Mathayo 6

6
Yesu Afundisha Kuhusu Kutoa
1Mnapofanya jambo jema, kuweni waangalifu msilifanye mbele za watu wengine ili wawaone. Mtakapofanya hivyo hamtapata thawabu kutoka kwa Baba yenu wa mbinguni.
2Unapowapa maskini na wahitaji, usilipigie mbiu sana jambo hilo. Maana hivyo ndivyo wanavyofanya wanafiki kwenye makusanyiko.#6:2 makusanyiko Au “masinagogi”. Wao hupiga mbiu kabla ya kutoa ili watu wawaone, kwa kuwa hutaka kila mtu awasifu. Ukweli ni kuwa, hiyo ndiyo thawabu yote waliyokwishapata. 3Hivyo unapowapa maskini, mtu yeyote asijue unachofanya.#6:3 asijue unachofanya Kwa maana ya kawaida, “Mkono wako wa kushoto usijue kile ambacho mkono wako wa kushoto unafanya.” 4Kutoa kwako kunapaswa kufanyika sirini kwa kuwa Baba yako huona mambo yanayofanywa sirini, naye atakupa thawabu.
Yesu Afundisha Kuhusu Maombi
(Lk 11:2-4)
5Mnapoomba, msiwe kama wanafiki. Wanapenda kusimama kwenye masinagogi na kwenye pembe za mitaa na kuomba kwa kupaza sauti. Wanapenda kuonwa na watu. Ukweli ni kuwa hiyo ndiyo thawabu yote watakayopata. 6Lakini unapoomba, unapaswa kuingia katika chumba chako cha ndani na ufunge mlango. Kisha mwombe Baba yako aliye mahali pa siri. Yeye anayaona mambo yanayofanyika katika siri na hivyo atakupa thawabu.
7Na unapoomba usiwe kama watu wasiomjua Mungu. Wao kila wanapoomba wanarudia maneno yale yale, tena na tena, wakidhani kuwa wanapoyarudia maneno hayo mara nyingi watasikiwa na Mungu na kujibiwa maombi yao. 8Msiwe kama wao. Baba yenu anajua yale mnayohitaji kabla hamjamwomba. 9Hivyo, hivi ndivyo mnapaswa kuomba:
‘Baba yetu uliye mbinguni,
Jina lako lipewe utukufu.
10Ufalme wako uje.
Mapenzi yako yafanyike hapa dunia,
kama yanavyofanyika huko mbinguni.
11Utupe leo chakula tunachohitaji.
12Utusamehe dhambi zetu,
kama tunavyowasamehe wale wanaotukosea.
13Usiruhusu tukajaribiwa,
lakini utuokoe na Yule Mwovu.’#6:13 Nakala zingine za Kiyunani zimeongeza: “Kwa kuwa ufalme na nguvu na utukufu ni vyako milele na milele. Amina.”
14Mkiwasemehe wengine makosa waliyowatendea, Baba yenu wa mbinguni naye atawasamehe makosa yenu pia. 15Lakini msipowasamehe wengine, Baba Yenu wa mbinguni hatawasamehe ninyi.
Yesu Afundisha Kuhusu Kufunga
16Mnapofunga, msijionyeshe kuwa na huzuni kama wanafiki wanavyofanya. Hukunja nyuso zao kwa kuonesha kuwa wana huzuni ili watu wawaone kuwa wamefunga. Ukweli ni kuwa wamekwishapata thawabu yao yote. 17Hivyo unapofunga, nawa uso wako na ujiweke katika mwonekano mzuri, 18ili watu wasijue kuwa umefunga, isipokuwa Baba yako, aliye nawe hata sirini. Anaweza kuona yanayofanywa sirini, naye atakupa thawabu.
Huwezi Kuwatumikia Mabwana Wawili
(Lk 12:33-34; 11:34-36; 16:13)
19Msijiwekee hazina hapa duniani, mahali nondo na kutu#6:19 nondo na kutu Pia katika mstari wa 20. huiharibu. Na wezi wanaweza kuvunja nyumba yako na kuziiba. 20Badala yake jiwekeeni hazina mbinguni ambako haziwezi kuharibiwa na nondo wala kutu na ambako wezi hawawezi kuvunja na kuziiba. 21Kwa kuwa roho yako itakuwa mahali ilipo hazina yako.
22Jinsi unavyowaangalia watu wengine ndivyo inavyoonyesha jinsi wewe mwenyewe ulivyo ndani yako. Ukiwaangalia watu kwa nia njema utajawa na nuru ndani yako. 23Lakini ukiwaangalia watu kwa nia mbaya, utajawa na giza ndani yako. Na ikiwa yote yanayoonekana ndani yako ni giza peke yake, basi unalo giza baya zaidi!#6:22-23 Kwa maana ya kawaida, 22 Taa ya mwili ni jicho. Hivyo, jicho lako likiwa safi, mwili wako wote utakuwa na nuru tele. 23 Lakini jicho lako likiwa na uovu, mwili wako wote utakuwa na giza. Hivyo ikiwa nuru ndani yako ni giza, giza hilo ni linatisha.
24Hamwezi kuwatumikia mabwana wawili kwa wakati mmoja. Mtamchukia mmoja na kumpenda yule mwingine au mtakuwa waaminifu kwa mmoja na kumdharau yule mwingine. Hamwezi kumtumikia Mungu pamoja na pesa.#6:24 pesa Au “mamona”, neno la Kiaramu linalomaanisha “utajiri”.
Utangulizeni Kwanza Ufalme wa Mungu
(Lk 12:22-34)
25Kwa hiyo ninawaambia, msiyahangaikie mahitaji ya mwili; mtakula nini, mtakunywa nini au mtavaa nini. Uhai ni zaidi ya chakula na mavazi. 26Waangalieni ndege wa angani. Hawapandi, hawavuni wala kutunza chakula ghalani, lakini Baba yenu wa mbinguni huwalisha. Je! hamjui kuwa ninyi mna thamani zaidi ya ndege? 27Hamwezi kujiongezea muda wa kuishi kwa kujisumbua.
28Na kwa nini mna wasiwasi kuhusu mavazi? Yaangalieni maua ya kondeni. Yatazameni namna yanavyomea. Hayafanyi kazi wala kujitengenezea mavazi. 29Lakini ninawaambia kuwa hata Suleimani, mfalme mkuu na tajiri, hakuvikwa vizuri kama mojawapo ya maua haya. 30Ikiwa Mungu anayafanya majani yanayoota mashambani kuwa mazuri mnafikiri atawafanyia ninyi kitu gani? Hayo ni majani tu, siku moja yako hai na siku inayofuata hutupwa katika moto. Lakini Mungu anajali kiasi cha kuyafanya kuwa mazuri ya kupendeza. Muwe na hakika basi atawapa ninyi mavazi mnayohitaji. Imani yenu ni ndogo sana!
31Msijisumbue na kusema, ‘Tutakula nini?’ au ‘Tutakunywa nini?’ au ‘Tutavaa nini?’ 32Haya ndiyo mambo ambayo watu wasiomjua Mungu huyawazia daima. Msiwe na wasiwasi, kwa sababu Baba yenu wa mbinguni anajua kuwa mnayahitaji haya yote. 33Utafuteni kwanza ufalme wa Mungu na mambo yote ambayo Mungu anahesabu kuwa ni mema na yenye haki. Ndipo Mungu atakapowapa yote mnayohitaji. 34Msiisumbukie kesho. Kwa kuwa kesho itajisumbukia yenyewe. Kila siku ina mahangaiko yake ya kutosha.

S'ha seleccionat:

Mathayo 6: TKU

Subratllat

Comparteix

Copia

None

Vols que els teus subratllats es desin a tots els teus dispositius? Registra't o inicia sessió