Mathayo 12

12
Yesu ni Bwana Juu ya Siku ya Sabato
(Mk 2:23-28; Lk 6:1-5)
1Katika wakati huo huo, Yesu alikuwa anasafiri akipita katika mashamba ya nafaka siku ya Sabato. Wafuasi wake walikuwa pamoja naye, na walikuwa na njaa. Hivyo walianza kuchuma nafaka na kula. 2Mafarisayo walioliona hili, wakamwambia Yesu, “Tazama! Wafuasi wako wanafanya kitu ambacho ni kinyume na sheria yetu kufanya katika siku ya Sabato.”
3Yesu akawaambia, “Mmekwisha soma alichofanya Daudi wakati yeye na wale waliokuwa pamoja naye walipokuwa na njaa. 4Daudi aliingia katika nyumba ya Mungu. Yeye na wale waliokuwa pamoja naye walikula mkate uliotolewa kwa Mungu. Ilikuwa kinyume cha sheria kwa Daudi au wale waliokuwa pamoja naye kula mkate huo. Makuhani pekee ndio walioruhusiwa kuula. 5Na mmekwisha soma katika Sheria ya Musa kuwa katika kila Sabato makuhani kwenye Hekalu wanavunja Sheria kwa kufanya kazi Siku ya Sabato. Lakini hawakosei kwa kufanya hivyo. 6Ninawaambia kuwa kuna kitu hapa ambacho ni kikuu kuliko Hekalu. 7Maandiko yanasema, ‘Sihitaji dhabihu ya wanyama; Ninataka ninyi muoneshe wema kwa watu.’#Hos 6:6 Hakika hamjui hilo linamaanisha nini. Iwapo mngelielewa, msingewahukumu wale ambao hawajafanya chochote kibaya.
8Mwana wa Adamu ni Bwana juu ya siku ya Sabato.”
Yesu Amponya Mtu Siku ya Sabato
(Mk 3:1-6; Lk 6:6-11)
9Kutoka hapo Yesu alikwenda katika sinagogi lao. 10Ndani ya sinagogi alikuwemo mtu aliyepooza mkono. Baadhi ya Mafarisayo waliokuwa pale walikuwa wanatafuta sababu ya kumshitaki Yesu kwa kutenda kitu kibaya, hivyo walimuuliza, “Je! ni halali kuponya siku ya Sabato?”
11Yesu akajibu, “Ikiwa mmoja wenu ana kondoo na akatumbukia shimoni siku ya Sabato, utamsaidia kumtoa yule kondoo katika shimo. 12Hakika mtu ni bora kuliko kondoo. Hivyo ni sawa kutenda wema siku ya Sabato.”
13Kisha Yesu akamwambia mtu mwenye mkono uliopooza, “Unyooshe mkono wako.” Mtu yule akaunyoosha mkono wake, na ukawa mzima tena, kama mkono mwingine. 14Lakini Mafarisayo waliondoka na wakaweka mipango ya kumuua Yesu.
Yesu ni Mtumishi Aliyechaguliwa na Mungu
15Yesu alitambua kuwa Mafarisayo walikuwa wanapanga kumuua. Hivyo aliondoka mahali pale na watu wengi walimfuata. Akawaponya wote waliokuwa wagonjwa, 16lakini aliwaonya wasiwaambie wengine yeye alikuwa nani. 17Hii ilikuwa ni kuthibitisha kile ambacho nabii Isaya alisema alipozungumza kwa niaba ya Mungu:
18“Hapa ni mtumishi wangu,
niliyemchagua.
Ndiye ninayempenda,
na ninapendezwa naye.
Nitamjaza Roho yangu,
naye ataleta haki kwa mataifa.
19Hatabishana au kupiga kelele;
hakuna atakayesikia sauti yake mitaani.
20Hatavunja wala kupindisha unyasi.
Hatazimisha hata mwanga hafifu.
Hatashindwa mpaka ameifanya haki kuwa mshindi.
21Watu wote watatumaini katika yeye.”#Isa 42:1-4
Nguvu ya Yesu Inatoka kwa Mungu
(Mk 3:20-30; Lk 11:14-23; 12:10)
22Kisha baadhi ya watu wakamleta mtu kwa Yesu. Mtu huyu alikuwa asiyeona na hakuweza kuzungumza, kwa sababu alikuwa na pepo ndani yake. Yesu akamponya na akaweza kuzungumza na kuona. 23Watu wote walikishangaa kile Yesu alichotenda. Walisema, “Pengine ni Mwana wa ahadi wa Daudi!”
24Mafarisayo waliposikia hili, walisema, “Mtu huyu anatumia nguvu za Shetani#12:24 Shetani Jina la Mwovu lenye maana “Adui”. Kwa maana ya kawaida, “Beelzebuli” kwa Kiyunani (mwovu). Pia katika mstari wa 27. kufukuza mashetani kutoka kwa watu. Beelzebuli ni mtawala wa mashetani.”
25Yesu alijua kile Mafarisayo walikuwa wanafikiri. Hivyo akawaambia, “Kila ufalme unaopigana wenyewe utateketezwa. Na kila mji au familia iliyogawanyika haiwezi kuishi. 26Hivyo ikiwa Shetani anayafukuza mashetani#12:26 ikiwa Shetani … mashetani Kwa maana ya kawaida, “ikiwa Shetani atamfukuza Shetani.” yake mwenyewe, anapigana kinyume chake yeye mwenyewe, na ufalme wake hautaishi. 27Mnasema kuwa ninatumia nguvu za Shetani kuyatoa mashetani. Ikiwa hiyo ni kweli, sasa ni nguvu gani watu wenu hutumia wanapoyafukuza mashetani? Hivyo watu wenu wenyewe watathibitisha kuwa mmekosea. 28Lakini ninatumia nguvu ya Roho wa Mungu kuyafukuza mashetani, na hili linaonesha kuwa Ufalme wa Mungu umekuja kwenu. 29Watu wowote wanaotaka kuingia katika nyumba ya mtu mwenye nguvu na kuiba vitu vyake lazima wamfunge kwanza. Kisha wanaweza kuiba vitu kutoka katika nyumba yake. 30Yeyote ambaye hayuko pamoja nami yu kinyume nami. Na yeyote ambaye hakusanyi pamoja nami hutawanya.
31Hivyo ninawaambia, Mungu atawasamehe watu kila dhambi wanayotenda au kila jambo baya wanalosema kinyume naye. Lakini yeyote anayesema kinyume na Roho Mtakatifu hatasamehewa. 32Unaweza kusema kinyume na Mwana wa Adamu na ukasamehewa. Lakini yeyote anayesema kinyume na Roho Mtakatifu hatasamehewa; si sasa au baadaye.
Yale Unayofanya Yanaonesha Jinsi Ulivyo
(Lk 6:43-45)
33Ikiwa unataka matunda mazuri, ni lazima uutunze mti vizuri. Ikiwa mti wako siyo mzuri, utakuwa na matunda mabaya. Mti unajulikana kutokana na aina ya matunda inaozalisha. 34Ninyi nyoka! Ni waovu sana. Mnawezaje mkasema chochote kilicho chema? Kile ambacho watu husema kwa midomo yao kinatoka katika yale yaliyojaa katika mioyo yao. 35Walio wema wana vitu vizuri vilivyotunzwa katika mioyo yao. Ndiyo maana husema mambo mazuri. Lakini wale walio waovu wana mioyo iliyojaa uovu, na ndiyo sababu husema mambo maovu. 36Ninawaambia kuwa kila mmoja atajibu kwa ajili ya mambo yasiyo ya maana waliyosema. Hili litatokea siku ya hukumu. 37Maneno yenu yatatumika kuwahukumu ninyi. Uliyosema yataamua ikiwa una haki mbele za Mungu au unahukumiwa na Mungu.”
Baadhi ya Watu Wawa na Mashaka na Mamlaka ya Yesu
(Mk 8:11-12; Lk 11:29-32)
38Kisha baadhi ya Mafarisayo na walimu wa sheria wakamjibu Yesu. Wakasema, “Mwalimu, tunataka kukuona ukifanya miujiza kama ishara kuwa unatoka kwa Mungu.”
39Yesu akajibu, “Watu wenye dhambi na wasio na imani hutafuta kuona muujiza kama ishara kutoka kwa Mungu. Lakini hakuna muujiza utakaofanyika kudhibitisha chochote kwao. Yona#12:39 Yona Au “Nabii Yona”, nabii katika Agano la Kale. Baada ya kukaa katika tumbo la samaki mkubwa kwa siku tatu alitoka akiwa mzima, kisha akaenda kwenye mji uliojaa uovu wa Ninawi kuwaonya watu huko kama alivyotumwa na Mungu. Kwa njia hiyo hiyo, Yesu angetoka kaburini siku ya tatu, ishara ya kuthibitisha ukweli wa ujumbe wake kutoka kwa Mungu. ni ishara pekee itakayotolewa kwenu ninyi mlio wa kizazi kiovu cha leo. 40Yona alikuwa ndani ya tumbo la samaki mkubwa kwa siku tatu, mchana na usiku. Vivyo hivyo, Mwana wa Adamu atakuwa kaburini kwa siku tatu, mchana na usiku. 41Siku ya hukumu, ninyi watu mnaoishi leo mtalinganishwa na watu wa Ninawi, nao watakuwa mashahidi watakaoonyesha namna mlivyokosea. Kwa nini ninasema hivi? Kwa sababu Yona alipowahubiri watu hao, walibadili maisha yao. Na aliye mkuu kuliko Yona, yupo hapa lakini mnakataa kubadilika!
42Pia, siku ya hukumu, Malkia wa Kusini#12:42 Malkia wa Kusini Au “Malkia wa Sheba.” Alisafiri kama maili 1,000 (kilomita 1,600) ili kujifunza hekima ya Mungu kutoka kwa Sulemani. Tazama 1 Fal 10:1-13. atasimama pamoja na wale wanaoishi sasa, atasababisha mhukumiwe kuwa na makosa. Ninasema hivi kwa sababu alisafiri kutoka mbali, mbali sana kuja kusikiliza mafundisho yenye hekima ya Sulemani. Nami Ninawaambia aliye mkuu zaidi ya Sulemani yuko hapa, lakini hamnisikii!
Hatari ya Kuwa Mtupu
(Lk 11:24-26)
43Roho chafu inapotoka kwa mtu, husafiri katika sehemu kavu ikitafuta mahali pa kupumzika, lakini haipati mahali pa kupumzika. 44Inapokosa mahali pa kupumzika, husema, ‘Nitarudi katika nyumba niliyotoka.’ Inaporudi, ikakuta nyumba hiyo bado ni tupu, ikiwa safi na nadhifu, 45hutoka nje na kuleta roho zingine saba zilizo chafu zaidi yake. Huingia na kuishi humo, na mtu huyo anakuwa na matatizo mengi kuliko mwanzo wakati roho chafu moja iliishi ndani yake. Ndivyo ilivyo kwa kizazi hiki cha watu wanaoishi leo.”
Wafuasi wa Yesu ni Familia Yake Halisi
(Mk 3:31-35; Lk 8:19-21)
46Yesu alipokuwa akiongea na watu, mama yake na ndugu zake walikuwa nje. Walitaka kuongea naye. 47Mtu mmoja akamwambia, “Mama yako na wadogo zako wanakusubiri nje. Wanataka kuongea nawe.”
48Yesu akajibu, “Mama yangu ni nani? Ndugu zangu ni nani?” 49Kisha akanyoosha kidole kwa wafuasi wake na akasema, “Unaona! Watu hawa ni mama yangu na ndugu zangu. 50Kaka yangu, dada yangu na mama yangu halisi ni yule anayefanya yale Baba yangu wa mbinguni anataka.”

Tällä hetkellä valittuna:

Mathayo 12: TKU

Korostus

Jaa

Kopioi

None

Haluatko, että korostuksesi tallennetaan kaikille laitteillesi? Rekisteröidy tai kirjaudu sisään