Yohana 19

19
Isa Ahukumiwa Kusulubiwa
(Mathayo 27:15-31; Marko 15:6-20; Luka 23:13-25)
1 Ndipo Pilato akamtoa Isa akaamuru apigwe mijeledi. 2Askari wakasokota taji ya miiba, wakamvika Isa kichwani. Wakamvalisha joho la zambarau. 3 Wakawa wanapanda pale alipo tena na tena, wakisema, “Salamu! Mfalme wa Wayahudi!” Huku wakimpiga makofi usoni.
4 Pilato akatoka tena nje akawaambia wale waliokusanyika, “Tazameni, namkabidhi Isa kwenu kuwajulisha kwamba mimi sikumwona ana hatia.” 5 Kwa hiyo Isa akatoka nje akiwa amevaa ile taji ya miiba na lile vazi la zambarau. Pilato akawaambia, “Tazameni, huyu hapa huyo mtu!”
6 Wale viongozi wa makuhani na maafisa walipomwona, wakapiga kelele wakisema, “Msulubishe! Msulubishe!”
Pilato akawaambia, “Mchukueni ninyi mkamsulubishe, mimi sioni hatia juu yake.”
7 Wayahudi wakamjibu, “Sisi tunayo sheria na kutokana na sheria hiyo, hana budi kufa kwa sababu yeye alijiita Mwana wa Mungu.#19:7 Yaani Mwana wa asili moja na Mwenyezi Mungu (Yn 1:1-2), wa kiroho, bali si wa kimwili.
8Pilato aliposikia haya, akaogopa zaidi. 9 Akaingia tena ndani ya jumba la kifalme, akamuuliza Isa, “Wewe umetoka wapi?” Lakini Isa hakumjibu. 10Pilato akamwambia, “Wewe unakataa kuongea na mimi? Hujui ya kuwa nina mamlaka ya kukuachia huru au kukusulubisha?”
11 Ndipo Isa akamwambia, “Wewe hungekuwa na mamlaka yoyote juu yangu kama hungepewa kutoka juu. Kwa hiyo yeye aliyenitia mikononi mwako ana hatia ya dhambi iliyo kubwa zaidi.”
12 Tangu wakati huo, Pilato akajitahidi kutafuta njia ya kumfungua Isa, lakini Wayahudi wakazidi kupiga kelele wakisema, “Ukimwachia huyu mtu, wewe si rafiki wa Kaisari. Mtu yeyote anayedai kuwa mfalme anampinga Kaisari.”
13 Pilato aliposikia maneno haya akamtoa Isa nje tena akaketi katika kiti chake cha hukumu, mahali palipoitwa Sakafu ya Jiwe (kwa Kiebrania paliitwa Gabatha). 14 Basi ilikuwa siku ya Maandalio ya Pasaka, yapata kama saa sita hivi.
Pilato akawaambia Wayahudi, “Huyu hapa mfalme wenu!”
15 Wao wakapiga kelele, “Mwondoe! Mwondoe! Msulubishe!”
Pilato akawauliza, “Je, nimsulubishe mfalme wenu?”
Wale viongozi wa makuhani wakamjibu, “Sisi hatuna mfalme mwingine ila Kaisari.”
16 Ndipo Pilato akamkabidhi Isa kwao ili wamsulubishe.
Kusulubiwa Kwa Isa
(Mathayo 27:32-44; Marko 15:21-32; Luka 23:26-43)
Kwa hiyo askari wakamchukua Isa. 17 Isa, akiwa ameubeba msalaba wake, akatoka kuelekea mahali palipoitwa Fuvu la Kichwa (kwa Kiebrania ni Golgotha). 18 Hapo ndipo walipomsulubisha. Pamoja naye walisulubisha watu wengine wawili, mmoja kila upande wake, naye Isa katikati.
19 Pilato akaamuru tangazo liandikwe na liwekwe juu kwenye msalaba wa Isa, likasema: “isa al-nasiri, mfalme wa wayahudi.”
20 Kwa kuwa mahali hapo Isa aliposulubiwa palikuwa karibu na mjini, Wayahudi wengi walisoma maandishi haya yaliyokuwa yameandikwa kwa lugha za Kiebrania, Kiyunani na Kilatini. 21 Viongozi wa makuhani wa Wayahudi wakapinga, wakamwambia Pilato, “Usiandike ‘Mfalme wa Wayahudi,’ bali andika kwamba mtu huyu alisema yeye ni mfalme wa Wayahudi.”
22Pilato akawajibu, “Nilichokwisha kuandika, nimeandika!”
Mavazi Ya Isa Yagawanywa
23 Askari walipokwisha kumsulubisha Isa, walichukua nguo zake wakazigawa mafungu manne, kila askari fungu lake. Ila walikubaliana wasilichane lile vazi lake kwa maana lilikuwa halina mshono bali limefumwa tangu juu hadi chini. 24 Wakaambiana, “Tusilichane ila tulipigie kura ili kuamua ni nani atalichukua.”
Hili lilitukia ili Maandiko yapate kutimizwa yale yaliyosema,
“Wanagawana nguo zangu,
na vazi langu wanalipigia kura.”
Hayo ndiyo waliyoyafanya wale askari.
25 Wakati huo huo karibu na msalaba wa Isa walikuwa wamesimama mama yake, na dada wa mamaye, na Maria mke wa Klopa, na Maria Magdalene. 26 Isa alipomwona mama yake mahali pale pamoja na yule mwanafunzi aliyempenda wamesimama karibu, akamwambia mama yake, “Mwanamke, huyo hapo ndiye mwanao,” 27 kisha akamwambia yule mwanafunzi, “Nawe huyo hapo ndiye mama yako.” Tangu wakati huo yule mwanafunzi akamchukua mama yake Isa nyumbani kwake.
Kifo Cha Isa
(Mathayo 27:45-56; Marko 15:33-41; Luka 23:44-49)
28 Baada ya haya, Isa hali akijua kuwa mambo yote yamemalizika, alisema ili kutimiza Maandiko, “Naona kiu.” 29 Hapo palikuwa na bakuli lililojaa siki. Kwa hiyo wakachovya sifongo kwenye hiyo siki, wakaiweka kwenye ufito wa mti wa hisopo, wakampelekea mdomoni. 30 Baada ya kuionja hiyo siki, Isa akasema, “Imekwisha.” Akainamisha kichwa chake, akaitoa roho yake.
Isa Achomwa Mkuki Ubavuni
31 Kwa kuwa ilikuwa siku ya Maandalio ya Pasaka, Wayahudi hawakutaka miili ibaki msalabani siku ya Sabato, hasa kwa kuwa hiyo Sabato ingekuwa Sikukuu. Wakamwomba Pilato aamuru miguu ya wale waliosulubiwa ivunjwe ili wafe haraka miili iondolewe kwenye misalaba. 32 Kwa hiyo askari wakaenda wakavunja miguu ya mtu wa kwanza aliyesulubiwa pamoja na Isa na yule mwingine pia. 33Lakini walipomkaribia Isa, wakaona ya kuwa amekwisha kufa, hivyo hawakuvunja miguu yake. 34 Badala yake mmoja wa wale askari akamchoma mkuki ubavuni na mara pakatoka damu na maji. 35 Mtu aliyeona mambo hayo ndiye alitoa ushuhuda, nao ushuhuda wake ni kweli. Anajua kuwa anasema kweli, naye anashuhudia ili pia nanyi mpate kuamini. 36 Kwa maana mambo haya yalitukia ili Maandiko yapate kutimia, yale yasemayo, “Hakuna hata mfupa wake mmoja utakaovunjwa.” 37 Tena Andiko lingine lasema, “Watamtazama yeye waliyemchoma.”
Maziko Ya Isa
(Mathayo 27:57-61; Marko 15:42-47; Luka 23:50-56)
38Baada ya mambo haya, Yusufu wa Arimathaya, aliyekuwa mfuasi wa Isa, ingawa kwa siri kwa sababu ya kuwaogopa Wayahudi, alimwomba Pilato ruhusa ili kuuchukua mwili wa Isa. Pilato alimruhusu, hivyo akaja, akauchukua. 39 Naye Nikodemo, yule ambaye kwanza alimwendea Isa usiku, akaja, akaleta mchanganyiko wa manemane na manukato, yenye uzito wa zaidi ya kilo thelathini#19:39 Zaidi ya kilo 30; tafsiri nyingine zinasema ratili 100, na nyingine ratili 75, ambazo ni kama kilo 34. 40 Wakauchukua mwili wa Isa, wakaufunga katika sanda ya kitani safi pamoja na yale manukato, kama ilivyokuwa desturi ya Wayahudi. 41Basi palikuwa na bustani karibu na mahali pale aliposulubiwa, na pale ndani ya ile bustani palikuwa na kaburi jipya, ambalo halikuwa limezikiwa mtu bado. 42Kwa hiyo, kwa kuwa ilikuwa siku ya Wayahudi ya Maandalio, nalo kaburi hilo lilikuwa karibu, wakamzika Isa humo.

Jelenleg kiválasztva:

Yohana 19: NMM

Kiemelés

Megosztás

Másolás

None

Szeretnéd, hogy a kiemeléseid minden eszközödön megjelenjenek? Regisztrálj vagy jelentkezz be