Mwanzo Utangulizi

Utangulizi
Neno “Mwanzo” linatokana na neno la Kiyunani “Geneseos” ambalo maana yake ni “Asili”, “Chimbuko”, au “Chanzo”; linatokana na tafsiri ya Maandiko Matakatifu kwa Kiyunani ijulikanayo kama “Septuagint”. Kitabu hiki kinaeleza mwanzo wa ulimwengu, mwanzo wa mwanadamu (yaani mwanamke na mwanaume), mwanzo wa dhambi ya mwanadamu, mwanzo wa ahadi na mpango wa Mwenyezi Mungu wa wokovu, na uhusiano wa kipekee kati ya Ibrahimu na Mwenyezi Mungu. Pia kinaeleza kuhusu watu mahsusi wa Mwenyezi Mungu, na mipango yake katika maisha yao. Baadhi ya watu hawa ni Adamu na Hawa, Nuhu, Ibrahimu, Isaka, Yakobo, Yusufu na ndugu zake, na wengine wengi.
Mwanzo ni kitabu cha kwanza miongoni mwa vitabu vitano vinavyoitwa “Vitabu vya Musa”, vilivyo mwanzoni mwa Maandiko Matakatifu. Vitabu hivi vinaitwa pia “Torati” kwa sababu ni katika vitabu hivi yameandikwa maagizo na sheria za Mwenyezi Mungu kwa Waisraeli. Kitabu cha Mwanzo kinaeleza jinsi Mwenyezi Mungu aliumba vitu vyote, anguko la mtu wa kwanza, jinsi Mwenyezi Mungu alivyoendelea kujifunua kwa wanadamu, na mpango wa Mwenyezi Mungu wa ukombozi kwa mwanadamu aliyeanguka. Aidha, kitabu hiki kinaeleza jinsi Israeli walivyofanywa kuwa taifa teule la Mwenyezi Mungu.
Mwandishi
Waumini wa dini ya Kiyahudi na ya Kikristo wanashikilia kuwa mwandishi ni Musa.
Kusudi
Kumfunulia mwanadamu mwanzo wa kuumbwa kwa mbingu na nchi, na vyote vilivyomo. Kuonesha kuwa Mwenyezi Mungu ndiye Muumbaji pekee.
Mahali
Katika Ghuba ya Sinai, Waisraeli walipokuwa jangwani.
Tarehe
Mnamo 1450–1410 K.K.
Wahusika Wakuu
Adamu, Hawa, Nuhu, Ibrahimu, Sara, Isaka, Rebeka, Yakobo, Yusufu.
Wazo Kuu
Kuelezea kuhusu uumbaji, kuanguka kwa mwanadamu, na ahadi ya ukombozi wa mwanadamu kupitia kwa Isa Al-Masihi. Kila msingi mkuu wa imani katika Maandiko una mizizi yake katika Mwanzo kama asili (kitu kamili), au mfano, au ufunuo halisi.
Mambo Muhimu
Uumbaji, kuanguka kwa mwanadamu, ahadi za ukombozi wa mwanadamu kupitia kwa Isa Al-Masihi.
Yaliyomo
Kuumbwa kwa ulimwengu na mwanadamu (1:1–2:25)
Kuanguka kwa mwanadamu na matokeo ya dhambi (3:1–5:32)
Habari za Nuhu (6:1–9:29)
Kutawanywa kwa mataifa (10:1–11:32)
Maisha ya Ibrahimu (12:1–25:18)
Isaka na jamaa yake (25:19–27:46)
Yakobo na wanawe (28:1–37:1)
Yusufu na ndugu zake (37:2-36)
Yuda na Tamari (38:1-30)
Maisha ya Yusufu (39:1–50:26).

ハイライト

シェア

コピー

None

すべてのデバイスで、ハイライト箇所を保存したいですか? サインアップまたはサインインしてください。