Luka 19

19
Zakayo
1Yesu alikuwa anasafiri kupitia katika mji wa Yeriko. 2Katika mji wa Yeriko alikuwepo mtu aliyeitwa Zakayo. Alikuwa mtoza ushuru mkuu na alikuwa tajiri. 3Alitaka kumwona Yesu na watu wengine wengi walitaka kumwona Yesu pia. Lakini alikuwa mfupi na hakuweza kuona juu ya watu. 4Hivyo alikimbia akaenda mahali alipojua kuwa Yesu angepita. Kisha akapanda mkuyu ili aweze kumwona Yesu.
5Yesu alipofika mahali alipokuwa Zakayo, alitazama juu na kumwona akiwa kwenye mti. Yesu akasema, “Zakayo, shuka upesi! Ni lazima nikae nyumbani mwako leo.”
6Zakayo alishuka chini haraka. Alifurahi kuwa na Yesu nyumbani mwake. 7Kila mtu aliliona hili na watu wakaanza kulalamika, wakisema, “Tazama aina ya mtu ambaye Yesu anakwenda kukaa kwake. Zakayo ni mwenye dhambi!”
8Zakayo akamwambia Bwana, “Sikiliza Bwana nitawapa maskini nusu ya pesa zangu. Ikiwa nilimdhulumu mtu yeyote, nitamrudishia mara nne zaidi.”
9Yesu akasema, “Leo ni siku kwa ajili ya familia hii kuokolewa kutoka katika dhambi. Ndiyo, hata mtoza ushuru huyu ni mmoja wa wateule wa Mungu.#19:9 mmoja wa wateule wa Mungu Kwa maana ya kawaida, “mwana wa Abrahamu”. 10Mwana wa Adamu alikuja kuwatafuta na kuwaokoa watu waliopotea.”
Simulizi Kuhusu Watumishi Watatu
(Mt 25:14-30)
11Kundi la watu walipokuwa bado wanamsikiliza Yesu akizungumza mambo haya. Akaongeza kwa kuwasimulia simulizi hii. Na sasa alikuwa karibu na mji wa Yerusalemu na watu walidhani kuwa ufalme wa Mungu ulikuwa unakwenda kutokea haraka. 12Akasema, “Mtu mmoja maarufu alikuwa anajiandaa kwenda katika nchi ya mbali kutawazwa kuwa mfalme. Kisha arudi nyumbani na kuwatawala watu wake. 13Hivyo aliwaita watumishi wake kumi kwa pamoja. Akampa kila mtumishi fungu la pesa.#19:13 fungu la pesa Fungu moja la pesa kwa Kiyunani liliitwa mina, ambayo ni sarafu 100 za fedha, uliotosha kumlipa mtu mshahara kwa miezi mitatu. Pia katika mstari wa 16,18,20,24 na 25. Akamwambia kila mtumishi, ‘Zifanyie biashara pesa hizi mpaka nitakaporudi.’ 14Lakini watu katika ule ufalme walikuwa wanamchukia mtu huyu na hivyo walituma kundi la watu kwenda katika nchi nyingine. Walipofika huko wakasema, ‘Hatutaki mtu huyu awe mfalme wetu.’
15Lakini mtu yule akatawazwa kuwa mfalme. Aliporudi nyumbani, akaagiza akasema, ‘Waiteni wale watumishi wenye pesa zangu. Ninataka kujua wamezalisha kiasi gani kutokana na pesa hizo.’ 16Mtumishi wa kwanza alikuja na akasema, ‘Mkuu, nilizalisha mafungu kumi ya pesa kutokana na fungu moja ulilonipa.’ 17Mfalme akamwambia, ‘Vizuri sana! Wewe ni mtumishi mwema. Nilikuamini kwa vitu vidogo, lakini sasa utakuwa mtawala wa miji yangu kumi.’
18Mtumishi wa pili akasema, ‘Mkuu, kwa fungu moja la pesa zako, nilizalisha mafungu matano.’ 19Mfalme akamwambia mtumishi huyu, ‘Utatawala miji yangu mitano.’
20Kisha mtumishi mwingine akaingia na akasema, ‘Mkuu, fungu lako la pesa hili hapa. Nilizifunga katika kipande cha nguo na kulificha. 21Niliogopa kwa sababu wewe ni mgumu. Unachukua hata pesa ambazo hukuzizalisha na kukusanya chakula ambacho hukupanda.’
22Kisha mfalme akamwambia, ‘Wewe ni mtumishi mbaya! Nitatumia maneno yako mwenyewe kukuhukumu. Unasema kuwa mimi ni mtu mgumu, ninachukua hata pesa ambazo sikuzizalisha na nakusanya chakula ambacho sikupanda? 23Ikiwa hiyo ni kweli, ulipaswa kuweka pesa zangu kwa watoao riba. Ili nitakaporudi pesa hiyo iwe imezalisha faida.’ 24Kisha mfalme akawaambia watu waliokuwa pale, ‘Mnyang'anyeni mtumishi huyu fungu la pesa na mpeni mtumishi aliyezalisha mafungu kumi ya pesa.’
25Lakini watu wakamwambia mfalme, ‘Mkuu, yule mtumishi ana mafungu kumi tayari.’
26Mfalme akasema, ‘Waliozalisha faida watapata zaidi. Lakini ambao hawakuzalisha faida watanyang'anywa kila kitu. 27Sasa, adui zangu wako wapi? Wako wapi watu ambao hawakutaka niwe mfalme? Waleteni adui zangu hapa na waueni huku nikiangalia wanavyokufa.’”
Yesu Aingia Yerusalemu Kama Mfalme
(Mt 21:1-11; Mk 11:1-11; Yh 12:12-19)
28Baada ya Yesu kusema mambo haya, aliendelea kusafiri kuelekea Yerusalemu. 29Akakaribia Bethfage na Bethania, miji iliyo karibu na kilima kinachoitwa Mlima wa Mizeituni. Kisha akawatuma wawili miongoni mwa wafuasi wake, 30akawaambia, “Nendeni kwenye mji mnaoweza kuuona pale. Mtakapoingia mjini, mtamwona mwanapunda amefungwa ambaye bado mtu yeyote hajampanda. Mfungueni na mleteni hapa kwangu. 31Kama mtu yeyote akiwauliza, ‘Kwa nini mnamfungua?’ Semeni, ‘Bwana anamhitaji.’”
32Wafuasi wawili wakaenda kwenye mji ule. Wakamwona punda kama Yesu alivyowaambia. 33Wakamfungua, lakini wamiliki wa punda wakatoka. Wakawauliza wafuasi wa Yesu, “Kwa nini mnamfungua punda wetu?”
34Wafuasi wakajibu, “Bwana anamhitaji.” 35Hivyo wafuasi wakampeleka punda kwa Yesu. Wakatandika baadhi ya nguo zao juu ya mwanapunda, kisha wakampandisha Yesu juu yake. 36Yesu akaanza kwenda Yerusalemu. Wafuasi walikuwa wanatandaza nguo zao njiani mbele yake.
37Yesu alipokaribia Yerusalemu. Alipokuwa katika njia inayotelemka kutoka kwenye Mlima wa Mizeituni, kundi lote la wafuasi wake wakaanza kumsifu Mungu kwa kupaza sauti. Walimsifu Mungu kwa furaha kwa sababu ya miujiza yote waliyoiona. 38Walisema,
“Karibu! Mungu ambariki mfalme
anayekuja kwa jina la Bwana!#Zab 118:26
Amani iwe mbinguni,
na utukufu kwa Mungu!”
39Baadhi ya Mafarisayo waliokuwa katika kundi wakamwambia Yesu, “Mwalimu, waambie wafuasi wako wasiseme mambo haya!”
40Lakini Yesu akawajibu, “Ninawaambia ikiwa wafuasi wangu wasingesema, mawe haya yangesema kwa kupaza sauti!”
Yesu Aulilia Mji wa Yerusalemu
41Yesu alipoukaribia mji wa Yerusalemu, akautazama kisha akaanza kuulilia, 42akisema, “Laiti ungelijua leo kile kinachokuletea amani. Lakini kimefichwa kwako usikijue sasa. 43Wakati unakuja, ambao adui zako watajenga ukuta kukuzunguka na kukuzingira pande zote. 44Watakuteketeza wewe na watu wako wote. Hakuna jiwe hata moja katika majengo yako litaachwa juu ya jiwe jingine. Haya yote yatatokea kwa sababu hukujua wakati ambao Mungu alikuja kukuokoa.”
Yesu Asafisha Eneo la Hekalu
(Mt 21:12-17; Mk 11:15-19; Yh 2:13-22)
45Yesu aliingia katika eneo la Hekalu. Akaanza kuwafukuza watu waliokuwa wanauza vitu humo. 46Akasema, “Maandiko yanasema, ‘Hekalu langu litakuwa nyumba ya sala.’#Isa 56:7 Lakini mmeligeuza kuwa ‘maficho ya wezi.’”#Yer 7:11
47Yesu aliwafundisha watu kila siku katika eneo la Hekalu. Viongozi wa makuhani, walimu wa sheria na baadhi ya viongozi wa watu walikuwa wakitafuta namna ya kumwua. 48Lakini hawakujua namna ambavyo wangefanya, kwa sababu alikuwa anazungukwa na watu kila wakati waliokuwa wakimsikiliza. Kila mtu alifurahia yale ambayo Yesu alikuwa anasema, hawakuacha kumsikiliza.

वर्तमान में चयनित:

Luka 19: TKU

हाइलाइट

शेयर

कॉपी

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in