Luka MT. 24

24
1HATTA siku ya kwanza ya juma, ikianza kupambazuka, wakaenda kaburini wakiyaleta yale manukato waliyoyaweka tayari, na wengine pamoja nao. 2Wakalikuta lile jiwe limefingirishwa mbali ya kaburi. 3Wakaingia, wasiuone mwili wa Bwana Yesu. 4Ikawa wangali wakishangaa kwa haya, kumbe! watu wawili wakisimama karibu yao, wamevaa nguo za kumetameta. 5Nao wakiingiwa na khofu na kuinama kifudifudi hatta inchi, wakawaambia, Kwa nini mnamtafuta aliye hayi katika wafu? Hayupo hapa, bali amefufuka. 6Kumbukeni jinsi alivyosema nanyi alipokuwa hajatoka Galilaya, akinena, 7ya kwamba imempasa Mwana wa Adamu kutiwa katika mikono ya watu wenye dhambi, na kusulibiwa, na kufufuka siku ya tafu. 8Wakakumbuka maneno yake, 9wakarejea kutoka kaburi, wakawaarifu wale edashara na wale wengine wote pia mambo hayo yote. 10Na hao waliowaambia mitume mambo haya ni Mariamu Magdalene, na Yoanna, na Mariamu mama yake Yakobo na wengine waliokuwa pamoja nao. 11Maneno yao yakaonekana kuwa ni upuzi kwao, wala hawakuwasadiki. 12Lakini Petro akaondoka, akaenda mbio kaburini, akainama, akachungulia ndani, akaviona vile vitambaa vimewekwa peke yake, akarudi kwake, akistaajabu kwa yale yaliyotokea. 13Siku ileile wawili wao walikuwa wakienda hatta kijiji, jina lake Emmao, kilichokuwa mbali ya Yerusalemi yapata stadio sittini. 14Nao wakawa wakizumgumza haya yote yaliyotukia. 15Ikawa katika kuzumgumza kwao na kuulizana, Yesu mwenyewe akakaribia, akafuatana nao. 16Macho yao yakafumbwa, wasipate kumtambua. 17Akawaambia, Maneno gani haya mnayobishana katika kutembea kwenu? na tena nyuso zenu zimekunjamana. 18Akajibu mmoja wao, jina lake Kleopa, akamwambia, Je! wewe peke yako u mgeni katika Yerusalemi, usiyajue yaliyokuwa ndani yake siku hizi? 19Akawaambia, Mambo gani? Wakamwambia, Mambo ya Yesu Mnazareti, aliyekuwa mtu nabii mwenye nguvu kwa tendo na kwa neno mbele za Mungu na watu wote; 20na jinsi makuhani wakuu na wakubwa wetu walivyomtoa kwa hukumu ya kufa, wakamsulibisha; 21nasi twalitaraja ya kuwa yeye ndiye atakaekomboa Israeli. Hatta pamoja na haya yote, leo ni siku ya tatu tangu yalipokuwa haya. 22Kuna tena wanawake wengine wa kwetu waliotustusha, wakiamkia mapema kwenda kaburini: 23wasioukuta mwili wake, wakaja, wakasema ya kwamba wametokewa na malaika, waliowaambia yu hayi. 24Na wengine waliokuwa pamoja nasi wakaenda kaburini, wakaona vivyo hivyo kama wanawake walivyosema; illa yeye hawakumwona. 25Nae akawaambia, Enyi wapumbavu, na wenye mioyo mizito katika kuyaamini yote waliyoyasema manabii! 26Haikumpasa Kristo kupata mateso haya, ndipo aingie enzini mwake? 27Akaanza toka Musa na manabii, akawafasiria katika maandiko yote mambo yaliyomkhusu yeye. 28Wakakikaribia kijiji walikokuwa wakienda; nae akajifanya kama anataka kwenda mbele. 29Wakamshurutisha, wakisema, Kaa pamoja nasi, kwa maana kumekuchwa, na mchana unakwisha sasa. Akaingia kukaa nao. 30Ikawa, akiketi pamoja nao, akautwaa mkate, akaubariki, akaumega, akawagawia. 31Yakafumbuliwa macho yao, wakamtambua, akatoweka asionekane nao. 32Wakaambiana, Je! Mioyo yetu haikuwa ikiwaka ndani yetu, alipokuwa akisema nasi njiani, akitufunulia maandiko? 33Wakaondoka saa ileile, wakarudi Yerusalemi, wakawakuta wale edashara wamekusanyika, nao waliokuwa pamoja nao, 34wakisema, Hakika Bwana amefufuka, amemtokea Simon. 35Nao wakawahadithia yale ya njiani, na jinsi alivyotambulikana nao kwa kumega mkate.
36Walipokuwa wakisema hivyo, Yesu mwenyewe akasimama kati yao, akiwaambia, Amani kwenu. 37Wakafadhaika, wakaingiwa na khofu, wakidhani ya kuwa wanaona pepo. 38Akawaambia, Mbona mmefadhaika? na kwa nini mashaka yanatokea mioyoni mwenu. 39Tazameni mikono yangu, na miguu yangu, ya kuwa ni mimi mwenyewe. Nipapaseni, mkatazame; kwa maana pepo hana mwili na mifupa, kama mnionavyo mimi kuwa nayo. 40Na baada ya kusema haya akawaonyesha mikono yake na miguu yake. 41Bassi, wakiwa bado kuamini kwa furaha, wakitaajabu, akawaambia, Mna kitu cha kula hapa? 42Wakampa kipande cha samaki kilichookwa na asali kidogo. 43Akakitwaa, akala mbele yao. 44Akawaambia, Haya ndiyo maneno yangu niliyowaambieni, nilipokuwa kwenu, ya kuwa hayana buddi kutimizwa yote niliyoandikiwa katika torati ya Musa, na katika manabii, na katika zaburi. 45Ndipo akaamsha akili zao, wapate kuyatambua maandiko matakatifu. 46Akawaambia, Ndivyo ilivyoandikwa, na ndivyo ilivyompasa Kristo kuteswa, na kufufuka siku ya tatu; 47na mataifa yote wakhubiriwe kwa jina lake toba na ondoleo la dhambi, kuanzia Yerusalemi. 48Nanyi mashahidi wa mambo haya.
49Angalieni, bassi, naituma ahadi ya Baba yangu kwenu: lakini kaeni katika mji huu Yerusalemi, hatta mtakapovikwa nguvu zitokazo juu.
50Akawaongoza nje mpaka Bethania: akainua mikono yake, akawabariki. 51Ikawa katika kuwabariki, akajitenga nao, akachukuliwa juu mbinguni. 52Nao wakamsujudia, wakarudi Yerusalemi na furaha kuu: 53wakawa daima ndani ya hekalu, wakimsifu Mungu na kumhimidi. Amin.

S'ha seleccionat:

Luka MT. 24: SWZZB1921

Subratllat

Comparteix

Copia

None

Vols que els teus subratllats es desin a tots els teus dispositius? Registra't o inicia sessió