Yohana 5
5
Yesu Amponya Mtu Bwawani
1Baadaye, Yesu akaenda Yerusalemu kwa ajili ya sikukuu maalumu ya Wayahudi. 2Huko Yerusalemu kulikuwa na bwawa lenye mabaraza matano. Kwa Kiaramu liliitwa Bethzatha.#5:2 Bethzatha Pia huitwa Bethsaida au Bethesda. Ama bwawa la maji lililoko kaskazini mwa Hekalu kule. Bwawa hili lilikuwa karibu na Lango la Kondoo. 3Wagonjwa wengi walikuwa wamelala katika mabaraza pembeni mwa bwawa. Baadhi yao walikuwa wasiyeona, wengine walemavu wa viungo, na wengine waliopooza mwili.#5:3 Nakala zingine za Kiyunani zimeongeza, “na husubiri maji yatibuliwe”. 4Nyakati zingine malaika wa Bwana alishuka bwawani na kuyatibua maji. Baada ya hapo, mtu wa kwanza aliyeingia bwawani aliponywa ugonjwa aliokuwa nao.#5:4 Nakala zingine za baadaye ziliongeza mstari wa 4, hivyo kutenganisha mstari wa 4 na wa 5: “Nyakati zingine malaika wa Bwana alishuka bwawani na kuyatibua maji. Baada ya hapo, mtu wa kwanza aliyeingia bwawani aliponywa ugonjwa aliokuwa nao.” 5Mmoja wa watu waliolala hapo alikuwa mgonjwa kwa muda wa miaka thelathini na minane. 6Yesu alimwona akiwa amelala hapo na kutambua kuwa amekuwa mgonjwa kwa muda mrefu sana. Hivyo akamwuliza, “Je! unataka kuwa mzima?”
7Yule mgonjwa akajibu, “Bwana, hakuna mtu wa kunisaidia kuingia kwenye bwawa mara maji yanapotibuliwa. Najitahidi kuwa wa kwanza kuingia majini. Lakini ninapojaribu, mtu mwingine huniwahi na kuingia majini kabla yangu.”
8Kisha Yesu akasema, “Simama juu! Beba kirago chako na utembee.” 9Mara hiyo, mtu huyo akapona. Akabeba kirago chake na kuanza kutembea.
Siku yalipotokea haya yote ilikuwa ni Siku ya Sabato.#5:9 Siku ya Sabato Ilikuwa siku maalumu kwa Waisraeli na Wayahudi. Kwa amri ya Mungu siku hiyo ilitengwa kama siku ya mapumziko na ya kumheshimu Mungu. 10Hivyo baadhi ya Wayahudi wakamwambia yule mtu aliyeponywa, “Leo ni Sabato. Kulingana na sheria yetu wewe hauruhusiwi kubeba mkeka katika siku ya Sabato!”
11Lakini yeye akajibu, “Yule mtu aliyeniponya aliniambia, ‘Beba mkeka wako uende.’”
12Wakamwuliza, “Ni nani aliyekuambia kubeba mkeka wako na kutembea?”
13Lakini yule mtu aliyeponywa hakuwa amemfahamu ni nani. Walikuwepo watu wengi hapo, na Yesu alikwisha kuondoka.
14Baadaye, Yesu akamwona huyo mtu Hekaluni na akamwambia, “Tazama, umepona sasa. Kwa hivyo uache kutenda dhambi tena, la sivyo jambo baya zaidi laweza kukupata.” 15Kisha huyo mtu akaondoka na kurudi kwa wale Wayahudi waliomuuliza. Naye aliwaeleza kuwa Yesu ndiye aliyemponya.
16Yesu alikuwa anayafanya yote haya katika siku ya Sabato. Hivyo Wayahudi hao wakaanza kumsumbua asiendelee. 17Lakini yeye akawaambia, “Baba yangu hajawahi kuacha kufanya kazi, hivyo nami pia nafanya kazi.” 18Hili likawafanya waongeze juhudi ya kumwua. Wakasema, “Mwanzoni mtu huyu alikuwa anavunja sheria kuhusu siku ya Sabato. Kisha akasema kwamba Mungu ni Baba yake! Yeye anajifanya kuwa yuko sawa na Mungu.”
Yesu Anayo Mamlaka ya Mungu
19Lakini Yesu akajibu, “Hakika nawaambieni kuwa Mwana hawezi kufanya chochote peke yake. Bali hufanya tu yale anayoona Baba yake anayafanya. Kwa maana Mwana hufanya mambo ambayo Baba huyafanya. 20Baba anampenda Mwana na humwonesha kila kitu anachofanya. Pia Baba atamwonesha Mwana mambo makuu ya kufanya kuliko hili. Kisha nyote mtashangazwa. 21Baba huwafufua wafu na kuwapa uzima. Kwa njia hiyo hiyo, Mwana pia huwapa uzima wale anaowataka.”
22“Vile vile, Baba hamhukumu mtu. Bali amempa Mwana nguvu ya kufanya hukumu zote. 23Mungu alifanya hivi ili watu wote waweze kumheshimu Mwana kama vile wanavyomheshimu Baba. Mtu yeyote asiyemheshimu Mwana hamheshimu Baba. Kwani Baba ndiye aliyemtuma Mwana.
24Kwa hakika nawaambia, yeyote anayesikia ninayosema na kumwamini yule aliyenituma anao uzima wa milele. Hawa hawatahukumiwa kuwa na hatia. Kwani tayari wameshaivuka mauti na kuingia ndani ya uzima. 25Mniamini, wakati muhimu sana unakuja. Wakati huo tayari upo ambapo watu waliokufa wataisikia sauti ya Mwana wa Mungu. Na hao watakaoisikia watafufuka na kuwa hai. 26Uzima huja kutoka kwa Baba mwenyewe. Na pia Baba amemruhusu Mwana kutoa uzima. 27Na Baba amempa Mwana mamlaka ya kuwahukumu watu wote kwa sababu yeye ndiye Mwana wa Adamu.
28Ninyi msishangazwe na hili. Wakati unakuja ambapo watu wote waliokufa na kuwamo makaburini mwao wataisikia sauti yake. 29Kisha watatoka nje ya makaburi yao. Wale waliotenda mema watafufuka na kupata uzima wa milele. Lakini wale waliotenda maovu watafufuka na kuhukumiwa kwa kuwa na hatia.
30Siwezi kufanya jambo lolote peke yangu. Ninahukumu kama vile ninavyoagizwa. Na hukumu yangu ni halali, kwa sababu sitafuti kujifurahisha mwenyewe. Bali ninataka tu kumfurahisha yeye aliyenituma.”
Yesu Asema Zaidi Na Viongozi wa Kiyahudi
31“Endapo nitawaeleza watu mambo yangu mwenyewe, watu hawatakuwa na uhakika kama yale ninayosema ni kweli. 32Lakini yupo mwingine anayewaeleza watu mambo yangu, nami nafahamu kuwa yale anayoyasema juu yangu ni kweli.
33Mliwatuma watu kwa Yohana, naye akawaambia yaliyo kweli. 34Hivyo sihitaji mtu yeyote wa kuwaeleza watu juu yangu, isipokuwa nawakumbusha ninyi yale aliyoyasema Yohana ili muweze kuokolewa. 35Yohana alikuwa kama taa iliyowaka na kutoa mwanga, nanyi mlipata raha mkiufurahia mwanga wake japo kwa muda.
36Hata hivyo uthibitisho nilionao mwenyewe juu yangu ni mkuu kuliko chochote alichokisema Yohana. Mambo ninayofanya ndiyo yanayonithibitisha. Haya ndiyo Baba aliyonipa kufanya. Nayo yanadhihirisha kuwa Baba alinituma. 37Na Baba aliyenituma yeye mwenyewe ametoa uthibitisho juu yangu. Lakini hamjawahi kabisa kuisikia sauti yake. Hamjawahi pia kuuona uso wake jinsi ulivyo. 38Mafundisho ya Baba hayakai ndani yenu, kwa sababu hamumwamini yule aliyetumwa na Baba. 39Mnajifunza Maandiko kwa makini. Nanyi mnafikiri kuwa yanawapa uzima wa milele. Maandiko haya haya yanaeleza habari zangu! 40Lakini mnakataa kuja kwangu kuupata huo uzima.
41Sitaki kutukuzwa nanyi ama na mwanadamu mwingine yeyote. 42Hata hivyo ninawajua ninyi, na ninajua kwamba hamna upendo kwa Mungu. 43Nimekuja kutoka kwa Baba yangu nami ni msemaji wake, lakini hamnikubali. Lakini watu wengine wakija wakijisemea mambo yao tu, mnawakubali! 44Ninyi mnapenda kupeana sifa kila mmoja kwa mwenzake. Lakini hamjaribu kupata sifa zinazotoka kwa Mungu wa pekee. Hivyo mtawezaje kuamini? 45Msifikiri kwamba mimi ndiye nitakayesimama mbele za Baba na kuwashtaki. Musa ndiye atakayewashtaki. Na ndiye mliyetegemea angeliwaokoa. 46Kama kwa hakika mlimwamini Musa, nami mlipaswa kuniamini, kwa sababu yeye aliandika habari juu yangu. 47Lakini hamuyaamini aliyoyaandika, hivyo hamuwezi kuyaamini ninayoyasema.”
वर्तमान में चयनित:
Yohana 5: TKU
हाइलाइट
शेयर
कॉपी
Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi
Toleo la Awali
© 2017 Bible League International