Λογότυπο YouVersion
Εικονίδιο αναζήτησης

Mwanzo 27

27
Isaka ambariki Yakobo
1Isaka alipokuwa mzee na macho yake yakapofuka kwa kukosa nguvu, akamwita Esau mwanawe mkubwa, akamwambia, “Mwanangu.”
Akajibu, “Mimi hapa.”
2Isaka akasema, “Mimi sasa ni mzee na sijui siku ya kufa kwangu. 3Sasa basi chukua silaha zako, podo na upinde, uende nyikani, ukaniwindie mawindo. 4Uniandalie chakula kitamu nikipendacho uniletee nile, ili nikubariki kabla sijafa.”
5Rebeka alikuwa akisikiliza Isaka akizungumza na mwanawe Esau. Basi Esau alipoenda nyikani kuwinda mawindo ayalete, 6Rebeka akamwambia Yakobo mwanawe, “Tazama, nimemsikia baba yako akimwambia ndugu yako Esau, 7‘Niletee mawindo, kisha ukaniandalie chakula kitamu nile, ili nikubariki mbele za Mwenyezi Mungu kabla sijafa.’ 8Sasa mwanangu, nisikilize kwa makini na ufanye yale ninayokuambia: 9Nenda sasa katika kundi ukaniletee wana-mbuzi wawili wazuri, ili nimwandalie baba yako chakula kitamu kile anachokipenda. 10Kisha umpelekee baba yako ale, ili akubariki kabla hajafa.”
11Yakobo akamwambia Rebeka mama yake, “Lakini ndugu yangu Esau ana nywele mwilini, nami nina ngozi nyororo. 12Itakuwaje baba yangu akinigusa? Ataona kama ninamfanyia ujanja, nami nijiletee laana badala ya baraka.”
13Mama yake akamwambia, “Mwanangu, laana na iwe juu yangu. Fanya tu ninalokuambia: nenda ukaniletee hao wana-mbuzi.”
14Kwa hiyo alienda akawaleta, akampa mama yake, naye Rebeka akaandaa chakula kitamu, kile alichokipenda baba yake. 15Kisha Rebeka akachukua nguo nzuri za Esau mwanawe wa kwanza, alizokuwa nazo nyumbani, akamvika Yakobo mwanawe mdogo. 16Pia akamfunika mikononi na sehemu laini ya shingo kwa ngozi za mbuzi. 17Hatimaye akampa Yakobo hicho chakula kitamu pamoja na mkate aliouoka.
18Yakobo akaenda kwa baba yake, akasema, “Baba yangu.”
Akajibu, “Naam, mwanangu. Wewe ni nani?”
19Yakobo akamwambia baba yake, “Mimi ni Esau mzaliwa wako wa kwanza. Nimefanya kama ulivyoniambia. Tafadhali uketi, ule sehemu ya mawindo yangu ili unibariki.”
20Isaka akamuuliza mwanawe, “Umepataje mawindo haraka hivi, mwanangu?”
Akajibu, “Mwenyezi Mungu, Mungu wako, amenifanikisha.”
21Kisha Isaka akamwambia Yakobo, “Mwanangu, tafadhali sogea karibu nami ili nikupapase, nione kama hakika ndiwe Esau mwanangu, au la.”
22Yakobo akasogea karibu na baba yake Isaka, ambaye alimpapasa na kusema, “Sauti ni ya Yakobo, bali mikono ni ya Esau.” 23Hakumtambua, kwa sababu mikono yake ilikuwa na nywele kama ya ndugu yake Esau, kwa hiyo akambariki. 24Akamuuliza, “Kweli wewe ni mwanangu Esau?”
Akajibu, “Ni mimi.”
25Kisha Isaka akasema, “Mwanangu, niletee sehemu ya mawindo yako nile, ili nikubariki.”
Yakobo akamletea, naye akala; kisha akamletea na divai akanywa. 26Ndipo Isaka baba yake akamwambia, “Njoo hapa, mwanangu, unibusu.”
27Kwa hiyo akamwendea akambusu. Isaka aliposikia harufu ya nguo zake, akambariki, akasema,
“Aha, harufu ya mwanangu
ni kama harufu ya shamba
ambalo Mwenyezi Mungu amelibariki.
28Mungu na akupe umande wa mbinguni
na utajiri wa duniani:
wingi wa nafaka na divai mpya.
29Mataifa yakutumikie,
na mataifa yakusujudie.
Uwe bwana juu ya ndugu zako,
na wana wa mama yako wakusujudie.
Walaaniwe wale wanaokulaani,
na wabarikiwe wale wanaokubariki.”
30Baada ya Isaka kumbariki Yakobo, na punde tu alipoondoka kwa baba yake, ndugu yake Esau akaingia kutoka mawindoni. 31Naye pia akaandaa chakula kitamu, akamletea baba yake. Kisha akamwambia, “Baba yangu, keti ule sehemu ya mawindo yangu, ili upate kunibariki.”
32Isaka baba yake akamuuliza, “Wewe ni nani?”
Akamjibu, “Mimi ni mwanao, mzaliwa wako wa kwanza, Esau.”
33Isaka akatetemeka kwa nguvu sana, akasema, “Alikuwa nani basi, ambaye aliwinda mawindo akaniletea? Nilikula kabla tu hujaja na nikambariki, naye hakika atabarikiwa!”
34Esau aliposikia maneno haya ya baba yake, akalia kwa sauti kubwa na ya uchungu, na kumwambia baba yake, “Nibariki! Nibariki mimi pia, baba yangu!”
35Lakini akamjibu, “Ndugu yako amekuja kwa udanganyifu, akachukua baraka yako.”
36Esau akasema, “Si ndiyo sababu anaitwa Yakobo? Amenidanganya mara hizi mbili: Alichukua haki yangu ya kuzaliwa na sasa amechukua baraka yangu!” Kisha akauliza, “Hukubakiza hata baraka moja kwa ajili yangu?”
37Isaka akamjibu Esau, “Nimemfanya yeye kuwa bwana juu yako; pia nimewafanya ndugu zako wote kuwa watumishi wake, na nimemtegemeza kwa nafaka na divai mpya. Sasa nitaweza kukufanyia nini, mwanangu?”
38Esau akamwambia baba yake, “Je, baba yangu una baraka moja tu? Unibariki mimi pia, baba yangu!” Kisha Esau akalia kwa sauti kubwa.
39Baba yake Isaka akamjibu,
“Makao yako yatakuwa
mbali na utajiri wa dunia,
mbali na umande wa mbinguni.
40Utaishi kwa upanga,
nawe utamtumikia ndugu yako.
Lakini utakapokuwa umejikomboa,
utatupa nira yake
kutoka shingoni mwako.”
41Esau akawa na kinyongo dhidi ya Yakobo kwa ajili ya baraka ambazo baba yake alikuwa amembariki. Akasema moyoni mwake, “Siku za kuomboleza kwa ajili ya baba yangu zimekaribia; ndipo nitamuua ndugu yangu Yakobo.”
42Rebeka alipoambiwa yale Esau mwanawe mkubwa aliyoyasema, akamtumania Yakobo mwanawe mdogo, akamwambia, “Ndugu yako Esau anajifariji kwa wazo la kukuua. 43Sasa basi, mwanangu, fanya nisemalo: Kimbilia haraka kwa Labani ndugu yangu kule Harani. 44Ukae naye kwa muda hadi ghadhabu ya ndugu yako itulie. 45Ndugu yako atakapokuwa hana hasira nawe tena na amesahau uliyomtendea, nitakupelekea ujumbe urudi. Kwa nini niwapoteze nyote wawili siku moja?”
46Kisha Rebeka akamwambia Isaka, “Nimechukia maisha kwa sababu ya hawa wanawake Wahiti. Ikiwa Yakobo ataoa mke miongoni mwa wanawake wa nchi hii, wanawake Wahiti kama hawa, sitaona haja ya kuendelea kuishi.”

Επιλέχθηκαν προς το παρόν:

Mwanzo 27: NENO

Επισημάνσεις

Κοινοποίηση

Αντιγραφή

None

Θέλετε να αποθηκεύονται οι επισημάνσεις σας σε όλες τις συσκευές σας; Εγγραφείτε ή συνδεθείτε