Marko 4

4
Simulizi Kuhusu Mkulima Aliyepanda Mbegu
(Mt 13:1-9; Lk 8:4-8)
1Kwa mara nyingine Yesu akaanza kufundisha kando ya ziwa. Umati wa watu ukakusanyika kumzunguka, naye akapanda ndani ya mtumbwi ili akae na kufundisha huku mtumbwi ukielea. 2Yesu akawafundisha mambo mengi kwa simulizi zenye mafumbo. Katika mafundisho yake alisema:
3“Sikilizeni! Mkulima mmoja alitoka kwenda kupanda mbegu. 4Alipokuwa akitupa na kuzisambaza mbegu hizo nyingine ikaanguka katika njia, na ndege wakaja na kuila. 5Mbegu nyingine ikaanguka juu ya uwanja wenye miamba, mahali ambapo hapakuwa na udongo wa kutosha. Hiyo mbegu ilichanua haraka kwani udongo ule haukuwa na kina cha kutosha. 6Lakini jua lilipochomoza, ule mmea uliungua na kwa sababu haukuwa na mizizi ya kutosha ulinyauka. 7Mbegu nyingine ilianguka kwenye magugu yenye miiba, na miiba ile ilikua na hatimaye kuibana sana na hivyo haikuzaa chochote. 8Mbegu nyingine ilianguka kwenye udongo mzuri, nayo ikaota, ikakua na kuzaa matunda; ikazaa mara thelathini, sitini na hata mia zaidi.”
9Kisha akasema, “Kila mwenye masikio mazuri ayasikie haya.”
Kwa nini Yesu Alitumia Simulizi Kufundisha
(Mt 13:10-17; Lk 8:9-10)
10Yesu alipokuwa peke yake, wale waliomzunguka na wale kumi na wawili walimuuliza kuhusu mifano hiyo.
11Akawaambia, “Ni ninyi tu mliojaliwa kuzifahamu siri juu ya Ufalme wa Mungu. Lakini kwa wale walio nje nanyi mambo yote yatasemwa kwa simulizi zenye mafumbo, 12Ili kwamba,
‘japo watatazama
sana hawataona,
na kwamba japo watasikia
sana hawataelewa;
vinginevyo,
wangegeuka na kusamehewa!’”#Isa 6:9-10
Yesu Afafanua Simulizi Kuhusu Mbegu
(Mt 13:18-23; Lk 8:11-15)
13Akawaambia, “Hamuelewi mfano huu? Sasa je mtaelewaje mfano wowote nitakaowapa? 14Mkulima ni badala ya yule anayepanda lile neno la Mungu. 15Watu wengine ni kama ile mbegu zilizoanguka juu ya njia pale ambapo neno la Mungu limepandwa. Baada ya kulisikia lile neno la Mungu, ndipo Shetani huja haraka na kuyaondoa yale mafundisho ya Mungu yaliyopandwa ndani yao.
16Watu wengine ni kama mbegu iliyopandwa kwenye eneo lenye mawe mengi. Wanapolisikia neno wanalipokea haraka kwa furaha. 17Lakini wao wenyewe wanakuwa bado hawajaliruhusu lizame zaidi katika maisha yao. Shida au mateso yanapotokea kwa sababu ya lile neno, kwa haraka sana wanaiacha imani.
18Watu wengine ni kama mbegu iliyopandwa katika miiba. Hawa ndio wale wanaolisikia neno, 19lakini mahangaiko ya maisha haya ya sasa, kuvutiwa na mali, na tamaa mbalimbali zingine huja na kulibana sana lile neno, nalo haliwezi kuwa na matokeo mazuri.#4:19 haliwezi kuwa na matokeo mazuri Kwa maana ya kawaida, “inakuwa haina matunda”, kwa maana kwamba watu hawa hawafanyi yale mambo mazuri ambayo Mungu anataka watu wafanye.
20Wengine ni kama mbegu iliyopandwa katika udongo mzuri. Hawa ni wale wanaolisikia neno, na kulipokea na hivyo kuwa na matokeo mazuri; wengine kutoa thelathini, wengine sitini na wengine mia moja zaidi.”
Zingatieni Nuru
(Lk 8:16-18)
21Yesu akawaambia, “Unapoileta taa ndani#4:21 taa ndani Yesu anafananisha mafundisho yake kama taa iliyoletwa chumbani penye giza. je unaiweka chini ya bakuli ama uvungu wa kitanda? Au unaileta ndani na kuiweka juu ya kitako cha taa? 22Kwani kila kilichofichika kitafunuliwa, na kila kilicho cha siri kitatokea kweupe kwenye mwanga. 23Yeyote mwenye masikio mazuri ni bora asikie.” 24Kisha akawaambia, “Zingatieni kwa makini kile mnachokisikia. Kwani jinsi mnavyosikiliza kwa makini, ndivyo mtakavyoelewa na kuzidi kuelewa. 25Kwa kuwa kila aliye na uelewa kidogo ataongezewa zaidi. Lakini wale wasiosikiliza kwa makini watapoteza hata ule uelewa mdogo walio nao.”#4:25 Kwa kuwa … nao “Mtu anapoleta taa chumbani, haiweki chini ya kikapu au chini uvunguni mwa kitanda! Badala yake, anaiweka mahali pa juu chumbani. 24 Mzingatie kwa makini kile mnachokisikia. Jinsi mnavyosikiliza kwa makini, ndivyo mtakavyoelewa. Na Mungu atawawezesha muelewe zaidi. 25 Watu walio na uelewa kidogo watapokea zaidi, lakini wale ambao hawakusikiliza vizuri, hata ule uelewa mdogo waliyonao nao utaondolewa kwao. Watasahau kidogo walichoelewa.”
Yesu Atumia Simulizi Kuhusu Mbegu Inayokua
26Yesu akasema, “Hivi ndivyo Ufalme wa Mungu unavyofanana: Mtu mmoja alitoka kwenda kupanda mbegu zake katika udongo shambani. 27Usiku alienda kulala na asubuhi aliamka na zile mbegu zikiota na kukua; na hakujua jinsi gani hiyo ilifanyika. 28Ardhi yenyewe inatoa nafaka; kwanza hutoka shina, kisha kinafuata kichwa na mwishoni hutokea nafaka kamili katika kichwa. 29Nafaka ile inapokuwa imekomaa, basi mkulima huikata kwa fyekeo kwani wakati wa mavuno umekwishafika.”
Simulizi Nyingine ya Ufalme
(Mt 13:31-32,34-35; Lk 13:18-19)
30Yesu akasema, “Niufanananishe na kitu gani ufalme wa mbinguni? Au tutumie mfano gani kuuelezea? 31Ni kama mbegu ya haradali, ambayo ni mbegu ndogo sana kuliko zote inapopandwa ardhini. 32Lakini inapokuwa imepandwa, inakua na kuwa kubwa sana kuliko mimea yote ya bustanini, na pia hubeba matawi makubwa, kiasi kwamba ndege wa angani wanaweza kupumzika katika kivuli chake.”
33Kwa mifano mingi kama hii aliendelea kuwafundisha kila kitu kwa kuzingatia uwezo wao wa kuelewa. 34Yesu hakusema kitu kwao bila kutumia mfano. Lakini alipokuwa peke yake pamoja na wanafunzi wake, alifafanua kila kitu kwao.
Yesu Atuliza Dhoruba
(Mt 8:23-27; Lk 8:22-25)
35Siku ile ilipofika jioni aliwaambia, “Hebu tuvuke kwenda ng'ambo ya pili ya ziwa.” 36Kwa hiyo wakaliacha lile kundi. Wakamchukua pamoja nao alipokuwa amerudi katika mtumbwi. Wakati ule ule palikuwepo na mitumbwi mingi mingine ziwani. 37Dhoruba kubwa ikatokea na mawimbi yalikuwa yanakuja katika pembe zote za mtumbwi. Mtumbwi nao ulikaribia kujaa maji kabisa 38lakini Yesu alikuwa amelala nyuma ya mtumbwi akiegemea mto. Wakamwaamsha na kumwambia, “Mwalimu je wewe hujali kwamba tunazama?”
39Kisha akainuka, akaukemea upepo, na akaliamuru ziwa, “Nyamaza Kimya! Tulia!” Upepo ule ukatulia na ziwa nalo likatulia kabisa.
40Kisha akawaambia, “Kwa nini mnaogopa? Je! Bado hamna imani yoyote?”
41Lakini walikuwa na woga sana, na wakasemezana wao kwa wao, “Ni nani basi huyu ambaye hata upepo na ziwa vinamtii?”

S'ha seleccionat:

Marko 4: TKU

Subratllat

Comparteix

Copia

None

Vols que els teus subratllats es desin a tots els teus dispositius? Registra't o inicia sessió