Logo YouVersion
Îcone de recherche

Yohana UTANGULIZI

UTANGULIZI
Ijapokuwa jina la mwandishi wa Injili hii halitajwi katika Injili yenyewe, tangu karne ya pili Baada ya Kristo Kuzaliwa mapokeo ya Wakristo wa mwanzoni yanasema kuwa ni Yohana, mwana wa Zebedayo, nduguye Yakobo, mwanafunzi wa Yesu. Mama yake alikuwa Salome ambaye dada yake, Mariamu, alikuwa mama yake Yesu. Kwa hiyo, Yohana na Yesu walikuwa ndugu kwa upande wa mama zao (Mt 10:2; 27:56; Mk 15:40; Yn 19:25-27). Pengine huitwa “mwanafunzi ambaye Yesu alimpenda”, aliyeegamia kifuani mwa Yesu (13:23-25; 19:26-27; 21:7,20). Mapokeo hayo hutokana na ushuhuda uliomo katika Injili kwamba yote aliyoyaandika alikuwa ameyashuhudia yeye mwenyewe (1:14; 19:35: 21:24). Naye aliishi miaka mingi kuliko wanafunzi wenzake. Wakati wa uzee wake alikaa Efeso na huenda aliandika Injili hii akiwa huko.
Injili hii inaeleza fumbo la nafsi yake Yesu. Yohana anatupeleka mpaka kwenye kiini cha huduma ya Yesu, akitupa fursa ya kuona kidogo chanzo chake cha milele na maumbile yake ya uungu. Kadiri ya Injili hii Yesu alikuwa wa pekee kabisa: “Hapo mwanzo alikuwa na Mungu”, alishiriki katika kitendo cha kuumba ulimwengu, alikuwa chanzo cha nuru na uzima (1:2-3). Kutokana na hilo, alipojichukulia mwili wa kibinadamu, aliwajulisha watu juu ya Mungu wa milele ambaye alikuwa naye, lakini ambaye “hakuna mtu aliyemwona wakati wowote” (1:14,18). Kama waandishi wengine wa Injili, mwandishi huyu naye pia anatupa kumbukumbu za kweli za maisha, mafundisho na matendo ya Yesu, lakini yeye, zaidi ya wote wengine anakwenda mbali zaidi na kufafanua matukio hayo. Anatumia ishara za kawaida zilizochukuliwa kutoka maisha kwa mfano: mkate, maji, nuru, uzima au uhai, neno, mchungaji, njia, n.k. ili kufanya maana kamili ya Yesu iwe wazi na yenye kumbana kabisa msomaji au msikilizaji wa Injili. Baada ya utangulizi ambao ni wa kusisimua mno (1:1-18), mwandishi anatoa picha ya Yesu kama mtu ambaye binadamu anapaswa kumwamini (1:9—4:54), kisha anatoa habari za Yesu ambazo kwa jumla zinaonesha mzozo kati yake na wasioamini (5—12). Tazama hasa mzozo kati ya Yesu na Mafarisayo katika 8:31-59; 10:19-39, halafu kuna habari ambazo zinahusu zaidi uhusiano wake mwema na wale walioamini (13—17), habari za kifo na kufufuka kwake (18—20) na kumalizia na hatima (sura 21).
Sehemu ya kwanza ya Injili hii ina kumbukumbu za miujiza saba ya Yesu, miujiza ambayo mwandishi anaiita “ishara” maana kwa jumla ilidhihirisha utukufu wake (2:11) na hivyo kuamsha na kuimarisha imani ya wanafunzi wake. Hata hivyo, mwandishi anajua kwamba Yesu alitenda miujiza mingi zaidi ambayo haikuandikwa katika Injili hii (20:30).
Kusudi la mwandishi ni kuushuhudia ulimwengu kwamba Yesu ndiye Masihi, Mwana wa Mungu na mtoaji pekee wa uzima wa milele. Watu wanapaswa kumwamini ili wapokee uzima wa milele (20:30-31). Yesu ni Mungu kweli maana alikuwapo tangu milele, aliumba vitu vyote, alitoka mbinguni ili amdhihirishe Mungu kwa wanadamu (1:1-3,18; 3:13; 5:18-19; 14:9,11). Vile vile Yesu alikuwa mwanadamu kweli. Alikuwa na mwili wa kawaida pamoja na hisia za binadamu (1:14; 4:6-7; 9:6; 11:35; 12:27; 19:28,34).

Sélection en cours:

Yohana UTANGULIZI: SRUVDC

Surbrillance

Partager

Copier

None

Tu souhaites voir tes moments forts enregistrés sur tous tes appareils? Inscris-toi ou connecte-toi