Λογότυπο YouVersion
Εικονίδιο αναζήτησης

Mwanzo 4

4
Kaini na Habili
1Adamu akakutana kimwili na mkewe Hawa, naye akapata mimba, akamzaa Kaini. Hawa akasema, “Kwa msaada wa Mwenyezi Mungu nimemzaa mtoto wa kiume.” 2Baadaye akamzaa Habili ndugu yake.
Basi Habili akawa mfugaji, na Kaini akawa mkulima. 3Baada ya muda, Kaini akaleta baadhi ya mazao ya shamba ikiwa sadaka kwa Mwenyezi Mungu. 4Lakini Habili akaleta fungu nono kutoka baadhi ya wazaliwa wa kwanza wa mifugo yake. Mwenyezi Mungu akamkubali Habili pamoja na sadaka yake, 5lakini Mungu hakumkubali Kaini pamoja na sadaka yake. Kwa hiyo Kaini akakasirika sana, uso wake ukawa na huzuni.
6Kisha Mwenyezi Mungu akamwambia Kaini, “Kwa nini umekasirika? Kwa nini uso wako una huzuni? 7Ukifanya lililo sawa, je, hutakubalika? Lakini usipofanya lililo sawa, dhambi inakuvizia mlangoni mwako, ikikutamani wewe, lakini inakupasa uishinde.”
8Basi Kaini akamwambia ndugu yake Habili, “Twende shambani.” Walipokuwa shambani, Kaini akamshambulia Habili ndugu yake, akamuua.
9Kisha Mwenyezi Mungu akamuuliza Kaini, “Ndugu yako Habili yuko wapi?”
Akamjibu, “Sijui. Je, mimi ni mlinzi wa ndugu yangu?”
10Mwenyezi Mungu akasema, “Umefanya nini? Sikiliza! Damu ya ndugu yako inanililia mimi kutoka ardhini. 11Sasa umelaaniwa na umehamishwa kutoka ardhi, ambayo imefungua kinywa chake na kupokea damu ya ndugu yako kutoka mkononi mwako. 12Utakapoilima ardhi, haitakupa tena mazao yake. Utakuwa mtu wa kutangatanga duniani bila utulivu.”
13Kaini akamwambia Mwenyezi Mungu, “Adhabu yangu ni zaidi ya ninavyoweza kustahimili. 14Leo unanifukuza kutoka nchi, nami nitafichwa mbali na uwepo wako. Nitakuwa mtu wa kutangatanga duniani bila utulivu, na yeyote anionaye ataniua.”
15Lakini Mwenyezi Mungu akamwambia, “La, sivyo! Ikiwa mtu yeyote atamuua Kaini, atalipizwa kisasi mara saba.” Kisha Mwenyezi Mungu akamwekea Kaini alama ili yeyote angemwona asimuue. 16Kwa hiyo Kaini akaondoka mbele za Mwenyezi Mungu, akaenda kuishi katika nchi ya Nodi, mashariki mwa Edeni.
17Kaini akakutana kimwili na mkewe, naye akapata mimba na akamzaa Idrisi. Wakati huo Kaini alikuwa anajenga mji, akauita Idrisi, jina la mtoto wake. 18Idrisi akamzaa Iradi; Iradi akamzaa Mehuyaeli; Mehuyaeli akamzaa Methushaeli; naye Methushaeli akamzaa Lameki.
19Lameki alioa wanawake wawili: mmoja aliitwa Ada, na mwingine Sila. 20Ada akamzaa Yabali; huyu akawa baba wa wale wanaoishi katika mahema na kufuga wanyama. 21Kaka yake aliitwa Yubali, aliyekuwa baba wa wote wapigao zeze na filimbi. 22Pia Sila alikuwa na mtoto wa kiume aliyeitwa Tubali-Kaini, ambaye alifua vifaa vya aina mbalimbali vya shaba na chuma. Naama alikuwa dada wa Tubali-Kaini.
23Lameki akawaambia wake zake,
“Ada na Sila, nisikilizeni mimi;
wake wa Lameki sikieni maneno yangu.
Nimemuua mtu kwa kunijeruhi,
kijana mdogo kwa kuniumiza.
24Kama Kaini atalipizwa kisasi mara saba,
basi Lameki itakuwa mara sabini na saba.”
25Adamu akakutana kimwili na mke wake tena, akamzaa mwana, akamwita jina Sethi, akisema, “Mungu amenijalia mwana mwingine badala ya Habili, kwa kuwa Kaini alimuua.” 26Naye Sethi akamzaa mwana, akamwita jina Enoshi.
Wakati huo watu wakaanza kuliitia jina la Mwenyezi Mungu.

Επιλέχθηκαν προς το παρόν:

Mwanzo 4: NENO

Επισημάνσεις

Κοινοποίηση

Αντιγραφή

None

Θέλετε να αποθηκεύονται οι επισημάνσεις σας σε όλες τις συσκευές σας; Εγγραφείτε ή συνδεθείτε