Mwanzo 15
15
Agano la Mungu na Abramu
1 Baada ya jambo hili, neno la Bwana likamjia Abramu katika maono, akaambiwa:
“Usiogope, Abramu.
Mimi ni ngao yako,
na thawabu yako kubwa sana.”
2 Lakini Abramu akasema, “Ee Bwana Mwenyezi, utanipa nini na mimi sina mtoto, na atakayerithi nyumba yangu ni huyu Eliezeri Mdameski?” 3Abramu akasema, “Hukunipa watoto, hivyo mtumishi katika nyumba yangu ndiye atakuwa mrithi wangu.”
4 Ndipo neno la Bwana lilipomjia, likanena: “Mtu huyu hatakuwa mrithi wako, bali mwana atakayetoka katika viuno vyako ndiye atakayekurithi.” 5Akamtoa nje na kusema, “Tazama juu mbinguni na uhesabu nyota, kama hakika utaweza kuzihesabu.” Ndipo akamwambia, “Hivyo ndivyo uzao wako utakavyokuwa.”
6 Abramu akamwamini Bwana, naye kwake jambo hili likahesabiwa kuwa haki.
7Pia akamwambia, “Mimi ndimi Bwana, niliyekutoa Uru ya Wakaldayo nikupe nchi hii uimiliki.”
8 Lakini Abramu akasema, “Ee Bwana Mwenyezi, nitawezaje kujua kwamba nitaimiliki?”
9Ndipo Bwana akamwambia, “Niletee ndama jike, mbuzi, na kondoo dume, kila mmoja wa miaka mitatu, pamoja na hua na kinda la njiwa.”
10 Abramu akamletea hivi vyote, akampasua kila mnyama vipande viwili, akavipanga kila kimoja kuelekea mwenzake, lakini hata hivyo ndege hakuwapasua vipande viwili. 11Kisha ndege walao nyama wakatua juu ya mizoga, lakini Abramu akawafukuza.
12 Jua lilipokuwa linatua, Abramu akashikwa na usingizi mzito, na giza nene na la kutisha likaja juu yake. 13Kisha Bwana akamwambia, “Ujue hakika kwamba wazao wako watakuwa wageni katika nchi isiyo yao, nao watafanywa watumwa na kuteswa kwa miaka mia nne. 14Lakini nitaliadhibu taifa lile watakalolitumikia kama watumwa, na baadaye watatoka huko na mali nyingi. 15Wewe hata hivyo utaenda kwa baba zako kwa amani, na kuzikwa katika uzee mwema. 16Katika kizazi cha nne wazao wako watarudi hapa, kwa maana uovu wa Waamori bado haujafikia kipimo.”
17 Jua lilipokuwa limezama na giza limeingia, tanuru la moshi na mwali wa moto unaowaka vikatokea na kupita kati ya vile vipande vya nyama. 18Siku hiyo Bwana akafanya agano na Abramu, na kumwambia, “Nitawapa wazao wako nchi hii, kuanzia Kijito cha Misri#15:18 Kijito cha Misri ina maana Wadi-el-Arish kwenye mpaka wa kusini wa Yuda. hadi mto ule mkubwa, Frati: 19yaani nchi ya Wakeni, Wakenizi, Wakadmoni, 20Wahiti, Waperizi, Warefai, 21Waamori, Wakanaani, Wagirgashi na Wayebusi.”
Právě zvoleno:
Mwanzo 15: NEN
Zvýraznění
Sdílet
Porovnat
Kopírovat
Chceš mít své zvýrazněné verše uložené na všech zařízeních? Zaregistruj se nebo se přihlas
Holy Bible, Kiswahili Contemporary Version™ (Neno: Biblia Takatifu™) | Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. | Used with permission. All rights reserved worldwide.
Biblica® Cross Reference System | Copyright © 2025 by Biblica, Inc. | Used with permission. All rights reserved worldwide.