Mwanzo 12
12
Wito Wa Abramu
1 bwana akawa amemwambia Abramu, “Ondoka kutoka nchi yako, uache jamii yako na nyumba ya baba yako, uende hadi nchi nitakayokuonyesha.
2 “Mimi nitakufanya taifa kubwa
na nitakubariki,
Nitalikuza jina lako,
nawe utakuwa baraka.
3 Nitawabariki wale wanaokubariki,
na yeyote akulaaniye nitamlaani;
na kupitia kwako mataifa yote duniani
yatabarikiwa.”
4 Hivyo Abramu akaondoka kama bwana alivyokuwa amemwambia; naye Lutu akaondoka pamoja naye. Wakati Abramu alipoitwa aondoke Harani, alikuwa na miaka sabini na mitano. 5 Abramu akamchukua Sarai mkewe pamoja na Lutu mwana wa ndugu yake, mali zote walizokuwa nazo pamoja na watu aliokuwa amewapata huko Harani, wakasafiri mpaka nchi ya Kanaani, wakafika huko.
6 Abramu akasafiri katika nchi hiyo akafika huko Shekemu, mahali penye mti wa mwaloni ulioko More. Wakati huo Wakanaani walikuwa wanaishi katika nchi hiyo. 7 bwana akamtokea Abramu, akamwambia, “Nitawapa uzao wako nchi hii.” Hivyo hapa akamjengea madhabahu bwana aliyekuwa amemtokea.
8 Kutoka huko Abramu akasafiri kuelekea kwenye vilima mashariki ya Betheli, naye akapiga hema huko, Betheli ikiwa upande wa magharibi na Ai upande wa mashariki. Huko alimjengea bwana madhabahu na akaliitia jina la bwana. 9 Kisha Abramu akasafiri kuelekea upande wa Negebu.
Abramu Katika Nchi Ya Misri
10 Basi kulikuwako na njaa katika nchi, naye Abramu akashuka kwenda Misri kukaa huko kwa muda, kwa maana njaa ilikuwa kali. 11 Alipokuwa karibu kuingia Misri, akamwambia Sarai mkewe, “Ninajua ya kwamba wewe ni mwanamke mzuri wa sura. 12Wakati Wamisri watakapokuona, watasema, ‘Huyu ni mke wake.’ Ndipo wataniua, lakini wewe watakuacha hai. 13 Sema wewe ni dada yangu, ili nitendewe mema kwa ajili yako, na maisha yangu yatahifadhiwa kwa sababu yako.”
14Abramu alipoingia Misri, Wamisri wakamwona Sarai kuwa ni mwanamke mzuri sana wa sura. 15Maafisa wa Farao walipomwona, wakamsifia kwa Farao; ndipo Sarai akapelekwa kwa nyumba ya mfalme. 16 Kwa ajili ya Sarai, Farao akamtendea Abramu mema, naye Abramu akapata kondoo, ng’ombe, punda, ngamia na watumishi wa kiume na wa kike.
17 Lakini bwana akamwadhibu Farao na nyumba yake kwa maradhi ya kufisha kwa sababu ya kumchukua Sarai, mke wa Abramu. 18 Ndipo Farao akamwita Abramu, akamuuliza, “Umenifanyia nini? Kwa nini hukuniambia ni mke wako? 19 Kwa nini ulisema, ‘Yeye ni dada yangu,’ hata nikamchukua kuwa mke wangu? Sasa basi, mke wako huyu hapa. Mchukue uende zako!” 20Kisha Farao akawapa watu wake amri kuhusu Abramu, wakamsindikiza pamoja na mke wake na kila alichokuwa nacho.
S'ha seleccionat:
Mwanzo 12: NMM
Subratllat
Comparteix
Copia
Vols que els teus subratllats es desin a tots els teus dispositius? Registra't o inicia sessió
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018 by Biblica, Inc.
Used with permission.
All rights reserved worldwide.