Λογότυπο YouVersion
Εικονίδιο αναζήτησης

Mwanzo 29

29
Yakobo awasili Padan-Aramu
1Kisha Yakobo akaendelea na safari yake, na akafika nchi ya watu wa mashariki. 2Huko akaona kisima katika shamba, pamoja na makundi matatu ya kondoo yamelala karibu na kisima hicho, kwa sababu walikuwa wakinyweshwa kutoka kisima hicho. Jiwe lililokuwa juu ya mdomo wa kisima lilikuwa kubwa. 3Kondoo walipokusanyika hapo, wachungaji walilivingirisha jiwe hilo kutoka mdomo wa kisima. Kisha walilirudisha jiwe mahali pake juu ya mdomo wa kisima.
4Yakobo aliwauliza wachungaji, “Ndugu zangu, ninyi mmetoka wapi?”
Wakamjibu, “Tumetoka Harani.”
5Akawauliza, “Je, mnamfahamu Labani, mjukuu wa Nahori?”
Wakamjibu, “Ndiyo, tunamfahamu.”
6Kisha Yakobo akawauliza, “Je, yeye ni mzima?”
Wakasema, “Ndiyo, ni mzima; na hapa yuaja Raheli binti yake akiwa na kondoo.”
7Akawaambia, “Tazama, jua bado liko juu, si wakati wa kukusanya mifugo. Nywesheni kondoo na mwarudishe malishoni.”
8Wakamjibu, “Haiwezekani, hadi kondoo wote wakusanyike, nalo jiwe livingirishwe kutoka mdomo wa kisima. Ndipo tutawanywesha kondoo.”
9Alipokuwa akizungumza nao, Raheli akaja na kondoo wa baba yake, kwa maana alikuwa mchunga kondoo. 10Yakobo alipomwona Raheli binti Labani, ndugu wa mama yake, pamoja na kondoo wa Labani, alienda na kulivingirisha jiwe kutoka mdomo wa kisima na kuwanywesha kondoo wa mjomba wake. 11Kisha Yakobo akambusu Raheli, na akaanza kulia kwa sauti. 12Yakobo alikuwa amemwambia Raheli kuwa yeye alikuwa jamaa ya baba yake, na kwamba ni mwana wa Rebeka. Basi Raheli alikimbia na kumweleza baba yake.
13Mara Labani aliposikia habari kuhusu Yakobo, mwana wa ndugu yake, aliharakisha kwenda kumlaki. Akamkumbatia na kumbusu, halafu akamleta nyumbani mwake, naye Yakobo akamwambia mambo hayo yote. 14Ndipo Labani akamwambia, “Wewe ni mwili wangu na damu yangu mwenyewe.”
Yakobo awaoa Lea na Raheli
Baada ya Yakobo kukaa kwa Labani mwezi mzima, 15Labani akamwambia, “Kwa vile wewe ni jamaa yangu, ndiyo sababu unifanyie kazi bila ujira? Niambie ujira wako utakuwa nini.”
16Labani alikuwa na binti wawili; binti mkubwa aliitwa Lea, naye binti mdogo aliitwa Raheli. 17Lea alikuwa na macho dhaifu, lakini Raheli alikuwa na umbo la kupendeza na mzuri wa sura. 18Yakobo akampenda Raheli; akamwambia Labani, “Nitakutumikia kwa miaka saba kwa ajili ya kumpata Raheli binti yako mdogo.”
19Labani akasema, “Ni bora zaidi nikupe Raheli kuliko kumpa mtu mwingine yeyote. Kaa pamoja na mimi hapa.” 20Kwa hiyo Yakobo akatumika miaka saba ili kumpata Raheli, lakini ilionekana kwake kama siku chache tu kwa sababu ya upendo wake kwa Raheli.
21Ndipo Yakobo akamwambia Labani, “Nipe mke wangu. Muda wangu umekamilika, nami nataka niingie kwake.”
22Basi Labani akaalika watu wote wa mahali pale na akafanya karamu.
23Lakini ilipofika jioni, akamchukua Lea binti yake, akampa Yakobo, naye Yakobo akakutana naye kimwili. 24Naye Labani akamtoa Zilpa mjakazi wake kuwa mtumishi wa Lea, binti yake.
25Kesho yake asubuhi, Yakobo akagundua kuwa amepewa Lea! Basi Yakobo akamwambia Labani, “Ni jambo gani hili ulilonitendea? Nilikutumikia kwa ajili ya Raheli, sivyo? Kwa nini umenidanganya?”
26Labani akajibu, “Si desturi yetu kumwoza binti mdogo kabla ya kumwoza binti mkubwa. 27Maliza juma la arusi ya binti huyu, kisha pia nitakupa huyu binti mdogo, kwa kutumika miaka mingine saba.”
28Naye Yakobo akafanya hivyo. Akamaliza juma na Lea, kisha Labani akampa Raheli binti yake kuwa mke wake. 29Labani akamtoa Bilha mjakazi wake kwa Raheli ili kuwa mtumishi wake. 30Pia Yakobo akakutana na Raheli kimwili, naye akampenda Raheli kuliko Lea. Yakobo akamtumikia Labani kwa miaka mingine saba.
Wana wa Yakobo
31Mwenyezi Mungu alipoona kwamba Lea hapendwi, akamwezesha kupata watoto, lakini Raheli alikuwa tasa. 32Lea akapata mimba, akazaa mwana. Akamwita jina Reubeni#29:32 maana yake Ona mwana, kwa maana alisema, “Ni kwa sababu Mwenyezi Mungu ameona huzuni yangu. Hakika mume wangu sasa atanipenda.”
33Akapata tena mimba, naye alipozaa mwana akasema, “Kwa sababu Mwenyezi Mungu alisikia kwamba sipendwi, amenipa tena huyu mwana.” Kwa hiyo akamwita jina Simeoni#29:33 maana yake Anasikia.
34Akapata tena mimba, naye alipozaa mwana akasema, “Sasa mume wangu ataambatana na mimi, kwa sababu nimemzalia wana watatu.” Kwa hiyo akamwita jina Lawi#29:34 maana yake Nimeunganishwa.
35Akapata tena mimba, naye alipozaa mwana akasema, “Wakati huu nitamsifu Mwenyezi Mungu.” Kwa hiyo akamwita jina Yuda#29:35 maana yake Sifa. Kisha akaacha kuzaa watoto.

Επιλέχθηκαν προς το παρόν:

Mwanzo 29: NENO

Επισημάνσεις

Κοινοποίηση

Αντιγραφή

None

Θέλετε να αποθηκεύονται οι επισημάνσεις σας σε όλες τις συσκευές σας; Εγγραφείτε ή συνδεθείτε