Yohana MT. 4
4
1BASSI Bwana alipojua ya kuwa Mafarisayo wamesikia kwamba Yesu anafanya wanafunzi wengi kuliko Yohana, na kubatiza, 2(lakini Yesu mwenyewe hakuhatiza, hali wanafunzi wake), 3akaacha Yahudi akaenda zake Galilaya marra ya pili. 4Na alikuwa hana buddi kupita katikati ya Samaria. 5Bassi akafika mji wa Samaria, uitwao Sukar, karibu na lile shamba ambalo Yakobo alimpa Yusuf mwanawe. 6Na hapo palikuwa na kisima cha Yakobo. Bassi Yesu, kwa sababu amechoka kwa safari yake, akaketi vivi hivi kisimani. Ilikuwa yapata saa sita. 7Akaja mwanamke wa Kisamaria kuteka maji. Yesu akamwambia, Nipe maji ninywe. 8Maana wanafunzi wake wamekwenda mjini wanunue chakula. 9Bassi yule mwanamke wa Kisamaria akamwambia, Imekuwaje wewe Myahudi kutaka maji kwangu, nami ni mwanamke wa Kisamaria? kwa maana Wayahudi hawachangamani na Wasamaria. 10Yesu akajibu akamwambia, Kama ungaliijua karama ya Mungu, nae ni nani akuambiae, Nipe maji ninywe, ungalimwomba yeye, nae angalikupa maji yaliyo hayi. 11Yule mwanamke akamwambia, Bwana, huna kitu cha kutekea na kisima kinakwenda chini sana; bassi, umeyapata wapi haya maji yaliyo hayi? 12Je! wewe u mkubwa kuliko baba yetu Yakobo aliyetupa kisima hiki, nae mwenyewe akanywa maji yake, na wanawe pia, na nyama zake? 13Yesu akajibu, akamwambia, Killa anywae maji haya ataona kiu tena: 14walakini ye yote atakaekunywa maji yale nitakayompa mimi, hataona kiu milele, bali yale maji nitakayompa yatakuwa ndani yake chemchemi ya maji, yakibubujika hatta uzima wa milele. 15Yule mwanamke akamwambia, Bwana, nipe maji hayo, nisione kiu wala nisije huku kuteka. 16Yesu akamwambia, Enenda, kamwite mume wako uje nae hapa. 17Yule mwanamke akajibu akasema, Sina mume. Yesu akamwambia, Umesema vema, Sina mume, 18kwa maana umekuwa na waume watano, na yeye uliye nae sasa siye mume wako; hapo umesema kweli. 19Yule mwanamke akamwambia, Bwana, naona ya kuwa u nabii. 20Baba zetu waliabudu katika mlima huu, na ninyi husema kwamba Yerusalemi ni mahali patupasapo kuabudia. 21Yesu akamwambia, Ee mwanamke, uniamini, saa inakuja ambayo hamtamwabudu Baba katika mlima huu, wala katika Yerusalemi. 22Ninyi mnaabudu msichokijua; sisi tunaabudu tukijuacho: kwa kuwa wokofu watoka kwa Wayahudi. 23Lakini saa inakuja, na sasa ipo, ambayo wenye ibada khalisi watamwabudu Baba katika roho na kweli: kwa maana Baba awatafuta watu kama hao wamwabudu. 24Mungu ni roho, nao wamwabuduo imewapasa kumwabudu katika roho na kweli. 25Yule mwanamke akamwambia, Najua ya kuwa yuaja Masihi (aitwae Kristo). Atakapokuja yeye, atatufunulia yote. 26Yesu akamwambia, Mimi nisemae nawe, ndiye.
27Marra hiyo wakaja wanafunzi wake wakastaajabu kwa sababu alikuwa akisema na mwanamke; lakini hapana aliyesema, Unatafuta nini? au, Kwa nini unasema nae?
28Bassi yule mwanamke akauacha mtungi wake, akaenda zake mjini, akawaambia watu, 29Njoni, nitazame mtu aliyeniambia mambo yote niliyoyatenda. Je! haimkini huyu kuwa ndiye Kristo? 30Bassi wakatoka mjini wakamwendea.
31Huko nyuma wanafunzi wakamsihi wakisema, Rabbi, ule. 32Akawaambia, Mimi nina chakula msichokijua ninyi. 33Bassi wanafunzi wake wakasemezana, Je! mtu amemletea chakula? 34Yesu akawaambia, Chakula changu ndicho hiki, niyatende mapenzi yake aliyenipeleka nikaimalize kazi yake. 35Hamsemi ninyi, Imebaki miezi mine bado, ndipo yaja mavuno? Nami nawaambieni, Inueni macho yenu, mkayatazame mashamba, ya kuwa yamekwisha kuwa meupe tayari kwa mavuno. 36Avunae hupokea mshahara na kukusanya matunda kwa uzima wa milele, illi yeye apandae na yeye avunae wafurahi pamoja. 37Maana neno lile, Mmoja hupanda, mwingine akavuna, huwa kweli. 38Mimi naliwatuma myavune msiyoyataabikia; wengine walitaabika, nanyi mmeingia katika taabu yao.
39Na katika mji ule Wasamaria wengi wakaamini kwa sababu ya maneno ya yule mwananike, aliposhuhudu, kwamba, Aliniambia mambo yote niliyoyatenda.
40Bassi wale Wasamaria walipomwendea walimsihi akae kwao; akakaa huko siku mbili. 41Watu wengi zaidi wakamwamini kwa sababu ya neno lake. 42Wakamwambia yule mwanamke, Sasa tunaamini, wala si kwa sababu ya maneno yako; maana tumesikia wenyewe, tena twajua ya kuwa hakika yake huyu ni Mwokozi wa ulimwengu. 43Baada ya siku hizo mbili akaondoka huko, akaenda Galilaya. 44Kwa maana Yesu mwenyewe alishuhudu ya kwamba nabii hana heshima katika inchi yake mwenyewe. 45Bassi alipofika Galilaya Wagalilaya wakampokea, kwa kuwa wameona mambo yote aliyoyatenda Yerusalemi wakati wa siku kuu; maana hao nao waliendea siku kuu. 46Bassi akafika tena Kana ya Galilaya, hapo alipofanya maji kuwa divai. Na palikuwa na diwani mmoja, ana mwana hawezi Kapernaum. 47Huyu aliposikia ya kwamba Yesu amekuja kutoka Yahudi hatta Galilaya, akamwendea, akamsihi ashuke akamponye mwana wake; kwa maana alikuwa kufani. 48Bassi Yesu akamwambia, Msipoona ishara na maajabu hamtaamini kabisa. 49Yule diwani akamwambia, Bwana, shuka kabla hajafa mtoto wangu. 50Yesu akamwambia, Shika njia yako: mwana wako yu hayi. Mtu yule akaliamini lile neno aliloambiwa na Yesu, akashika njia. 51Hatta alipokuwa akishuka, watumishi wake wakamlaki, wakampasha khabari, wakisema ya kama, Mtoto wako yu hayi. 52Bassi akawauliza khabari ya saa alipoanza kuwa hajambo. Bassi wakamwamhia, Jana, saa saba, homa ilimwacha. 53Bassi baba yake akafahamu ya kuwa ni saa ileile aliyoambiwa na Yesu, Mwana wako yu hayi. Akaamini yeye na nyumba yake yote. 54Na hii ni isharaya pili aliyoifanya Yesu, alipotoka Yahudi kwenda Galilaya.
S'ha seleccionat:
Yohana MT. 4: SWZZB1921
Subratllat
Comparteix
Copia
Vols que els teus subratllats es desin a tots els teus dispositius? Registra't o inicia sessió
Swahili New Testament © Bible Society of Tanzania, 1921.