulima alitoka kwenda kupanda mbegu. 4Alipokuwa anatawanya mbegu, baadhi ziliangukia njiani. Ndege wakaja na kuzila zote. 5Mbegu zingine ziliangukia kwenye ardhi yenye mawe, ambako hakukuwa na udongo wa kutosha. Zikakua haraka pale, kwa sababu udongo haukuwa na kina. 6Lakini jua lilipowaka, likaichoma mimea. Mimea ikafa kwa sababu haikuwa na mizizi mirefu. 7Baadhi ya mbegu ziliangukia katikati ya miiba. Miiba ikakua na kusababisha mimea mizuri kuacha kukua. 8Lakini baadhi ya mbegu ziliangukia kwenye udongo wenye rutuba. Hapo zikakua na kuzaa nafaka. Baadhi ya mimea ikazaa nafaka mara mia zaidi, baadhi mara sitini na baadhi mara thelathini zaidi. 9Ninyi watu mnaoweza kunisikia, nisikilizeni!”
Kwa nini Yesu Alitumia Simulizi Kufundisha
(Mk 4:10-12; Lk 8:9-10)
10Wafuasi wake wakamwendea Yesu na kumuuliza, “Kwa nini unatumia simulizi hizi kuwafundisha watu?”
11Yesu akawajibu, “Mungu amewapa ninyi ujuzi wa kuelewa siri za ufalme wa Mungu, lakini hajawapa watu hawa wengine ujuzi huu. 12Kisha akawaambia, ‘Zingatieni kwa makini kile mnachokisikia. Kwani jinsi mnavyosikiliza kwa makini, ndivyo mtakavyoelewa na kuzidi kuelewa. Kwa kuwa kila aliye na uelewa kidogo ataongezewa zaidi. Lakini wale wasiosikiliza kwa makini watapoteza hata ule uelewa mdogo walio nao.’ 13Ndiyo sababu ninatumia simulizi hizi kuwafundisha watu: Wanaona, lakini hakika hawaoni. Wanasikia, lakini hakika hawasikii au kuelewa. 14Hiyo inathibitisha alichosema nabii Isaya kuhusu wao kuwa kweli:
‘Ninyi watu mtasikia na kusikia,
lakini hamtaelewa.
Mtatazama na kutazama,
lakini hakika hamtaona.
15Ndiyo, akili za watu hawa sasa zimefungwa.
Wana masikio, lakini hawasikii vizuri.
Wana macho, lakini wameyafumba.
Iwapo akili zao zisingekuwa zimefungwa,
wangeona kwa macho yao;
wangesikia kwa masikio yao;
Iwapo wangeelewa kwa akili zao.
Kisha wangenigeukia na kuponywa.’#Isa 6:9-10
16Bahati gani mliyonayo ninyi. Mnaelewa mnachokiona kwa macho yenu. Na mnaelewa mnachosikia kwa masikio yenu. 17Ninaweza kuwathibitishia, manabii na watakatifu wengi walitaka kuona mnayoyaona. Lakini hawakuyaona. Walitaka kusikia mnayosikia sasa. Lakini hawakuyasikia.
Yesu Afafanua Simulizi Kuhusu Mbegu
(Mk 4:13-20; Lk 8:11-15)
18Hivyo sikilizeni maana ya simulizi hiyo kuhusu mkulima:
19Vipi kuhusu mbegu zilizoangukia njiani? Hizo zinafanana na watu wanaosikia mafundisho kuhusu ufalme wa Mungu lakini hawauelewi. Mwovu huja na kuyachukua yaliyopandwa katika mioyo yao.
20Na vipi kuhusu mbegu zilizoangukia kwenye udongo wenye mawe? Hizo zinafanana na watu wanaosikia mafundisho haraka na kwa furaha huyapokea. 21Lakini hawaruhusu mafundisho kutawala maisha yao. Huyatunza kwa muda mfupi. Mara tatizo au mateso yanapokuja kwa sababu ya mafundisho waliyoyapokea, wanaacha kuyafuata.
22Na vipi kuhusu mbegu zilizoanguka katikati ya miiba? Hizo zinafanana na watu wanaosikia mafundisho lakini huyaruhusu mahangaiko ya maisha na kutaka utajiri, hufanya mafundisho yasikue. Hivyo mafundisho hayazai mazao mazuri katika maisha yao.
23Lakini vipi kuhusu mbegu zilizoanguka kwenye udongo wenye rutuba? Hizo ni sawa na watu wanaosikia mafundisho na kuyaelewa. Hukua na kuzaa mazao mazuri, wakati mwingine mara mia, wakati mwingine mara sitini, na wakati mwingine mara thelathini zaidi.”
Simulizi Kuhusu Ngano na Magugu
24Kisha Yesu akatumia simulizi nyingine kuwafundisha. Yesu akasema, “Ufalme wa Mungu unafanana na mtu aliyepanda mbegu nzuri katika shamba lake. 25Usiku ule, kila mtu alipokuwa amelala, adui wa yule mtu akaja na kupanda magugu katikati ya ngano kisha akaondoka. 26Baadaye, ngano ikakua na vichwa vya nafaka vikaota juu ya mimea. Kisha mtumishi akayaona magugu. 27Watumwa wa mwenye shamba wakaja na akasema, ‘Bwana ulipanda mimea mizuri kwenye shamba lako. Magugu yametoka wapi?’
28Yule mtu akajibu, ‘Adui alipanda magugu.’
Wale watumwa wakauliza, ‘Je! unataka twende na kung'oa magugu?’
29Akajibu, ‘Hapana, kwa sababu mtakapokuwa mnang'oa magugu, mtaweza pia kung'oa ngano. 30Yaacheni magugu na ngano vikue pamoja mpaka wakati wa mavuno. Wakati wa mavuno nitawaambia wafanyakazi hivi: Kwanza, yakusanyeni magugu na kuyafunga pamoja ili myachome. Kisha kusanyeni ngano na kuileta ghalani mwangu.’”
Simulizi Nyingine ya Ufalme
(Mk 4:30-34; Lk 13:18-21)
31Kisha Yesu akawaambia watu simulizi nyingine: “Ufalme wa Mungu unafanana na mbegu ya mharadali ambayo mtu alipanda katika shamba lake. 32Ni mbegu ndogo sana kuliko mbegu zote. Lakini unapokua, ni kubwa kuliko mimea yote ya bustanini. Unakuwa mti mkubwa unaotosha ndege kuja na kutengeneza viota kwenye matawi yake.”
33Kisha Yesu akawaambia simulizi nyingine: “Ufalme wa Mungu unafanana na chachu ambayo mwanamke huichanganya katika bakuli kubwa la unga ili atengeneze mkate. Chachu hufanya kinyunya chote kiumuke.”
34Yesu alitumia simulizi akasema mambo yote haya kwa watu. Daima alitumia simulizi kuwafundisha. 35Hii ilikuwa kuweka wazi maana halisi kama manabii walivyosema:
“Nitazungumza kwa kutumia simulizi;
Nitayasema mambo ambayo yamekuwa siri
tangu ulimwengu ulipoumbwa.”#Zab 78:2
Yesu Afafanua Simulizi Kuhusu Magugu
36Kisha Yesu akawaacha watu na kuingia katika nyumba. Wafuasi wake wakamwendea na akasema, “Tufafanulie maana ya simulizi kuhusu magugu ndani ya shamba.”
37Akajibu, “Mtu aliyepanda mbegu nzuri katika shamba ni Mwana wa Adamu. 38Shamba ni ulimwengu. Mbegu nzuri ni watoto katika ufalme wa Mungu. Magugu ni watu wa Yule Mwovu. 39Na adui aliyepanda mbegu mbaya ni ibilisi. Mwisho wa nyakati ndiyo wakati wa mavuno. Wafanyakazi wanaokusanya ni malaika wa Mungu.
40Magugu hung'olewa na kuchomwa motoni. Itakuwa vivyo hivyo nyakati za mwisho. 41Mwana wa Adamu atawatuma malaika zake, nao watawatafuta watu wanaosababisha dhambi na wale wote watendao maovu. Malaika watawatoa watu hao katika ufalme wa Mungu. 42Watawatupia katika tanuru la moto. Huko watu watakuwa wakilia na kusaga meno kwa maumivu. 43Kisha wenye haki watang'aa kama jua. Watakuwa katika ufalme wa baba yao. Ninyi watu, mlio na masikio, sikilizeni!
Simulizi Kuhusu Hazina na Lulu
44Ufalme wa Mungu unafanana na hazina iliyofichwa shambani. Siku moja mtu alipoiona aliificha tena; na kwa sababu alikuwa na furaha sana alikwenda kuuza kila kitu alichonacho na kulinunua shamba.
45Pia, ufalme wa Mungu unafanana na mchuuzi anayetafuta lulu safi. 46Siku moja alipoipata, alikwenda na akauza kila kitu alichokuwa nacho ili kuinunua.
Simulizi Kuhusu Wavu wa Kuvulia Samaki
47Pia, ufalme wa Mungu unafanana na nyavu kubwa iliyowekwa katika ziwa. Nyavu ile ikavua aina nyingi tofauti ya samaki. 48Ikajaa, hivyo wavuvi wakaivuta mpaka pwani. Wakakaa chini na kutoa samaki wote wazuri na kuwaweka kwenye kikapu. Kisha wakawatupa samaki wabaya. 49Itakuwa hivyo wakati wa mwisho. Malaika watakuja na kuwatenganisha waovu na watakatifu. 50Watawatupa waovu katika tanuru la moto. Huko watu watalia na kusaga meno yao kwa sababu ya maumivu.”
51Kisha Yesu akawauliza wafuasi wake, “Mnaelewa mambo yote haya?”
Wakasema, “Ndiyo, tunaelewa.”
52Kisha Yesu akawaambia wafuasi wake, “Hivyo kila mwalimu wa sheria aliyejifunza kuhusu ufalme wa Mungu ana baadhi ya vitu vizuri vya kufundisha. Ni kama mmiliki wa nyumba, aliye na vitu vipya na vya zamani nyumbani mwake. Na huvitoa nje vipya na vya zamani.”
Yesu Aenda Kwenye Mji wa Kwao
(Mk 6:1-6; Lk 4:16-30)
53Yesu alipomaliza kufundisha kwa simulizi hizi, aliondoka pale. 54Alikwenda katika mji wa kwao. Aliwafundisha watu katika sinagogi lao, nao walishangaa. Walisema, “Mtu huyu alipata wapi hekima na nguvu hii ya kutenda miujiza? 55Je! yeye si mwana wa seremala tunayemfahamu? Je! jina la mamaye si Mariamu na wadogo zake ni Yakobo, Yusufu, Simoni na Yuda? 56Na dada zake bado wanaishi hapa katika mji huu? Anawezaje kutenda mambo haya?” 57Hivyo wakawa na mashaka kumpokea.
Lakini Yesu akawaambia, “Watu kila mahali huwaheshimu manabii, lakini katika mji wake au katika nyumba yake nabii hapati heshima yoyote.” 58Yesu hakufanya miujiza mingi huko, kwa sababu watu hawakumwamini.
S'ha seleccionat:
Mathayo 13: TKU
Subratllat
Comparteix
Copia
Vols que els teus subratllats es desin a tots els teus dispositius? Registra't o inicia sessió
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi
Toleo la Awali
© 2017 Bible League International