Luka 24
24
Yesu Amefufuka Kutoka Mauti
(Mt 28:1-10; Mk 16:1-8; Yh 20:1-10)
1Asubuhi mapema sana siku ya Jumapili, wanawake walikwenda kaburini ulikolazwa mwili wa Yesu. Walibeba manukato yanayonukia vizuri waliyoyaandaa. 2Walikuta jiwe kubwa lililokuwa limeziba mlango wa kaburi limevingirishwa kutoka kwenye mlango wa kaburi. 3Waliingia kaburini, lakini hawakuuona mwili wa Bwana Yesu. 4Hawakulielewa hili. Walipokuwa wangali wanashangaa, watu wawili waliovaa mavazi yaliyong'aa walisimama pembeni mwao. 5Wanawake waliogopa sana. Waliinama nyuso zao zikaelekea chini. Wale watu wakawaambia, “Kwa nini mnamtafuta aliye hai hapa? Hapa ni mahali pa waliokufa. 6Yesu hayuko hapa. Amefufuka kutoka kwa wafu. Mnakumbuka alivyosema alipokuwa Galilaya? 7Alisema kwamba, ‘Mwana wa Adamu lazima atatolewa kwa mamlaka ya watu wenye dhambi, lazima atauawa msalabani na kufufuka kutoka kwa wafu siku ya tatu.’” 8Ndipo wanawake wakakumbuka Yesu alivyosema.
9Wanawake wakaondoka kaburini na kurudi kwa mitume kumi na mmoja na wafuasi wengine. Waliwaeleza kila kitu kilichotokea kaburini. 10Wanawake hawa walikuwa Mariamu Magdalena, Yoana, na Mariamu, mama yake Yakobo na wanawake wengine. Waliwaambia mitume kila kitu kilichotokea. 11Lakini mitume hawakuamini yale waliyosema. Ilionekana kama upuuzi. 12Lakini Petro alinyanyuka na kukimbia kwenda kaburini kuona. Alitazama ndani, lakini aliona nguo tu iliyotumika kuufunga mwili wa Yesu. Petro aliondoka kwenye kaburi akarudi nyumbani alikokuwa anakaa, akijiuliza nini kilichotokea.#24:12 Nakala chache za Kiyunani hazina mstari huu.
Njiani Kwenda Emausi
(Mk 16:12-13)
13Siku hiyo hiyo, wafuasi wawili#24:13 wafuasi wawili Kwa maana ya kawaida, “Miongoni mwa wafuasi”. Ni wazi kutokana na simulizi kuwa wote wawili ni wafuasi wa Yesu, lakini mmoja wao tu ndiye anayetajwa jina (mstari wa 18). Inawezekana akawa ndiye Kleopa, anayeelezwa katika Yh 19:25 kama mume wa mmoja wa wanawake anayeitwa Mariamu. Inawezekama mfuasi wa pili anayezungumzwa hapa ndiye huyu Mariamu. wa Yesu walikuwa wanakwenda kwenye mji mdogo uitwao Emausi, uliokuwa yapata kilomita kumi na mbili#24:13 kilomita kumi na mbili Kwa Kiyunani umbali huo ni sawa na “stadia 60”. kutoka Yerusalemu. 14Walikuwa wanazungumza kuhusu mambo yote yaliyotokea. 15Walipokuwa wakizungumza, wakijadiliana juu ya mambo haya, Yesu mwenyewe aliwasogelea na akawa anatembea nao. 16Lakini hawakuruhusiwa kumtambua. 17Yesu akawauliza, “Ni mambo gani ninayosikia mnajadiliana mnapotembea?”
Wale wafuasi wawili wakasimama, sura zao zilionekana zenye huzuni. 18Mmoja wao, aliyeitwa Kleopa akasema, “Lazima wewe ni mtu pekee katika Yerusalemu ambaye hujui yaliyotokea huko.”
19Yesu akasema, “Unasema kuhusu nini?”
Wakasema, “Ni kuhusu Yesu, kutoka Nazareti, alikuwa nabii mkuu mbele za Mungu na watu wote. Alisema na kutenda mambo makuu mengi. 20Lakini viongozi wetu na viongozi wa makuhani walimtoa ili ahukumiwe na kuuawa. Wakampigilia msalabani. 21Tulitegemea kuwa ndiye atakayeiweka huru Israeli. Lakini sasa haya yote yametokea.
Na sasa kitu kingine: Imekuwa ni siku tatu tangu alipouawa, 22lakini leo baadhi ya wanawake kutoka kwenye kundi letu walituambia jambo la kushangaza. Mapema asubuhi hii walikwenda kaburini ambako mwili wa Yesu ulilazwa. 23Lakini hawakuuona mwili wake pale. Walikuja na kutuambia kuwa wamewaona malaika. Malaika waliwaambia Yesu yu hai! 24Hivyo baadhi ya watu walio katika kundi letu walikwenda kaburini pia. Ilikuwa kama wanawake walivyosema. Waliliona kaburi, lakini hawakumwona Yesu.”
25Ndipo Yesu akawaambia, “Ninyi ni wajinga na wazito wa kuyakubali yale waliyoandika manabii. 26Manabii waliandika kwamba Masihi lazima ateseke kwa mambo haya kabla hajaingia katika utukufu wa ufalme wake.” 27Kisha akaanza kufafanua kila kitu walichosema manabii kuhusu yeye. Alianzia katika vitabu vya Musa na kusema yale waliyosema manabii kuhusu yeye.
28Wakakaribia mji wa Emausi, na Yesu akafanya kama vile alikuwa anaendelea mbele. 29Lakini walimtaka akae, wakamsihi: “Kaa nasi. Tayari ni usiku. Mchana unakaribia kwisha.” Hivyo aliingia ndani kukaa nao.
30Alipokuwa mezani pamoja nao ili kula chakula cha usiku, Yesu akachukua mkate na kushukuru. Kisha akaumega na kuwapa. 31Baada ya kufanya hivyo, wafuasi wale wawili wakaruhusiwa kumtambua. Lakini walipojua yeye ni nani, alitoweka. 32Wakasemezana, “Alivyokuwa anazungumza nasi tulipokuwa barabarani, tulijisikia kama moto unawaka ndani yetu. Ilitusisimua sana alipotufafanulia maana halisi ya Maandiko!”
33Hivyo wafuasi wale wawili wa Bwana Yesu wakasimama na kurudi Yerusalemu haraka. Walipofika Yerusalemu waliwakuta mitume kumi na mmoja wamekusanyika pamoja na wafuasi wengine wa Bwana Yesu. 34Kundi likawaambia wale wafuasi wawili, “Hakika Bwana amefufuka kutoka kwa wafu! Alimtokea Simoni.”
35Ndipo wafuasi wawili wakaeleza kilichotokea barabarani. Wakaeleza jinsi walivyomtambua Yesu aliposhiriki mkate pamoja nao.
Yesu Awatokea Wafuasi Wake
(Mt 28:16-20; Mk 16:14-18; Yh 20:19-23; Mdo 1:6-8)
36Wakati wafuasi wawili wakiwa bado wanawaeleza mambo haya wafuasi wengine, Yesu mwenyewe akaja na kusimama katikati yao. Akawaambia, “Amani iwe kwenu.”
37Wafuasi walishituka na wakaogopa. Walidhani wanaona mzimu. 38Lakini Yesu akasema, “Kwa nini mnaogopa? Na kwa nini mnakitilia mashaka kile mnachokiona? 39Angalieni mikono na miguu yangu. Hakika ni mimi. Niguseni. Mtaweza kuona kuwa nina mwili wenye nyama na mifupa; mzimu hauna mwili kama huu.”
40Mara baada ya Yesu kusema haya, aliwaonesha mikono na miguu yake. 41Wafuasi walishangaa na kufurahi sana walipoona kuwa Yesu alikuwa hai. Kwa kuwa bado walikuwa hawaamini wanachokiona, akawaambia, “Mna chakula chochote hapa?” 42Wakampa kipande cha samaki aliyepikwa. 43Wafuasi wake wakiwa wanaangalia akakichukua na kukila.
44Yesu akawaambia, “Mnakumbuka nilipokuwa pamoja nanyi? Nilisema kila kitu kilichoandikwa kuhusu mimi katika Sheria ya Musa, vitabu vya manabii na Zaburi lazima kitimilike.”
45Kisha Yesu akawafafanulia Maandiko ili waelewe maana yake halisi. 46Yesu akawaambia, “Imeandikwa kuwa Masihi atauawa na atafufuka kutoka kwa wafu siku ya tatu. 47-48Mliona mambo haya yakitokea, ninyi ni mashahidi. Na maandiko yanasema inawapasa mwende na kuwahubiri watu kuwa ni lazima wabadilike na kumgeukia Mungu, ili awasamehe. Ni lazima mwanzie Yerusalemu na mhubiri ujumbe huu kwa jina langu kwa watu wa mataifa yote. 49Kumbukeni kwamba nitamtuma kwenu yule ambaye Baba yangu aliahidi. Kaeni jijini mpaka mtakapopewa nguvu hiyo kutoka mbinguni.”
Yesu Arudi Mbinguni
(Mk 16:19-20; Mdo 1:9-11)
50Yesu akawaongoza wafuasi wake kutoka nje ya Yerusalemu hadi karibu na Bethania. Akanyenyua mikono yake na kuwabariki wafuasi wake. 51Alipokuwa anawabariki, alitenganishwa nao na kuchukuliwa mbinguni. 52Wafuasi wake walimwabudu, kisha wakarudi Yerusalemu wakiwa na furaha sana. 53Walikuwa katika Hekalu wakati wote, wakimsifu Mungu.
Attualmente Selezionati:
Luka 24: TKU
Evidenziazioni
Condividi
Copia
Vuoi avere le tue evidenziazioni salvate su tutti i tuoi dispositivi?Iscriviti o accedi
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi
Toleo la Awali
© 2017 Bible League International