Luka 10

10
Isa Awatuma Wale Sabini Na Wawili
1 Baada ya hayo, Isa akawachagua wengine sabini na wawili, akawatuma wawili wawili katika kila mji na kila sehemu aliyokusudia kwenda baadaye. 2 Akawaambia, “Mavuno ni mengi, lakini watendakazi ni wachache. Kwa hiyo mwombeni Bwana wa mavuno, ili apeleke watendakazi katika shamba lake la mavuno. 3 Haya! nendeni. Ninawatuma kama wana-kondoo katikati ya mbwa mwitu. 4 Msichukue mkoba, wala mfuko, wala viatu, na msimsalimu mtu yeyote njiani.
5 “Mkiingia katika nyumba yoyote, kwanza semeni, ‘Amani iwe kwenu.’ 6Kama kuna mtu wa amani humo, basi amani yenu itakuwa juu yake. La sivyo, itawarudia. 7 Kaeni katika nyumba hiyo, mkila na kunywa kile watakachowapa, kwa sababu kila mtendakazi anastahili malipo yake. Msihamehame kutoka nyumba hadi nyumba.
8 “Mkienda katika mji na watu wake wakawakaribisha, kuleni chochote kiwekwacho mbele yenu, 9 waponyeni wagonjwa waliomo na waambieni: ‘Ufalme wa Mwenyezi Mungu umekaribia.’ 10Lakini mkiingia katika mji, nao hawakuwakaribisha, tokeni mwende katika barabara zake mkaseme: 11 ‘Hata mavumbi ya mji wenu yaliyoshikamana na miguu yetu, tunayakung’uta dhidi yenu. Lakini mjue kwamba Ufalme wa Mwenyezi Mungu umekaribia.’ 12 Ninawaambia, itakuwa rahisi zaidi kwa Sodoma kustahimili katika siku ile kuliko mji ule.
Onyo Kwa Miji Isiyotubu
(Mathayo 11:20-24)
13 “Ole wako Korazini! Ole wako Bethsaida! Kwa kuwa kama miujiza iliyofanyika kwenu ingefanyika Tiro na Sidoni, miji hiyo ingekuwa imetubu zamani, kwa kuvaa magunia na kujipaka majivu. 14Lakini itakuwa rahisi zaidi kwa Tiro na Sidoni kustahimili katika siku ya hukumu, kuliko ninyi. 15 Nawe, Kapernaumu, je, utainuliwa hadi mbinguni? La hasha, utashushwa mpaka kuzimu.”
16 “Yeye awasikilizaye ninyi anisikiliza mimi; naye awakataaye ninyi amenikataa mimi. Lakini yeye anikataaye mimi amkataa yeye aliyenituma.”
17 Wale sabini na wawili wakarudi kwa furaha, na kusema, “Bwana Isa, hata pepo wachafu wanatutii kwa jina lako.”
18 Isa akawaambia, “Nilimwona Shetani akianguka kutoka mbinguni kama umeme wa radi. 19 Tazama nimewapa mamlaka ya kukanyaga nyoka na nge na juu ya nguvu zote za adui; wala hakuna kitu chochote kitakachowadhuru. 20 Basi, msifurahi kwa kuwa pepo wachafu wanawatii, bali furahini kwa kuwa majina yenu yameandikwa mbinguni.”
Isa Anashangilia
(Mathayo 11:25-27; 13:16-17)
21 Wakati huo Isa akashangilia katika Roho wa Mwenyezi Mungu, akasema, “Nakuhimidi Baba,#10:21 Jina Baba linaonyesha uhusiano maalum wa Isa na Mwenyezi Mungu. Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa umewaficha mambo haya wenye hekima na wenye elimu, nawe ukawafunulia watoto wadogo. Naam, Baba, kwa kuwa hivyo ndivyo ilivyokupendeza.
22 “Nimekabidhiwa vitu vyote na Baba yangu. Hakuna mtu amjuaye Mwana ni nani ila Baba, wala hakuna amjuaye Baba ni nani ila Mwana na yeyote ambaye Mwana anapenda kumfunulia.”
23 Basi Isa akawageukia wanafunzi wake akanena nao faraghani, akawaambia, “Heri macho yanayoona yale mambo mnayoyaona. 24 Kwa maana nawaambia, manabii wengi na wafalme walitamani kuona yale mnayoyaona lakini hawakuyaona, na walitamani kusikia yale mnayoyasikia lakini hawakuyasikia.”
Mfano Wa Msamaria Mwema
25 Wakati huo mtaalamu mmoja wa sheria alisimama ili kumjaribu Isa, akamuuliza, “Mwalimu, nifanye nini ili niurithi uzima wa milele?”
26Isa akamjibu, “Imeandikwaje katika Torati? Kwani unasoma nini humo?”
27 Akajibu, “ ‘Mpende Bwana Mwenyezi Mungu wako kwa moyo wako wote, kwa roho yako yote, kwa nguvu zako zote, na kwa akili zako zote’; tena, ‘Mpende jirani yako kama unavyojipenda mwenyewe.’ ”
28 Isa akamwambia, “Umejibu vyema. Fanya hivyo nawe utaishi.”
29 Lakini yule mtaalamu wa Torati, akitaka kujionyesha kuwa mwenye haki, akamuuliza Isa, “Jirani yangu ni nani?”
30Isa akamjibu akasema, “Mtu mmoja alikuwa akiteremka kutoka Yerusalemu kwenda Yeriko, naye akaangukia mikononi mwa wanyang’anyi. Wakampiga, wakaondoka, wakamwacha akiwa karibu kufa. 31 Kuhani mmoja alikuwa akipitia njia ile, alipomwona huyo mtu, akapita upande mwingine, akamwacha hapo barabarani. 32Vivyo hivyo, Mlawi mmoja naye alipofika mahali pale, alimwona, akapita upande mwingine, akamwacha hapo barabarani 33 Lakini Msamaria mmoja aliyekuwa akisafiri alipomwona, alimhurumia. 34Akaenda alipokuwa na akasafisha majeraha yake kwa divai na mafuta, kisha akayafunga. Ndipo akampandisha kwenye punda wake, akampeleka mpaka kwenye nyumba ya wageni na kumtunza. 35Kesho yake, yule Msamaria akachukua dinari mbili#10:35 Dinari mbili ni sawa na mshahara wa kibarua wa siku mbili. akampa yule mwenye nyumba ya wageni na kusema, ‘Mtunze, nami nirudipo nitakulipa gharama yoyote ya ziada uliyotumia kwa ajili yake.’
36“Ni yupi basi miongoni mwa hawa watatu wewe unadhani ni jirani yake yule mtu aliyeangukia mikononi mwa wanyang’anyi?”
37Yule mtaalamu wa Torati akajibu, “Ni yule aliyemhurumia.”
Ndipo Isa akamwambia, “Nenda, ukafanye vivyo hivyo.”
Isa Awatembelea Martha Na Maria
38 Ikawa Isa na wanafunzi wake walipokuwa wakienda Yerusalemu, akaingia kwenye kijiji kimoja ambapo mwanamke mmoja aliyeitwa Martha alimkaribisha nyumbani kwake. 39 Martha alikuwa na mdogo wake aliyeitwa Maria, ambaye aliketi chini miguuni mwa Bwana Isa akisikiliza yale aliyokuwa akisema. 40 Lakini Martha alikuwa akihangaika na maandalizi yote yaliyokuwa yafanyike. Martha akaja kwa Isa na kumuuliza, “Bwana Isa, hujali kwamba ndugu yangu ameniachia kazi zote mwenyewe? Basi mwambie anisaidie.”
41 Lakini Bwana Isa akamjibu, “Martha, Martha, mbona unasumbuka na kuhangaika na mengi? 42 Lakini kunahitajika kitu kimoja tu. Maria amechagua kile kilicho bora, wala hakuna mtu atakayemwondolea.”

वर्तमान में चयनित:

Luka 10: NMM

हाइलाइट

शेयर

कॉपी

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in