Mattayo MT. 4

4
1NDIPO Yesu alipopandishwa na Roho hatta jangwani, illi ajaribiwe na Shetani. 2Akafunga siku arubaini mchana na usiku, baadae akaona njaa. 3Mjaribu akamjia akasema, Ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu, amuru mawe haya yawe mikate. 4Akajibu akasema, Imeandikwa, Mtu hataishi kwa mkate tu, illa kwa killa neno litokalo katika kinywa cha Mungu. 5Kisha Shetani akamchukua hatta mji mtakatifu, akamweka juu ya mnara wa hekalu, akamwambia, 6Ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu, jitupe chini: kwa maana imeandikwa,
Atakuagizia malaika zake:
Mikononi mwao watakuchukua,
Usije ukajikwaa mguu wako katika jiwe.
7Yesu akamwambia. Tena imeandikwa, Usimjaribu Bwana Mungu wako. 8Tena Shetani akamchukua hatta mlima mrefu mno, akamwonyesha milki zote za ulimwengu, na fakhari yake, akamwambia, 9Hizi zote nitakupa, ukianguka kunisujudia. 10Ndipo Yesu akamwambia, Nenda zako, Shetani: kwa maana imeandikwa, Utamsujudia Bwana Mungu wako, nae peke yake utamwabudu. 11Kisha Shetani akamwacha; wakaja malaika wakamtumikia.
12Yesu aliposikia ya kwamba Yohana amefungwa, akaenda zake hatta Galilaya; 13akatoka Nazareti, akaenda, akakaa Kapernaum, ulioko pwani, mipakani mwa Zabulon na Nafthalim: 14illi litimie neno lililonenwa na Nabii Isaya, akisema,
15Inchi ya Zabulon na inchi ya Nafthalim,
Njia ya bahari ngʼambu ya Yordani,
Galilaya ya mataifa,
16Watu waliokaa gizani
Waliona mwanga mkuu,
Nao waliokaa katika inchi na kivuli cha mauti,
Mwanga umewazukia.
17Tokea wakati huo Yesu akaanza kukhubiri, na kusema, Tubuni, maana ufalme wa mbinguni umekaribia. 18Nae Yesu akitembea kando ya bahari ya Galilaya, akaona ndugu wawili, Simon aitwae Petro, na Andrea ndugu yake, wakitupa jarife baharini; maana walikuwa wavuvi. 19Akawaambia, Nifuateni, nami nitawafanya kuwa wavuvi wii watu. 20Marra wakaziacha nyavu, wakamfuata. 21Akaendelea mbele, akaona ndugu wengine wawili. Yakob wa Zebedayo, na Yohana ndugu yake, walikuwa katika chombo pamoja na Zebedayo baba yao, wakitengeneza nyavu zao; akawaita. 22Marra wakakiacha chombo na baba yao, wakamfuata.
23Yesu akazunguka katika Galilaya yote, akifundisha katika sunagogi zao, na kuikhubiri injili ya ufalme, na kuponya ugonjwa na udhaifu wa killi namna katika watu. 24Khabari zake zikaenea katika Sham yote; wakamletea watu waliokuwa hawawezi, walioshikwa mi maradhi mbali mbali na mateso, nao wenye pepo, na wenye kifafa, na wenye kupooza; akawaponya. 25Makutano mengi wakamfuata, wakitoka Galilaya, na Dekapoli, na Yerusalemi, na Yahudi, na ngʼambu ya Yordani.

S'ha seleccionat:

Mattayo MT. 4: SWZZB1921

Subratllat

Comparteix

Copia

None

Vols que els teus subratllats es desin a tots els teus dispositius? Registra't o inicia sessió