Mwanzo 22
22
Kujua uthabiti wa Ibrahimu
1Baadaye Mungu akamjaribu Ibrahimu. Akamwambia, “Ibrahimu!”
Ibrahimu akamjibu, “Mimi hapa.”
2Kisha Mungu akamwambia, “Mchukue mwanao, mwana wako wa pekee umpendaye, Isaka, uende nchi ya Moria. Mtoe kama sadaka ya kuteketezwa juu ya mlima nitakaokuambia.”
3Ibrahimu akaamka asubuhi na mapema siku iliyofuata, akamtayarisha punda wake. Akawachukua watumishi wake wawili pamoja na Isaka mwanawe. Baada ya kuchanja kuni za kutosha kwa ajili ya hiyo sadaka ya kuteketezwa, akaondoka kuelekea mahali Mungu alipokuwa amemwambia. 4Siku ya tatu Ibrahimu akainua macho, akapaona mahali pale kwa mbali. 5Akawaambia watumishi wake, “Kaeni hapa pamoja na punda, wakati mimi na kijana tunaenda kule. Tutaabudu na kisha tutawarudia.”
6Ibrahimu akachukua kuni kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa, akamtwika Isaka mwanawe, naye mwenyewe akachukua moto na kisu. Walipokuwa wakienda pamoja, 7Isaka akamwambia Ibrahimu baba yake, “Baba yangu!”
Ibrahimu akaitika, “Mimi hapa, mwanangu.”
Isaka akasema, “Moto na kuni zipo. Je, yuko wapi mwana-kondoo kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa?”
8Ibrahimu akajibu, “Mwanangu, Mungu mwenyewe atajipatia mwana-kondoo kwa ajili ya hiyo sadaka ya kuteketezwa.” Nao hawa wawili wakaendelea mbele pamoja.
9Walipofika mahali pale alipokuwa ameambiwa na Mungu, Ibrahimu akajenga madhabahu hapo, akaziweka kuni juu yake. Akamfunga Isaka mwanawe na akamlaza kwenye madhabahu, juu ya zile kuni. 10Kisha akanyoosha mkono wake na akachukua kisu ili amchinje mwanawe. 11Lakini malaika wa Mwenyezi Mungu akamwita kutoka mbinguni, akamwambia, “Ibrahimu! Ibrahimu!”
Akajibu, “Mimi hapa.”
12Akamwambia, “Usimdhuru kijana, wala usimtendee jambo. Sasa ninajua kwamba unamcha Mungu, kwa sababu hukunizuilia mwanao, mwana wako wa pekee.”
13Ibrahimu akainua macho, akaona nyuma yake kondoo dume akiwa amenaswa pembe zake katika kichaka. Akaenda akamchukua huyo kondoo dume, akamtoa awe sadaka ya kuteketezwa badala ya mwanawe. 14Ibrahimu akapaita mahali pale Yehova-Yire.#22:14 maana yake Mwenyezi Mungu atapata Hadi leo inasemekana, “Katika mlima wa Mwenyezi Mungu itapatikana.”
15Basi malaika wa Mwenyezi Mungu akamwita Ibrahimu kutoka mbinguni mara ya pili, 16akasema, “Ninaapa kwa nafsi yangu, asema Mwenyezi Mungu, kwa sababu umefanya jambo hili na hukunizuilia mwanao, mwana wako wa pekee: 17Hakika nitakubariki, na nitauzidisha uzao wako kama nyota za angani na kama mchanga wa pwani. Wazao wako watamiliki miji ya adui zao, 18na kupitia uzao wako mataifa yote duniani yatabarikiwa, kwa sababu umenitii.”
19Ndipo Ibrahimu akawarudia watumishi wake, wakaondoka wote, wakaenda hadi Beer-Sheba. Naye Ibrahimu akaishi huko Beer-Sheba.
Wana wa Nahori
20Baada ya muda, Ibrahimu akaambiwa, “Milka pia amepata watoto; amemzalia ndugu yako Nahori wana:
21Usi mzaliwa wake wa kwanza, Buzi nduguye,
Kemueli (baba wa Aramu),
22Kesedi, Hazo, Pildashi, Yidlafu na Bethueli.”
23Bethueli akamzaa Rebeka.
Milka alimzalia Nahori nduguye Ibrahimu hao wana wanane.
24Suria wake Nahori aliyeitwa Reuma pia alizaa wana:
Teba, Gahamu, Tahashi na Maaka.
Επιλέχθηκαν προς το παρόν:
Mwanzo 22: NENO
Επισημάνσεις
Κοινοποίηση
Αντιγραφή
Θέλετε να αποθηκεύονται οι επισημάνσεις σας σε όλες τις συσκευές σας; Εγγραφείτε ή συνδεθείτε
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.