Yohana 3
3
Yesu na Nikodemu
1Alikuwepo mtu aliyeitwa Nikodemu, mmoja wa Mafarisayo. Yeye alikuwa kiongozi muhimu sana wa Kiyahudi. 2Usiku mmoja alikwenda kwa Yesu na kumwambia, “Mwalimu, tunajua kuwa wewe ni mwalimu uliyetumwa kutoka kwa Mungu. Hayupo mtu yeyote anayeweza kutenda ishara na miujiza unayotenda bila msaada wa Mungu.”
3Yesu akajibu, “Hakika nakuambia, ni lazima kila mtu azaliwe upya.#3:3 azaliwe upya Kuzaliwa tena katika mstari huu na ule wa 7 maneno haya yanaweza kutafsiriwa “kuzaliwa kutoka juu”. Yeyote ambaye hajazaliwa mara ya pili hawezi kuingia katika ufalme wa Mungu.”
4Nikodemu akasema, “Yawezekanaje mtu ambaye tayari ni mzee akazaliwa tena? Je! anaweza kuingia tena katika tumbo la mama yake na kuzaliwa kwa mara ya pili?”
5Yesu akamjibu, “Uniamini ninapokwambia kuwa kila mtu anapaswa kuzaliwa tena kwa maji na kwa Roho. Yeyote ambaye hakuzaliwa kwa maji na kwa Roho hawezi kuuingia ufalme wa Mungu. 6Maisha pekee ambayo watu huyapata kutoka kwa wazazi wao ni ya kimwili. Lakini maisha mapya anayopewa mtu na Roho ni ya kiroho. 7Usishangae kwa kuwa nilikuambia, ‘Ni lazima mzaliwe upya.’ 8Upepo huvuma kuelekea popote unakopenda. Unausikia, lakini huwezi kujua unakotoka na unakoelekea. Hivyo ndivyo ilivyo kwa kila aliyezaliwa kwa Roho.”
9Nikodemu akauliza, “Je! haya yote yanawezekana namna gani?”
10Yesu akasema, “Wewe ni mwalimu mashuhuri wa Israeli, inakuwaje huelewi mambo haya? 11Ukweli ni kwamba, tunaongea yale tunayoyafahamu. Tunayasema yale tuliyoyaona. Hata hivyo ninyi hamyakubali yale tunayowaambia. 12Nimewaeleza juu ya mambo ya hapa duniani, lakini hamniamini. Vivyo hivyo nina uhakika hamtaniamini hata nikiwaeleza mambo ya mbinguni! 13Sikiliza, hakuna mtu aliyewahi kwenda kwa Mungu mbinguni isipokuwa Mwana wa Adamu. Yeye pekee ndiye aliyekuja duniani kutoka mbinguni.”
14Unakumbuka yule nyoka wa shaba ambaye Musa alimwinua kule jangwani?#3:14 Musa alimwinua … jangwani Wakati watu wa Mungu walikuwa wanakufa kutokana na kuumwa na nyoka, Mungu alimwambia Musa kuweka nyoka wa shaba kwenye mlingoti ili waweze kumwangalia na kuponywa. Tazama Hes 21:4-9. Vivyo hivyo Mwana wa Adamu anapaswa kuinuliwa juu. 15Kisha kila anayemwamini aweze kuupata uzima wa milele.#3:15 Wataalamu wengine wanafikiri kwamba maneno ya Yesu kwa Nikodemo yanaendelea hadi mstari wa 21.
16Kweli, hivi ndivyo Mungu alivyouonyesha upendo wake mkuu kwa ulimwengu: akamtoa Mwanawe wa pekee, ili kila mtu anayemwamini asiharibiwe na mauti bali aupate uzima wa milele. 17Mungu alimtuma Mwanawe ili kuuokoa ulimwengu. Hakumtuma kuja kuuhukumu na kuuweka hatiani, bali kuuokoa kwa njia ya mwanawe. 18Wote wanaomwamini Mwana wa Mungu hawahukumiwi hatia yoyote. Lakini wale wasiomwamini wamekwisha kuhukumiwa tayari, kwa sababu hawakumwamini Mwana pekee wa Mungu. 19Wamehukumiwa kutokana na ukweli huu: Kwamba nuru#3:19 nuru Lenye maana ya Kristo, Neno, aliyeleta ulimwenguni uelewa kuhusu Mungu. imekuja ulimwenguni, lakini watu hawakuitaka nuru. Bali walilitaka giza, kwa sababu walikuwa wanatenda mambo maovu. 20Kila anayetenda maovu huichukia nuru. Hawezi kuja kwenye nuru, kwa sababu nuru itayaweka wazi matendo maovu yote aliyotenda.
21Lakini yeyote anayeifuata njia ya kweli huja kwenye nuru. Nayo nuru itaonesha kuwa Mungu amekuwepo katika matendo yake yote.
Yesu na Yohana Mbatizaji
22Baada ya hayo, Yesu na wafuasi wake wakaenda katika eneo la Uyahudi. Kule Yesu alikaa pamoja na wafuasi wake na kuwabatiza watu. 23Yohana naye alikuwa akiwabatiza watu kule Ainoni, eneo karibu na Salemu mahali palipokuwa na maji mengi. Huko ndiko watu walipoenda kubatizwa. 24Hii ilikuwa kabla ya Yohana kufungwa gerezani.
25Baadhi ya wafuasi wa Yohana walikuwa na mabishano pamoja na Myahudi mwingine juu ya utakatifu.#3:25 ya utakatifu Wayahudi walikuwa na sheria za kidini za kunawa maji kwa namna maalumu kabla ya kula, kabla ya kufanya ibada katika Hekalu, na pia nyakati zingine maalumu. 26Ndipo wakaja kwa Yohana na kusema, “Mwalimu, unamkumbuka mtu aliyekuwa pamoja nawe ng'ambo ya Mto Yordani? Yule uliyekuwa ukimwambia kila mtu juu yake.” Huyo pia anawabatiza watu na wengi wanaenda kwake.
27Yohana akajibu, “Mtu anaweza tu kuyapokea yale ambayo Mungu anayatoa. 28Ninyi wenyewe mlinisikia nikisema, ‘Mimi siye Masihi. Mimi ni mtu yule aliyetumwa na Mungu kutengeneza njia kwa ajili ya Masihi.’ 29Bibi arusi siku zote yupo kwa ajili ya bwana arusi. Rafiki anayemsindikiza bwana arusi yeye hungoja na kusikiliza tu na hufurahi anapomsikia bwana arusi akiongea. Hivyo ndivyo ninavyojisikia sasa. Ninayo furaha sana kwani Masihi yuko hapa. 30Yeye anapaswa kuwa juu zaidi yangu mimi, na mimi napaswa kuwa chini yake kabisa.”
Ajaye Kutoka Mbinguni
31“Anayekuja kutoka juu ni mkubwa kuliko wengine wote. Anayetoka duniani ni wa dunia. Naye huzungumza mambo yaliyo ya duniani. Lakini yeye anayekuja kutoka mbinguni ni mkuu kuliko wengine wote. 32Huyo huyasema aliyoyaona na kuyasikia, lakini watu hawayapokei anayoyasema. 33Bali yeyote anayepokea anayoyasema basi amethibitisha kwamba Mungu husema kweli. 34Na kwamba Mungu alimtuma, na yeye huwaeleza watu yale yote Mungu aliyoyasema. Huyo Mungu humpa Roho kwa ujazo kamili. 35Baba anampenda Mwana na amempa uwezo juu ya kila kitu. 36Yeyote anayemwamini Mwana anao uzima wa milele. Lakini wale wasiomtii Mwana hawataupata huo uzima. Na hawataweza kuiepuka hasira ya Mungu.”
वर्तमान में चयनित:
Yohana 3: TKU
हाइलाइट
शेयर
कॉपी
Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi
Toleo la Awali
© 2017 Bible League International