Λογότυπο YouVersion
Εικονίδιο αναζήτησης

Matendo Utangulizi

Utangulizi
Kitabu hiki ni cha pili katika vitabu viwili ambavyo Luka alimwandikia Theofilo. Kinajihusisha na huduma ya wafuasi wa Al-Masihi. Luka anaonesha hali ambayo kundi la waumini wa Isa wa kwanza lilikabiliwa nayo wakati wa kuenea kwake katika utawala wa Rumi. Anathibitisha kuwa kazi ambayo Isa alianzisha alipokuwa duniani, aliendelea kuifanya katika kundi lake la waumini kupitia kwa Roho wa Mungu. Katika kuenea kwa Jumuiya ya waumini wa Isa, mkazo mkubwa uliwekwa kwa mitume kuwezeshwa na Roho wa Mungu.
Petro ndiye anayeonekana sana wakati wa kuanzishwa kwa kundi la waumini huko Yerusalemu. Tunaona jinsi kituo cha Jumuiya ya waumini wa Isa kilihama hadi Antiokia ya Siria. Luka pia alionesha vile Paulo, ambaye alikuwa mtesi wa waumini wa Isa, hatimaye aliokoka na akawa kiongozi mkuu wa waumini wa Isa. Hivyo sehemu ya mwisho ya kitabu hiki imetoa nafasi kubwa kwa Paulo na utume wake. Kitabu kinaishia Paulo akiwa mfungwa anayehubiri Injili huko Rumi.
Mwandishi
Luka.
Kusudi
Kueleza utendaji wa Roho wa Mungu na wa mitume katika kuthibitisha Maandiko Matakatifu, na pia kutoa maelezo kuhusu kuanza kwa Jumuiya ya waumini wa Isa, na jinsi Mwenyezi Mungu alivyodhihirisha nafsi yake mwenyewe katika mwili wa Isa Al-Masihi kupitia kwa waumini wa Isa.
Mahali
Hapajulikani.
Tarehe
Mnamo 63–70 B.K.
Wahusika Wakuu
Petro, Paulo, Stefano, Filipo na Barnaba.
Wazo Kuu
Kueleza jinsi Injili ilivyoenezwa kutoka kwa Wayahudi na kuwafikia watu wa mataifa mengine, na vile Injili ya kufa na kufufuka kwake Isa ilivyo kiini cha msingi wa imani ya waumini wa Isa.
Mambo Muhimu
Kitabu hiki kinatoa kumbukumbu ya kuenea kwa waumini wa Isa, kushuka kwa Roho wa Mungu katika waumini wa Isa ili kuwatia mitume nguvu ya kuendeleza kazi ya Al-Masihi. Kinaelezea jinsi Injili ya Al-Masihi ilivyoenea katika utawala wa Rumi, kuanzia Yerusalemu hadi Rumi.
Yaliyomo
Waumini wa Isa wa kwanza (1:1–5:42)
Mateso na kuenea kwa Injili (6:1–9:31)
Matendo ya Petro (9:32–12:25)
Safari ya kwanza ya Paulo kueneza Injili (13:1–14:28)
Baraza la Yerusalemu na matokeo yake (15:1-35)
Safari ya pili ya Paulo kueneza Injili (15:36–18:22)
Safari ya tatu ya Paulo kueneza Injili (18:23–21:16)
Kukamatwa kwa Paulo na safari yake kwenda Rumi (21:17–28:31).

Επιλέχθηκαν προς το παρόν:

Matendo Utangulizi: NENO

Επισημάνσεις

Κοινοποίηση

Αντιγραφή

None

Θέλετε να αποθηκεύονται οι επισημάνσεις σας σε όλες τις συσκευές σας; Εγγραφείτε ή συνδεθείτε