Yohana MT. 9

9
1HATTA alipokuwa akipita akamwona nitu, kipofu tangu kuzaliwa. 2Wanafunzi wake wakamwuliza, wakinena, Rabbi, ni nani aliyetenda dhambi, mtu huyu au wazazi wake, hatta akazaliwa kipofu? 3Yesu akajibu, Huyu hakutenda dhambi wala wazazi wake; bali kazi za Mungu zidhihirishwe kwake. 4Yanipasa kuzifanya kazi zake aliyenipeleka maadam ni mchana: usiku waja, asipoweza mtu kufanya kazi. 5Maadam nipo ulimwenguni, mimi ni nuru ya ulimwengu. 6Alipokwisha kusema haya, akatema mate chini, akafanya tope kwa yale mate, 7akampaka kipofu macho kwa lile tope, akamwambia, Enenda, kanawe katika birika ya Siloam (tafsiri yake, Aliyetumwa). Bassi akaenda, akanawa, akarudi, anaona. 8Bassi jirani zake, na wale waliomwona zamani kuwa ni kipofu, wakanena, Je! huyu siye yule aliyekuwa akiomba, ameketi? 9Wengine wakimena, Amefanana nae. 10Yeye mwenyewe alisema, Mimi ndiye. Bassi wakamwambia, Macho yako yalifumhuliwaje? 11Yeye akajibu, akanena, Mtu aitwae Yesu alifanya tope, akanipaka macho yangu, akaniambia, Enenda hatta birika ya Siloam, ukanawe; bassi nikaenda nikanawa, nikapata kuona. 12Wakamwambia, Yuko wapi mtu huyo? Akanena, Sijui.
13Wakampeleka yule aliyekuwa kipofu zamani kwa Mafarisayo. 14Na ilikuwa sabato hapo Yesu alipofanya tope na kumfumbua macho. 15Bassi Mafarisayo nao wakamwuliza tena jinsi alivyopata kuona. Akawaambia, Alitia tope juu ya macho yangu nikanawa, na sasa naona. 16Bassi baadhi ya Mafarisayo wakanena, Mtu huyu hakutoka kwa Mungu, kwa sababu haishiki sabato. Wengine wakanena, Awezaje mtu mwenye dhambi kufanya ishara kama hizo? 17Kukawa matangukano kati yao. Bassi wakamwambia yule kipofu marra ya pili, Wewe unasema nini katika khabari zake kwa kuwa alikufumbua macho? Akasema, Yu nabii. 18Bassi Wayahudi hawakusadiki khabari zake ya kuwa alikuwa kipofu akapata kuona, hatta wakawaita wazazi wake yule aliyepata kuona; wakawauliza, wakinena, 19Huyu ndiye mwana wenu msemae kwamba alizaliwa kipofu? Amepataje, bassi, kuona sasa? 20Wazazi wake wakawajibu, wakasema, Tunajua ya kuwa huyu ni mwana wetu, na ya kuwa alizaliwa kipofu; 21lakiui jinsi aonavyo sasa, hatujui, na ni nani aliyemfumbua macho, hatujui; yeye ni mtu mzima; mwulizeni yeye mwenyewe, atajisemea. 22Wazazi wake waliyasema haya kwa sababu waliwaogopa Wayahudi; kwa maana Wayahudi wamekwisha kuwafikana kwamba mtu akimwungama kuwa Kristo, ataharamishwa sunagogi. 23Ndio sababu wazazi wake walisema, Yeye ni mtu mzima, mwulizeni. 24Bassi marra ya pili wakamwita yule mtu aliyekuwa kipofu wakamwambia, Mpe Mungu utukufu. Sisi tunajua ya kuwa mtu huyu ni mwenye dhambi. 25Bassi yule mtu akajibu akasema, Kwamba yeye m mwenye dhambi, sijui. Najua neno moja, mimi nalikuwa kipofu, na sasa naona. 26Wakamwambia tena, Alikutenda nini? Alikufumbuaje macho? 27Akawajibu, Nimekwisha kuwaambieni, wala hamkusikia: Mbona mnataka kusikia marra ya pili? Ninyi nanyi mnataka kuwa wanafunzi wake? 28Bassi wakamshutumu, wakasema, Wewe u mwanafunzi wake mtu yule; sisi tu wanafunzi wa Musa. 29Sisi twajua ya kuwa Mungu alisema na Musa, bali huyo hatujui atokako. 30Yule mtu akajibu akawaambia, Neno hili ni la ajabu, kwamba ninyi hamjui atokako, nae alinifumbua macho. 31Twajua ya kuwa Mungu hawasikii wenye dhambi: bali mtu akiwa mcha Mungu, na kufanya mapenzi yake, huyo amsikia. 32Tangu awali haijasikiwa ya kuwa mtu ameyafumbua macho ya kipofu aliyezaliwa hali hii. 33Kama huyu asingalitoka kwa Mungu, asingeweza kutenda neno. 34Wakajibu, wakamwambia, Wewe ulizaliwa katika dhambi tupu, nawe unatufuudisha sisi? Wakamtoa nje.
35Yesu akasikia kwamba wamemtoa nje; akamwona, akasema, Wewe wamwamini Mwana wa Mungu? 36Nae akajibu, akasema, Ni nani, Bwana, nipate kumwamini? 37Yesu akamwambia, Umemwona, na yeye anaesema nawe ndiye. 38Akasema, Naamini, Bwana; akamsujudia. 39Yesu akasema, Mimi nimekuja ulimwenguni humu kwa hukumu, illi wasioona waone, nao wanaoona wawe vipofu. 40Baadhi ya Mafarisayo waliokuwa pamoja nae wakasikia haya, wakamwambia, Je! sisi nasi tu vipofu? 41Yesu akawaambia, Kama mngekuwa vipofu, msingekuwa na dhambi; lakini sasa mwasema Twaona; bassi dhambi yenu inakaa.

S'ha seleccionat:

Yohana MT. 9: SWZZB1921

Subratllat

Comparteix

Copia

None

Vols que els teus subratllats es desin a tots els teus dispositius? Registra't o inicia sessió