Yohana 2
2
Arusi Katika Mji wa Kana
1Siku tatu baadaye kulikuwa na arusi katika mji wa Kana huko Galilaya, mama yake Yesu naye pia alikuwapo. 2Yesu na wafuasi wake nao walialikwa. 3Hapo arusini divai ilipungua, mama yake Yesu akamwambia mwanaye, “Hawana divai ya kutosha.”
4Yesu akajibu, “Mama, kwa nini unaniambia mambo hayo? Wakati sahihi kwangu kufanya kazi haujafika bado.”
5Mama yake akawaambia wahudumu wa arusi, “Fanyeni lo lote lile atakalowaambia.”
6Mahali hapo ilikuwepo mitungi mikubwa sita iliyotengenezwa kwa mawe iliyotumiwa na Wayahudi katika desturi yao maalumu ya kunawa.#2:6 desturi yao maalumu ya kunawa Wayahudi walikuwa na sheria za kidini za kunawa maji kwa namna maalumu kabla ya kula, kabla ya kufanya ibada katika Hekalu, na pia nyakati zingine maalumu. Kila mtungi mmoja ulikuwa na ujazo wa lita 80 au 120.#2:6 lita 80 au 120 Kwa maana ya kawaida, “metretas 2 au 3”.
7Yesu akawaambia wale wahudumu, “Ijazeni maji hiyo mitungi.” Nao wakaijaza maji mpaka juu.
8Kisha akawaambia, “Sasa choteni hayo maji kiasi na mumpelekee mkuu wa sherehe.” Nao wakafanya kama walivyoambiwa. 9Mkuu wa sherehe akayaonja yale maji, ambayo tayari yamegeuka na kuwa divai. Naye hakujua wapi ilikotoka hiyo divai, bali wahudumu walioleta yale maji wao walijua. Akamwita bwana arusi 10na kumwambia, “Watu wanapoandaa huleta kwanza divai iliyo bora zaidi. Baadaye, wageni wanapokuwa wametosheka, huleta divai iliyo na ubora pungufu. Lakini wewe umeandaa divai bora zaidi hadi sasa.”
11Ishara hii ilikuwa ya kwanza aliyoifanya Yesu katika mji wa Kana ya Galilaya. Kwa hili Yesu alionesha ukuu wake wa kimungu, na wafuasi wake wakamwamini.
12Kisha Yesu akashuka kwenda katika mji wa Kapernaumu. Mama yake, ndugu zake, na wafuasi wake nao walienda pamoja naye. Wote wakakaa huko kwa siku chache.
Yesu Asafisha Eneo la Hekalu
(Mt 21:12-13; Mk 11:15-17; Lk 19:45-46)
13Kipindi hicho wakati wa kusherehekea Pasaka ya Wayahudi ulikaribia, hivyo ikampasa Yesu kwenda Yerusalemu. 14Katika eneo la Hekalu aliwaona watu wakiuza ng'ombe, mbuzi na njiwa. Aliwaona wengine wakikalia meza na kufanya biashara ya kubadili fedha za watu. 15Yesu akatengeneza kiboko kwa kutumia vipande vya kamba. Kisha akawafukuza watu wote, kondoo na ng'ombe watoke katika eneo la Hekalu. Akazipindua meza za wafanya biashara wa kubadilisha fedha na kuzitawanya fedha zao. 16Baada ya hapo akawaambia wale waliokuwa wanauza njiwa, “Viondoeni humu vitu hivi! Msiifanye nyumba ya Baba yangu kuwa mahali pa kununua na kuuza!”
17Haya yaliwafanya wafuasi wake kukumbuka maneno yaliyoandikwa kwenye Maandiko: “Upendo wangu mkuu kwa Hekalu lako utaniangamiza.”#Zab 69:9
18Baadhi ya Wayahudi wakamwambia Yesu, “Tuoneshe muujiza mmoja kama ishara kutoka kwa Mungu. Thibitisha kwamba unayo haki ya kufanya mambo haya.”
19Yesu akajibu, “Bomoeni hekalu hili nami nitalijenga tena kwa muda wa siku tatu.” 20Wakajibu, “Watu walifanya kazi kwa miaka 46 kulijenga Hekalu hili! Je! ni kweli unaamini kwamba unaweza kulijenga tena kwa siku tatu?”
21Lakini Yesu aliposema “hekalu hili”, alikuwa anazungumzia mwili wake. 22Baada ya kufufuliwa kutoka katika wafu, wafuasi wake wakakumbuka kwamba alikuwa ameyasema hayo. Hivyo wakayaamini Maandiko, na pia wakayaamini yale aliyoyasema Yesu.
23Yesu alikuwa Yerusalemu kwa ajili ya sikukuu ya Pasaka. Watu wengi wakamwamini kwa sababu waliona ishara na miujiza alioitenda. 24Lakini Yesu hakuwaamini wao, kwa sababu alijua jinsi watu wote wanavyofikiri. 25Hakuhitaji mtu yeyote amwambie jinsi mtu fulani alivyo. Kwa sababu alikwishamjua tayari.
Attualmente Selezionati:
Yohana 2: TKU
Evidenziazioni
Condividi
Copia
Vuoi avere le tue evidenziazioni salvate su tutti i tuoi dispositivi?Iscriviti o accedi
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi
Toleo la Awali
© 2017 Bible League International